2016-04-28 15:09:00

Sherehe ya Pasaka iwe ni kielelezo cha mshikamano wa upendo!


Makanisa ya Mashariki yanayofuata kalenda ya Juliani yanaadhimisha Pasaka, Mei, Mosi, 2016. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli katika ujumbe wake kwa waamini katika maadhimisho haya anawakumbusha kwamba, Pasaka kwa waamini wa Kanisa la Kiorthodox si kukimbia majukumu na ukweli wa mambo bali kusimama kidete kumkiri na kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa watu, kielelezo cha ushindi dhidi ya dhambi na kifo na kwamba, anaendelea kukaa pamoja na wafuasi wake hadi utimilifu wa nyakati!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasikitika kusema kwamba, leo hii, vitendo vya kigaidi, vita na mambo yanayofumbata utamaduni wa kifo yanaendelea kutishia usalama na maisha ya binadamu; yanasababisha maafa na majanga makubwa, kiasi cha kuwakosesha watu matumaini ya maisha bora zaidi. Licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini kuna masumbuko na mahangaiko makubwa katika nyoyo za watu. Kumbe, viongozi wa Makanisa, Kisiasa na Kijamii wanayo dhamana ya upendo kuhakikisha kwamba, wanawasaidia watu kuondokana na hali hii tete, kwa kuonesha ushuhuda wa upendo kwa jirani!

Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu n ikiini cha imani ya Kikristo, bila Fumbo hili, imani ya Kikristo ni utupu. Neno wa Mungu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake amemkirimia mwanadamu ile sura na mfano wa Mungu baada ya kuchafuliwa na madoa ya dhambi na ukosefu wa utii. Sherehe ya Pasaka ya Bwana ni ushindi wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika vita ya kidini na ukosefu wa haki msingi za binadamu.

Wakristo wanatangaza na kushuhudia Ufufuko wa Kristo dhidi ya kifo, kwani Neno wa Mungu ni chemchemi ya maisha na mwanga wa imani na matumaini yanayong’ara katika maisha na utume wa Kanisa na kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini cha maisha, utume na tasaufi ya Kanisa la Kiorthodox. Fumbo la Ufufuko linaunganisha kwa namna ya pekee imani, maadili, ibada na sheria za Kanisa. Kutokana na imani hii, Fumbo la Ekaristi Takatifu linaadhimishwa kwa furaha na imani timilifu, kwa kukumbuka Siku ya kwanza ya Juma, Yesu Kristo alipofufuka kutoka kwa wafu!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakaza kusema Fumbo la Uumbaji linapata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kutangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka katika maisha yao ya kila siku hadi miisho ya dunia. Mama Kanisa anaendelea kuishi Fumbo la Msalaba ambalo linafumbatwa katika Ufufuko kwa kuwahamasisha waamini kuwa ni mwanga wa Kristo Mfufuka, ili kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano kati ya watu, kwani kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Kristo amewaunganisha walimwengu kuwa wamoja! Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume linapaswa kujikita katika mchakato wa upatanisho, ili kupata maisha mapya yanayosimikwa katika ukweli, ili kuwa sehemu ya watu wa Mungu.

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao kwani vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chchote kilichofanyika. Ndani mwake ndimo mlimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Huu ndio ujumbe ambao Patriaki Bartolomeo wa kwanza anataka kuipatia familia Mungu wakati huu wa maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa Makanisa ya Mashariki, ili kuunganisha furaha na machungu yanayomwandama mwanadamu ili kuwaonjesha upendo na sadaka ya maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.