2016-04-26 09:46:00

Msitoe shavu kwa shetani akazimisha moto wa huruma ya Mungu!


Chama cha Kitume cha Uamsho wa Roho Mtakatifu nchini Italia limehitimisha mkutano wake wa thelathini na tisa ambao ulikuwa unaongozwa na kauli mbiu “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka”. Umekuwa ni muda wa sala, tafakari, ibada na shuhuda za maisha ya Kikristo, kielelezo cha imani tendaji, changamoto ya pekee wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Upatanisho, ushuhuda, huduma makini kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni mambo ambayo yamepewa msukumo wa pekee kwa mwaka huu.

Waamini wanahamasishwa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu na kamwe wasikubali kumpatia “shavu” shetani ili kuzimisha moto wa Roho Mtakatifu katika maisha yao. Hiki ni kipindi cha huruma ya Mungu inayomwezesha binadamu kupata wokovu! Wakati mwingine huruma inaogopesha sana ndiyo maana utakutana na makundi ya watu wanaopambana dhidi ya huruma kama anavyosema Mtakatifu Yohane Paulo II.

Hawa ni watu ambao wanataka kuona Kanisa, uchumi, siasa na haki isiyokuwa na chembe ya huruma hata kidogo na kusahau kwamba, huruma ni jina la Mungu; chembe ya uhai na nguzo thabiti inayowawezesha waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu. Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Bwana Salvatore Martines, Rais wa Chama cha Kitume cha Uamsho wa Roho Mtakatifu nchini Italia wakati wa kufunga mkutano wa thelathini na tisa wa chama hiki uliokuwa unafanyika mjini Rimini, Italia. Sasa wanachama wanatumwa kutoka nje ili kutangaza na kushuhudia nguvu na karama za Roho Mtakatifu katika maisha yao kwa kumwilishwa matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Siku kuu ya Mtakatifu Marko mwinjili, hapo tarehe 25 Aprili 2016, Kardinali Crescenzio Sepe, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Napoli, Italia amewataka wajumbe wa mkutano huu kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu, huku wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Wawe imara katika imani na mashuhuda amini wa huruma ya Mungu kwa watu wasiokuwa na matumaini; watu wanaoteseka kutokana na hali mbali mbali za maisha!

Katika tafakari yake, Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa nyumba ya kipapa, amewataka wanachama zaidi ya elfu kumi na tano waliokuwa wanashiriki mkutano huu kwa ngazi ya kitaifa kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu mintarafu mazingira ya watu wa nyakati hizi, kwa kutambua kwamba, Roho Mtakatifu anaendelea kufanya kazi ndani ya Kanisa.

Waamini wawe ni vyombo vya kubeba chakula na maji ya Roho Mtakatifu ili kuzima njaa na kiu ya wale wanaotafuta kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, changamoto endelevu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Waamini wasali na hatimaye kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao kuhakikisha kwamba, Roho Mtakatifu anaingia na kupenya katika maisha na vipaumbele vya waamini; ili waweze kutumia vyema karama na mapaji yao ili kushuhudia na kumtangaza Kristo kuwa ni Bwana.

Askofu mkuu Matteo Maria Zuppi, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bologna, Italia amesema Mwenyezi Mungu anataka watu wote waokoke pamoja na kupata kujua yale yaliyo kweli kwani Mungu ni mmoja na Kristo Yesu ni mpatanishi kati ya Mungu na binadamu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu! Hii ni changamoto ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini yanayofumbatwa katika huruma ya Mungu, ili kumtambua jirani aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kwa njia hii, waamini wanaweza kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa kuonesha upendo na mshikamano na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kuwalinda wanaotafuta hifadhi ya maisha na kuwaonjesha matumaini wale waliokata tamaa. Hi indio njia muafaka anasema Askofu mkuu Matteo Maria Zuppi ya kumwilisha amri ya upendo kwa Mungu na jirani, watu wanaoonesha Uso wa huruma ya Baba.

Washiriki wa mkutano huu wametafakari kwa kina na mapana umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani, kwa kuondokana na sera za kibaguzi, woga na wasi wasi usiokuwa na mashiko kwa ustawi na maendeleo ya wengi. Upendo kwa jirani pasi na ubaguzi ni chachu ya mabadiliko ya kweli katika maisha ya wengi, mwaliko kwa waamini kumwilisha upendo pale ambapo chuki, hofu na uhasama vinatawala.

Mchakato wa Uinjilishaji mpya unajikita katika ushuhuda makini katika medani mbali mbali za maisha ya watu. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko, Kristo Yesu amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kumrudishia tena hadhi yake kama mtoto mpendwa wa Mungu, mwaliko wa kumwilisha huruma, upendo na wema wa Kristo kwa wahitaji zaidi. Majadiliano ya kidini yajikite katika uhalisia wa maisha, ili kweli huruma na upendo wa Mungu viweze kuwagusa watu wengi zaidi.

Bwana Salvatore Martines, Rais wa Chama cha Kitume cha Uamsho wa Roho Mtakatifu nchini Italia anasema, huruma ni dhana inayofumbatwa katika dini mbali mbali duniani kwani ni sifa na utambulisho wa Mwenyezi Mungu, changamoto na mwaliko wa kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini yanayofumbata matumaini kwa vijana wa kizazi kipya na chachu ya mageuzi yanayopania kwa namna ya pekee kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Amani, upendo, majadiliano na upatanisho yanafumbatwa katika neno moja tu: huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.








All the contents on this site are copyrighted ©.