2016-04-27 15:03:00

Wafiadini 38 kutoka Albania kutangazwa kuwa Wenyeheri!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, Jumanne, tarehe 26 Aprili 2016, ameridhia tamko la kutambua muujiza uliofanywa kwa maombezi ya Mwenyeheri Padre Alfonso Maria Fusco, muasisi wa Shirika la Watawa wa Mtakatifu Yohane Baptisti, aliyezaliwa kunako tarehe 23 Machi 1839 na kufariki dunia tarehe 6 Februari 1910.

Baba Mtakatifu pia ameridhia tamko la kutambua miujiza iliyotendwa kwa maombezi ya watumishi wa Mungu kumi na mmoja, kati yao ni Mtumishi wa Mungu Maria Montserrat Grases Garcia, mwamini mlei kutoka Shirika la Opus Dei aliyezaliwa tarehe 10 Juali 1941 na kufariki dunia hapo tarehe 26 Machi 1959. Kanisa limetambua muujiza uliotendwa kwa maombezi ya Mtumishi wa Mungu Padre Giovanni Sullivan, Mtawa wa Shirika la Wayesuit, aliyezaliwa kunako tarehe 8 Mei 1861 na kufariki dunia tarehe 19 Februari 1933. Kanisa limeridhia ushuhuda wa imani uliooneshwa na Mtumishi wa Mungu Vincenzo Prennushi wa Shirika la Ndugu Wafranciskani Wakapuchini, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Durazzo, nchini Albania pamoja na wenzake 37 waliouwawa kati ya mwaka 1945 na mwaka 1974.

Kanisa limetambua ushuhuda ulioneshwa na Giuseppe Antòn Gòmez na wenzake watatu, Mapadre wa Shirika la Mtakatifu Benedikto, waliouwawa kunako mwaka 1936. Mama Kanisa anaridhika na ushuhuda wa imani ulioneshwa na Mtumishi wa Mungu Padre Tommaso Choe Yang-Eop aliyezaliwa tarehe Mosi Machi 1821 na kufariki dunia tarehe 15 Juni 1861.

Katika mwendelezo huo huo, Kanisa limetambua ushuhuda wa imani uliodhihirishwa na Mtumishi wa Mungu Padre Sosio Del Prete wa Shirika la Ndugu Wafranciskani Wakapuchini na muasisi wa Shirika Watumishi Wadogo wa Kristo Mfalme aliyezaliwa tarehe 28 Desemba 1885 na kufariki dunia tarehe 27 Januari 1952. Kanisa pia limetambua ujasiri wa kiimani ulioshuhudiwa na Padre Venanzio Katarzyniec, Mtawa wa Shirika la Wafranciskani, aliyezaliwa kunako tarehe 7 Oktoba 1889 na kufariki dunia tarehe 31 Machi 1921.

Mama Kanisa ametambua na kuridhia ushuhuda wa imani ulioneshwa na Mtumishi wa Mungu Maria Mshauri wa Roho Mtakatifu, muasisi wa Shirika la Watawa wa Bikira Maria Mteswa, aliyezaliwa kunako tarehe 5 Januari 1845 na kufariki dunia 11 Januari 1900. Kanisa pia limetambua fadhila ya ushuhuda kutoka kwa Mtumishi wa Mungu Maria wa B.M. wa Umwilisho; mwanzilishi wa Shirika la Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Francisko aliyezaliwa kunako tarehe 24 Machi 1840 na kufariki dunia tarehe 24 Novemba 1917.

Kanisa limeridhia na fadhila ya ushuhuda ulioneshwa na Mtumishi wa Mungu Laura Baraggia, mwanzilishi wa Shirika la Watawa wa Familia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, aliyezaliwa Mei Mosi, 1851 na kufariki dunia tarehe 18 Desemba 1923. Mwishoni, Kanisa limetambua na kuridhia ushuhuda wa imani ulioneshwa na Mtumishi wa Mungu Ilia Corsaro, muasisi wa Shirika la Wamissionari Wadogo wa Ekaristi Takatifu, aliyezaliwa tarehe 4 Oktoba 1897 na kufariki dunia tarehe 23 Machi 1977.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.