2016-04-29 14:57:00

Acheni unafiki!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe, 29 Aprili 2016 amewataka waamini kuachana kabisa na maisha ya undumila kuwili kwa kutembea katika giza la maisha ambako huko hakuna ukweli wa Mungu na badala yake kuambata mwanga unaojikita katika upendo, huruma na msamaha wa Mungu. Waamini wawe ni mashuhuda wa mwanga kwa kuondokana na maisha ya dhambi na pale wanapotumbukia dhambini basi wawe na ujasiri wa kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, wakisema kuwa hawana dhambi ni waongo na wala ukweli haumo ndani mwao! Mapambano dhidi ya dhambi ni endelevu na ushindi unaweza kupatikana tu kwa njia ya neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Waamini waache tabia ya kuwa na maisha ya undumila kuwili kwani ni hatari kabisa. Ibilisi ni baba wa maovu yote duniani, changamoto kwa waamini kujenga na kuimarisha muungano wao na Kristo, ili kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Waamini wajitahidi kuwa wakweli na waaminifu katika maisha yao, changamoto kwa kila mtu awaye yote!

Baba Mtakatifu anasema, Kristo anawaalika waja wake kwa maneno yenye upendo kwa kuwataka wajifunze kutoka kwake kwani Yeye ni mnyenyekevu wa moyo na mzigo wake ni mwepesi kuchukua! Anawataka waja wake wasitende dhambi, lakini wakianguka dhambini kutokana na udhaifu wa kibinadamu, wasikate tamaa bali waoneshe ujasiri wa kusimama tena na kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, kwani wanaye Mwombezi, Yesu Kristo anayewaombea kila siku mbele ya Mwenyezi Mungu, Kristo ni mtakatifu wa Mungu anayewahesabia haki waja wake kwa kuwakirimia neema.

Waamini waje na ujasiri wa kutubu dhambi zao kwani huruma ya Mungu ndio kielelezo cha ukuu wake na chemchemi ya nguvu na kwamba, daima anawasubiri watoto wake kumwendea kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani, ili kutembea tena katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Neema ya Mungu inaweza kumhesabia mdhambi kuwa na haki mbele ya Mungu, kwani Mungu anahurumia na kusamehe na kwamba anatambua udhaifu na mapungufu ya watoto wake. Neno la Mungu linaonesha ukweli unaopaswa kufumbatwa katika maisha ya Mkristo, kwa kuambata toba, wongofu na ukweli wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.