2016-04-27 15:24:00

Huruma ya Mungu inaokoa ulimwengu!


Askofu mkuu William Goh Seng Chye wa Jimbo kutoka Singapore katika Waraka wake wa kichungaji Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema, watu wanahitaji huruma ya Mungu kwa nyakati hizi, pengine kuliko hata nyakati zilizotangulia katika historia ya mwanadamu. Leo hii kuna maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, lakini kwa bahati mbaya, huruma ya Mungu imetundikwa pembezoni kabisa mwa vipaumbele vya mwanadamu.

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, vitendo vya kigaidi, vita, nyanyaso, kinzani na mipasuko ya kijamii inaendelea kushamiri kiasi cha kuwajengea watu wogam hofu na mashaka katika maisha yao. Kwa bahati mbaya baadhi ya vitendo vya kigaidi vinavyofanywa kutokana na misimamo mikali ya kiimani, vinatekelezwa kwa kulikashfu jina la Mungu ambaye ni chemchemi na kiini cha upendo. Utamaduni wa kifo unaokumbatia sera za utoaji mimba na kifo laini ni mambo yanayosigana na kukinzana na huruma na upendo wa Mungu ambaye kimsingi ni asili ya maisha na wema wote.

Wazee na maskini hawana nafasi tena katika vipaumbele vya jamii; wanathaminiwa wale wenye “vijisenti vyao”, lakini alina yakhe pangu pakavu tia mchuzi wanaishia kulamba vumbi! Mtu anapimwa si kutokana na utu wake kwa vile ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, lakini ni kwa jinsi gani anavyoweza kuzalisha na kuchangia katika mchakato wa kukuza na kustawisha uchumi na huduma. Hata katika maisha ya kawaida wanasema hapendwi mtu isipokuwa pochi! Fedha inaabudiwa kuliko hata utu na heshima ya binadamu! Katika mazingira kama haya, Kanisa linahamasishwa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anapenda kuwahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu, kielelezo cha imani tendaji. Huu ni mwaliko wa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ili nao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu unaibubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Ili kufanikisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuna haja ya kuwa na mbinu mkakati utakaokuwa ni dira na mwongozo wa utekelezaji wa matendo ya huruma: kiroho  na kimwili. Askofu mkuu William Goh Seng Chye katika Waraka wake wa kichungaji anakaza kusema mwaamini wanapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa kutambua udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu, tayari kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu inayotolewa na Mama Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Waamini waoneshe umoja na mshikamano katika: mawazo, maneno na matendo badala ya kujikita katika ubinafsi usiokuwa na mvuto wala mashiko, matokeo yake ni waamini kumezwa na malimwengu na huko ndiko kuliko na patashika nguo kuchanika!Waamini watambue kwamba wanahitaji huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani bado wanaogelea katika dimbwi la dhambi na mauti. Huu ni mwaliko pia kwa waamini kumkimbilia Kristo Yesu kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu; kwa kushiriki kikamilifu maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; kwa kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria sanjari na kusali Rozari takatifu muhtasari wa Injili.

Waamini wanahamasishwa katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuhakikisha kwamba wanaungama mara kwa mara, walau mara moja kila mwezi pale inapowezekana. Washiriki katika matukio mbali mbali ya maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu kwa njia ya hija, Warsha, Makongamano na Semina, lakini zaidi kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili sanjari na ushiriki mkamilifu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu hususan Siku ya Bwana ambayo kimsingi ni siku ya: Mungu, Kristo, Kanisa, Binadanmu na Muda wa kutafakari mambo ya nyakati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.