2016-04-26 15:12:00

Mh. Pd. John Alphonsus Ryan ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Mzuzu, Malawi


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre John Alphonsus Ryan, S.P.S kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mzuzu nchini Malawi. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Ryan ambaye ni Mmissionari wa Shirika la Mtakatifu Patrick, alikuwa ni Jaalim wa Chuo Kikuu cha Mzuzu, nchini Malawi. Askofu mteule Ryan alizaliwa tarehe 27 Februari 1952 Jimbo kuu la Cashel na Emly, nchini Ireland. Kunako mwaka 1971 alijiunga na Shirika la Mtakatifu Patrick na kupewa Daraja Takatifu la Upadre tarehe 18 Juni 1978.

Tangu wakati huo: Kuanzia mwaka 1978 – 2005 metekeleza utume wake katika Parokia mbali mbali nchini Malawi; Mwalimu na mlezi wa Seminari ndogo ya Mtakatifu Patrick huko Rumphi, Jimboni Mzuzu na baadaye akajiendeleza kwa masomo ya juu na kujipatia Shahada ya uzamivu kwenye hisabati huko Ireland.

Kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2011 alikuwa ni Baba wa maisha ya kiroho kwa Watawa wa Rozari takatifu huko Katete. Kuanzia mwaka 2000 amekuwa ni Padre wa maisha ya kiroho na Jaalim wa hisabati, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mzuzu; Paroko msaidizi na mjumbe wa baraza la washauri. Itakumbukwa kwamba Jimbo Katoliki Mzuzu, nchini Malawi liliundwa kunako mwaka 1961 ni sehemu ya Jimbo kuu la Lilongwe. Jimbo hili limekuwa wazi tangu tarehe 5 Januari 2015 kufuatia kifo cha Askofu Joseph Mukasa Zuza kilichotokea kwa ajali ya gari!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

Unaweza kuwasiliana nasi kwa kutumia e mail ifuatayo:

engafrica@vatiradio.va

Au kuandika barua kwa anuani ifuatayo:

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican,

Vatican Radio,

Vatican city, 00120.








All the contents on this site are copyrighted ©.