2016-04-25 10:28:00

Kumbu kumbu ya miaka 101 ya mauaji ya kimbari Armenia!


Familia ya Mungu nchini Armenia tarehe 24 Aprili 2016 imeadhimisha kumbu kumbu ya miaka 101 tangu yalipotokea mauaji ya kimbari “Metz Yegern” yaliyosababisha watu zaidi ya millioni 1. 5 kupoteza maisha kutokana na chuki za kidini. Tukio hili limekumbukwa kwa ibada na makesha katika Makanisa mbali mbali nchini Armenia. Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki ameshiriki Ibada ya mkesha wa tukio hili kwenye  Chuo kikuu cha Kipapa cha Waarmenia mjini, Roma. Maadhimisho ya Mwaka huu yanakwenda sanjari na Maadhimisho ya Pasaka ya Wayahudi, wanapokumbuka matendo makuu ya Mungu aliyewaokoa Waisraeli kutoka utumwani Misri kwa nguvu na uweza mkuu.

Waisraeli wanakumbuka kipindi cha giza na utupu katika historia ya maisha yao na kwamba, wanaweza kuwa huru zaidi kuonesha uaminifu wao kwa Mungu. Daima Waisraeli wamekumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu ameendelea kuwa mwaminifu kwa sababu hii ni asili yake! Mwaka huu, familia ya Mungu nchini Armenia inafanya kumbu kumbu ya miaka 101 tangu mauaji ya kimbari yalipotokea, mwaliko wa kutafakari mateso na mahangaiko ya waamini yaliowawezesha kuwa kweli ni mashuhuda wa imani.

Hawa ni watu waliovumilia: mateso, nyanyaso na dhuluma na hatimaye, wakaonesha uaminifu wao kwa Mungu na sasa wanafurahia maisha ya uzima wa milele mbinguni kama alivyowahi kusema Mtakatifu Gregori wa Narek. Kardinali Sandri anasema, hii ni fursa pia ya kumsindikiza Baba Mtakatifu Francisko wakati huu anapojiandaa kufanya hija yake ya kitume nchini Armenia, ili aweze kuwasha moto wa huruma na haki katika akili na nyoyo za watu. Mwanga angavu kutoka mbinguni ufukuzie mbali giza la kifo ili nguvu ya Mungu iweze kung’ara zaidi.

Wameombea: imani, matumaini na faraja kutoka kwa Yesu, ili kweli mwanga wake angavu wa ukombozi uweze kuleta faraja kwa wote! Jumapili tarehe 24 Aprili 2016, Monsinyo Nareg Naamoian, Gombera wa Chuo kikuu cha Kipapa cha Waarmeni ameongoza Ibada Takatifu na baadaye, kuweka shada la maua kwenye “Khatchar” iliyoko kwenye mlango wa kuingilia Kanisani hapo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.