2016-04-25 11:49:00

Utakatifu wa maisha na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji!


Mtandao wa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Ukanda wa Sahel, Kaskazini mwa Afrika na Ulaya umehitimisha mkutano wao kwa kuunga mkono maamuzi ya mwingiliano wa watu kwenye Jumuiya ya Uchumi Afrika Magharibi, ECOWAS inayounganisha nchi kumi na tano. Padre Alphonce Seck, Katibu mkuu wa Caritas Senegal anasema, mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu “Changamoto ya uhamiaji na haki msingi za binadamu. Dhamana ya Caritas Sahel, Kaskazini mwa Afrika na Barani Ulaya?”

Ili kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambao wamehifadhiwa kwenye kambi za utambulisho kuna haja kwa Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki kushirikiana na kushikamana kwa kukazia kwa namna ya pekee: utakatifu wa maisha ya binadamu, mshikamano na matumizi ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Caritas Senegal ndiyo ambayo imepewa dhamana ya kuratibu huduma inayotolewa na Caritas Ukanda wa Sahel.

Lengo ni kusaidia pia kutoa huduma ya ulinzi na usalama katika maeneo ambayo yana vita na kinzani za kijamii, ili kujenga na kuimarisha mchakato wa haki, amani, upatanisho na umoja wa kitaifa, Caritas Afrika inapaswa kuibua sera na mbinu mkakati wa kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika. Mashirika haya yameamua kushirikiana kwa karibu zaidi katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Benjamin Ndiaye wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal, ameyataka Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Ukanda wa Sahel kuwajibika zaidi katika kuwahudumia na kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika. Familia ya Mungu Barani Afrika inampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuamuia kuonesha mshikamano wa huruma na upendo kwa wakimbizi kumi na wa wawili kutoka Syria ambao waliambata naye kutoka Lesvos, Ugiriki.

Kwa sasa wanahudumiwa na Vatican, kielelezo cha umwilishaji wa matendo ya huruma katika uhalisia wa maisha, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii ni changamoto makini kwa familia ya Mungu Barani Ulaya kuona na kuiga mfano wa Baba Mtakatifu Francisko katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.