2016-04-27 09:14:00

Papa Francisko anataka kupangusa machozi ya wanao huzunika!


Katika kipindi cha Siku 40 Yesu aliwaimarisha mitume wake katika imani, matumaini na mapendo na baadaye “Yesu alipaa mbinguni, amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi”. Sherehe ya Kupaa Bwana mbinguni, hapa mjini Vatican itaadhimishwa hapo tarehe 5 Mei 2016 sanjari na mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko wa kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha, kielelezo cha imani tendaji!

Baba Mtakatifu katika Sherehe hii, majira ya saa 12:00 za Jioni kwa saa za Ulaya, anatarajiwa kuongoza  Ibada ya Mkesha wa Sala kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ili “kupangusa machozi” ya watu wanaoteseka kiroho na kimwili, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kuna wazazi na walezi ambao wamewapoteza watoto wao kutokana na magonjwa, ajali na hali mbaya ya maisha; mambo yanayochangia uwepo wa Fumbo la Msalaba katika maisha ya ndoa na familia. Kuna watu ambao hawana tena fursa za ajira, kiasi kwamba, wanashindwa kuhudumia familia zao kutokana na hali ngumu ya maisha na umaskini!

Kuna kinzani na mipasuko ya kifamilia, baba hataki tena kumwona mkewe ambaye hapo awali alikuwa ni asali wa moyo wake! Leo hii amegeuka kuwa shetani na ibilisi wa maisha yake. Kuna wazee wanaoteseka kutokana na upweke hasi, magonjwa pamoja na kutelekezwa na jamii, kwani hawa hawana tena cha kuweza kuchangia katika uzalishaji na utoaji wa huduma, wameegeshwa pembezoni mwa jamii kama magari mabovu! Kuna vijana ambao wamekengeuka, leo hii wamegeuka kuwa ni “mateja” wa matumizi haramu ya dawa za kulevya”, mambo yanayowatesa na kuwahuzunisha sana wazazi ambao waliwekeza sana katika elimu ya watoto wao, lakini leo hii ni watu wanaotoka udende siku nzima!

Kuna watu ambao kutokana na magonjwa, hali ngumu ya maisha na ukosefu wa haki, amani na usalama hawaoni tena thamani ya maisha, kwani daima wanakiona kifo mbele yao. Zote hizi ni dalili za kukosa imani, matumaini na mapendo! Baba Mtakatifu Francisko anataka kuwakumbuka wote hawa katika mkesha huu wa sala, Mama Kanisa anapoadhimisha Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni! Kuwafariji wenye huzuni ni moja ya matendo ya huruma. Baba Mtakatifu anataka kuwatia shime watu wote wanaoteseka kwa kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Siracusa, ili aweze kuwasimamia na kuwasindikiza wote wanaohuzunika kutokana na sababu mbali mbali za maisha, hasa mwezi Mei ambao Kanisa linautoa kwa heshima ya Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.