2016-04-24 07:57:00

Maisha bila Yesu ni sawa na simu ya mkononi isiyokuwa na betri!


Watoto zaidi ya 70, 000 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kuupamba mji wa Roma kwa sala, tafakari, hija, nyimbo, michezo na nyuso za furaha, wakati huu wanapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa watoto. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu George, Shahidi sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yanaongozwa na  kauli mbiu “Kukua katika huruma kama Baba wa mbinguni”, Jumamosi, tarehe 23 Aprili 2016, amejiunga na Mapadre wengine 150 ili kutoa Sakramenti ya Upatanisho kwa watoto wenye umri kati ya miaka 13- 16 wanaoshiriki maadhimisho ya Jubilei ya watoto hapa mjini Vatican.

Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amewaungamisha watoto kumi na sita kuanzia saa 5: 30 hadi saa 6: 45 majira ya mchana kwa saa za Ulaya. Baba Mtakatifu kama mapadre wengine walitawanyika kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ili kutoa Sakramenti ya Upatanisho kwa watoto ambao walikuwa wanakimbilia huruma ya Mungu kama sehemu ya masharti pia ya kupata rehema kamili wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Ni uhakika anasema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume Uso wa huruma kwamba, Sakramenti ya Upatanisho ni kiini cha uhakika wa huruma ya Mungu kwa sababu inamfanya mwamini aguse kwa mkono wake ukuu wa huruma ya Mungu katika maisha yake na kwamba, toba ya kweli ni chimbuko la amani ya ndani!

Jumamosi usiku, watoto hawa wamefanya mkesha kwenye Uwanja wa michezo wa Olimpic ulioko mjini Roma. Hiki kimekuwa ni kipindi cha sherehe kubwa miongoni mwa watoto waliobahatika kusikiliza shuhuda  na muziki na hatimaye kusikia ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko uliotumwa kwao kwa njia ya video. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, ameshindwa kujiunga nao kwenye tamasha hili la muziki.

Anawashukuru na kuwapongeza kwa kukubali na kuitikia mwaliko wake na hatimaye, kuja kujiunga naye kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu mjini Roma, kwa kuungama dhambi zao na hatimaye kuvuka Lango la huruma ya Mungu, kielelezo cha kukutana na Kristo Yesu anayewaonjesha upendo wa Baba yake wa mbinguni na kuwataka kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni! Huu umekuwa ni muda muafaka kwa watoto hawa kukaa pamoja ili kusikiliza shuhuda mbali mbali zinazoweza kuwasaidia kukua na kukomaa katika imani na maisha.

Baba Mtakatifu anawaalika watoto hawa kumwilisha katika maisha yao matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwani huu ndio mtindo wa maisha ya Kikristo unaopaswa kushuhudiwa kila siku ya maisha, ili kugundua Uso wa Yesu unaojionesha kati ya watu mbali mbali wanaokutana nao. Kuna watoto kama wao ambao wana njaa, kiu; ni wakimbizi na wahamiaji; au ni wagonjwa, wote hawa wanahitaji kupewa msaada na kuonjeshwa urafiki. Kuwa na huruma maana yake ni kuwa na uwezo pia wa kusamehe; kwani msamaha unaweza kuhitajika sehemu mbali mbali za maisha yao! Wakati mwingine, wao wenyewe wanaweza kuwa ni chanzo cha vurugu na matokeo yake ni kutaka kulipiza kisasi!

Hali hii anasema Baba Mtakatifu haiwasaidii hata kidogo, inawatendea na kuwakosesha furaha ya ndani, changamoto ni kusamehe na kusahau, kama sehemu ya utekelezaji wa mafundisho ya Yesu, kwa kuwa ni wafuasi wake na mashuhuda wa huruma. Maisha bila Yesu ni sawa sawa na simu ya mkononi isiyokuwa na betri, matokeo yake ni mtu kujifungia katika ubinafsi wake. Baba Mtakatifu anawaalika watoto kujenga mshikamano wa upendo katika familia, parokia na shule na kwa njia hii, daima watakuwa na uwezo wa kusema lililojema na la kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.