2016-04-27 10:34:00

Mkiona na kuguswa na mahangaiko ya jirani, tendeni kwa huruma na mapendo!


Mfano wa Msamaria mwema ni kielelezo makini cha kumwilisha Amri ya Upendo kwa Mungu na kwa jirani kwa njia ya matendo ya huruma kwa maskini kama njia ya kujipatia maisha ya uzima wa milele. Ni mfano hai unaotolewa na Yesu Kristo wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii ni sehemu ya Katekesi ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumatano, tarehe 27 Aprili 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anasema, Sheria ya Mungu inawataka waamini kutoa msaada kwa wahitaji, mwaliko kwa wakleri na waamni wote katika ujumla wao kumwilisha huruma ya Mungu kwa njia ya upendo kwa jirani na kwamba ibada ya kweli inajikita katika huduma ya upendo makini kwa jirani! Hawa ni watu wanaoteseka kutokana na vita, njaa, umaskini na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Familia ya Mungu haiwezi kufumbia macho mateso na mahangaiko ya watu hawa kama watazamaji bila ya kujishughulisha kikamilifu!

Kutoguswa na mahangaiko ya binadamu ni sawa na kumpuuza Mwenyezi Mungu katika maisha! Watu wajifunze kuona na kutenda. Mfano wa Msamaria mwema ni kielelezo makini cha huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; Mungu anayeguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watoto wake na daima yuko tayari kuwasaidia kwa kuwaonjesha upendo mkamilifu. Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na jirani inajikita katika matendo yanayotafsiriwa kuwa ni huduma kwa jirani kiasi hata cha kujisadaka kwa ajili ya wengine.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwishoni mwa Mfano wa Msamaria mwema, Yesu anaonesha kwamba, Jirani si yule mhitaji aliyekuwa amekung’utwa na majambazi pale njiani, bali yule Msamaria mwema aliyeona shida na mahangaiko ya yule mtu, akajibu kwa huruma na upendo. Huu ndio mwelekeo ambao Yesu anawataka wafuasi wake kuutekeleza katika maisha yao, yaani kuona na kuguswa na mahangaiko ya wengine, tayari kuyafanyia kazi kwa njia ya huduma ya upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Yesu ni kielelezo makini cha Msamaria mwema anayejitaabisha kuganga na kuponya madonda ya mwanadamu; kwa kuuiga huruma na upendo wake, Wakristo wanaonesha kuwa kweli ni wafuasi wa Yesu si tu kwa maneno bali kwa njia ya matendo yanayomwilishwa katika huduma makini! Baba Mtakatifu amewaombea wote huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao ya kila siku!

Waamini wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuwa na jicho la huruma tayari kuona, kuguswa na mahangaiko ya jirani, ili kuyafanyia kazi, kama kielelezo makini cha ujirani mwema. Waamini wajifunze kutembea na kushikamana katika: imani, matumaini na mapendo, ili kuweza kusaidiana kama Wasamaria wema. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Wayesuiti cha Mtakatifu Yosefu, cha Beirut, nchini Lebanon, wanapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka 140 tangu kuanzishwa kwa Chuo kikuu hiki, changamoto ya kuendelea kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya upatanisho, msamaha na upendo, ili kweli huruma ya Mungu iweze kung’ara katika mapaji ya nyuso zao!

Waamini wafarijike na maneno ya Yesu kwamba, kila tendo walilomtendea mmojawapo wa wadogo hawa amemtendea Yesu mwenyewe! Waamini waendelee kujichotea rehema kamili kwa kupita kwenye Lango la Huruma ya Mungu baada ya toba, wongofu wa ndani na sala, chachu inayoimarisha imani kwa Kristo Yesu, tayari kuambata maisha mapya na kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka! Hija za Mwaka Mtakatifu ziwakirimie waamini matunda mema ya maisha ya kiroho kwa ajili yao wenyewe, ndugu na jirani zao.

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea Mapadre walezi kutoka Seminari kuu ambazo ziko chini ya Chuo kikuu cha Kipapa cha Urbaniana wanaohudhuria semina maalum hapa mjini Roma. Amewataka waamini kuwa waaminifu kwa ahadi zao za Ubatizo, daima wakishuhudia ile furaha ya kukutana na Yesu katika maisha yao! Wagonjwa wavumilie mateso kwa kumwangalia Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili mateso haya yawe ni chemchemi ya wokovu! Wanandoa wapya wawe na upendo unaosamehe na kuvumilia yote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.








All the contents on this site are copyrighted ©.