2016-04-27 07:44:00

Hali ya kisiasa nchini Afrika ya Kusini ni tete sana!


Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linasikitishwa sana na hali tete, kinzani na mipasuko ya kisiasa inayoendelea kushamiri nchini humo kiasi hata cha kutishia umoja, amani, mshikamano na mafungamano ya wananchi wa Afrika ya Kusini katika ujumla wao! Kumekuwepo na mapambano kati ya Jeshi la Polisi na waandamanaji kutoka vyama vya upinzani, hali ambayo inahatarisha amani na utulivu nchini Afrika ya Kusini.

Askofu Abel Gabuza, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini, anasema, wanasiasa wasipobadili mwelekeo na kuanza kujikita katika misingi ya haki, amani, utulivu na maridhiano, kuna hatari kwamba, uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini Afrika ya Kusini hapo tarehe 3 Agosti 2016 utaweza kugubikwa na ghasia pamoja na vurugu, hali ambayo itawakosesha wananchi haki yao ya kikatiba kwa kuwachagua viongozi wanaowataka katika mazingira huru na salama.

Hali kwa sasa ni tete na Afrika ya Kusini inaweza kujikita ikitumbukia tena katika vita ya wenyewe kwa wenyewe! Kiongozi mkuu wa Chama cha Wapigania Uhuru cha Afrika ya Kusini Bwana Julius Malema ametishia kuanza kupambana na Serikali kwa kutumia mtutu wa bunduki, ikiwa kama serikali itaendelea kuvikandamiza na kuvinyanyasa vyama vya upinzani! Hali hii inaweza kuleta maafa makubwa kwa watu na mali zao; pamoja na hasara kubwa katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Huu si mwelekeo sahihi wanasema Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini.

Serikali inapaswa kuangalia hali tete inayopelekea wananchi kuandamana kwa nguvu kiasi hata cha kuhatarisha amani na utulivu! Kwanza kabisa kumekuwepo na pengo kubwa kati ya matajiri na maskini, akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi! Uksoefu wa ajira miongoni mwa vijana ni changamoto pevu kwa Serikali ya Afrika ya Kusini; uchu wa mali na madaraka; kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema; umoja na uzalendo!

Hizi ni changamoto zinazopaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka badala ya vikosi vya ulinzi nau salama kutumia nguvu kupita kiasi. Kimsingi hali ngumu ya uchumi Afrika ya Kusini ni chanzo kikuu cha hali tete inayoendelea kwa sasa nchini humo. Kuna wananchi wanaoendelea kuogelea katika dimbwi na umaskini, magonjwa na umaskini, wakati ambapo kuna kundi la watu wachache wanaotafuna utajiri wa nchi pasi na woga. Wizi wa mali ya umma na ufisadi unaofanywa na vigogo wa serikali ni hali ambayo inatibua nyongo kwa wananchi wengi wa Afrika ya Kusini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.