2016-04-27 08:25:00

Wanasayansi na viongozi wa dini wanakutana Vatican kuangalia tiba!


Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa kushirikiana na Mfuko wa “Stem for Life” kuanzia tarehe 28 – 30 Aprili 2016, linafanya mkutano wa tatu kimataifa unaopania pamoja na mambo mengine kupembua kwa kina na mapana tiba inayopatikana kwa kutumia chembe chembe za mwili wa binadamu katika kutibu magonjwa na kupunguza mateso ya watu duniani. Huu ni mkutano unaopembua jinsi ambavyo: Imani, sayansi, teknolojia, habari na mawasiliano yanavyoweza kuleta mabadiliko makubwa katika mchakato wa tiba ya mwanadamu nyakati hizi za maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Wajumbe wa mkutano huu wanatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Mkutano huu kwa namna ya pekee unaangalia jinsi ya kutibu ugonjwa wa Saratani miongoni mwa maskini duniani; magonjwa ya watoto pamoja na magonjwa yanayowakumba watu wenye umri mkubwa zaidi. Dr. Robin Smith, Rais wa Mfuko wa “Stem for Life” anasema, hadi sasa kuna majaribio zaidi ya 30, 000 ya kutumia chembe hai za binadamu kama sehemu ya tiba. Mkutano huu unataka kutoa matumaini kwa wagonjwa kwamba, chembe chai za binadamu zina uwezo kusaidia kutoa tiba sanjari na kupunguza mateso na mahangaiko ya wagonjwa wengi duniani, hususan wale wanaotoka katika nchi maskini zaidi duniani!

Kardina Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni changamoto kwa wataalam na mabingwa wa sekta ya afya kutafuta tiba muafaka kwa magonjwa yanayomwandama mwanadamu sanjari na kuwapatia matumaini ya maisha, maskini wanaoishi katika nchi zinazoendelea duniani. Tiba ya chembe za binadamu inapaswa sasa kuwafikia watu wengi zaidi badala ya kuendelea kukaa kwenye maabara na kliniki.

Kwa upande wake Monsinyo Tomasz Trafny, afisa mwandamizi wa idara ya sayansi na imani kutoka Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema, tukio hili ni muhimu sana katika kukoleza majadiliano kati ya sayansi, teknolojia na imani; wanasayansi na viongozi wa kidini kuangalia jinsi ambavyo kwa pamoja wanaweza kusaidia mchakato wa tiba makini kwa wagonjwa kwa kutumia maendeleo ya sayansi na teknolojia! Hii ni fursa ya kuhamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuhusu tiba inayojikita katika chembe hai za binadamu pamoja na kutafuta fedha za kuendeleza tafiti na tiba kwa wagonjwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.