2016-04-22 08:59:00

Jubilei ya huruma ya Mungu kwa watoto wadogo!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi muafaka cha neema, amani, toba, wongofu wa ndani na furaha inayowaambata wote: wakubwa kwa wadogo; walioko karibu na wale walioko mbali na kwamba, hakuna kizuizi chochote kinachoweza kujikitokeza ili kukwamisha huruma ya Mungu isiwafikie na kujidhihirisha kati ya watu wake. Lango la Huruma ya Mungu limefunguliwa Roma na sehemu mbali mbali za dunia, changamoto kwa waamini kukimbilia na kupitia kwenye Lango hili!

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa watoto wadogo, yatakayo fikia kilele chake hapo tarehe 24 Aprili 2016, Kanisa linapoadhimisha Jumapili ya tano ya Kipindi cha Pasaka. Watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia watamzunguka Baba Mtakatifu Francisko ambaye Jumamosi tarehe 23 Aprili 2016 anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu George, Shahidi.

Baba Mtakatifu anawahamasisha watoto kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya kwa kutambua kwamba, wao ni watoto wapendwa na wateule wa Mungu! Anapenda kumwita kila mmoja wao kwa jina kama alivyokuwa anafanya Yesu Kristo kwa kutambua kwamba, majina yao yameandikwa mbinguni na kuchongwa katika  Moyo Mtakatifu wa Baba mwenye huruma, chemchemi ya upatanisho na unyenyekevu wa moyo!

Baba Mtakatifu anawambia watoto kwamba, Mwaka Mtakatifu ni kipindi maalum kinacho wahamasisha waamini kuchuchumilia utakatifu, safari inayopaswa kufanywa kila siku ya maisha, kwa kutambua kuwa, wao ni ndugu, wanaotamani kuadhimisha sherehe kubwa ya imani isiyomtenga wala kumbagua mtu awaye yote. Hapa, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watoto kutenga siku maalum kwa ajili ya sala na kufurahia maisha na kwamba, anatarajia kukutana nao kwa wingi wakati wa Jubilei yao hapa mjini Roma.

Maadhimisho ya Jubilei ya watoto yanaongozwa na kauli mbiu “Kukua katika huruma kama Baba wa mbinguni”. Hii ndiyo sala ambayo Mama Kanisa anapenda kuitolea kwa ajili ya watoto; ili watoto hawa waweze kuwa ujasiri unaojikita katika upendo usiotafuta faida binafsi; kuna maanisha kukua na kukomaa kiroho na kimwili; kuwa Wakristo wenye ujasiri ili kujenga kila siku ulimwengu unaojikita katika amani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema katika umri wao, inaonekana kana kwamba, kila kitu kinawezekana na wakati huo huo, si kila kitu kinawezekana! Hapa watoto wanapaswa kujikita katika imani na matumaini kwa Kristo Yesu, siri ya safari yao ya maisha hapa duniani kwa kumtegemea Kristo anayewapatia ujasiri na nguvu ya kusonga mbele kiasi hata cha kufanya mambo makubwa; kwa kuwaonjesha furaha ya kuwa ni wafuasi na mashuhuda wake. Watoto wawe na ndoto ya kutenda makubwa. Baba Mtakatifu anawakumbuka na kuwaombea watoto wanaoishi katika maeneo yenye vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; watoto wanaoelemewa na umaskini, magonjwa na hali ya kutelekezwa!

Katika mazingira yote haya, watoto hawana sababu ya kukata tamaa kwani Mwenyezi Mungu ana mpango mahususi kwa ajili ya maisha yao. Kuna watoto wenzao wanaowakumbuka na kuwaombea, ili haki na amani viweze kutawala. Wasikubali kumezwa na maneno ya chuki na uhasama, bali wajitahidi kuwa ni marafiki wapendwa wa Yesu, Mfalme wa amani na maisha yote ya Yesu ni chemchemi ya huruma.

Baba Mtakatifu anatambua kwamba, si watoto wote wataweza kufika Roma ili kuadhimisha Jubilei ya watoto, lakini pia wanaweza kuadhimisha tukio hili la imani katika Majimbo na Parokia zao. Hiki kiwe ni kipindi cha kuandaa mioyo na akili zao. Watoto wafanye tafakari ya kina ili waweze kuwasilisha maombi yao kwa Yesu; waendelee kurutibisha maisha yao kwa Neno na Ekaristi Takatifu, ili kujenga ulimwengu unaosimikwa katika haki na udugu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaombea baraka tele katika kila hatua watakayoifanya ili kupitia Lango la Huruma ya Mungu. Roho Mtakatifu awaongoze na kuwaangazia; Bikira Maria awaombee ili waweze kukua katika wema na neema, ili kweli waweze kuwa ni Lango la Huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.