2016-04-22 09:54:00

Jibuni changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi kwa ujasiri na uadilifu


Viongozi 270 wa kidini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanawaalika viongozi wa Serikali na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake kuweka sahihi itifaki ya makubaliano ya mkutano kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi yaliyofikiwa mjini Paris, Ufaransa, Desemba 2015. Changamoto za athari za mabadiliko ya tabianchi zinahitaji kujibiwa kwa ujasiri na uadilifu, ili kupunguza hewa ya ukaa inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, Ijumaa tarehe 22 Aprili 2016 wanatarajiwa kutia sahihi kwenye Itifaki ya makubaliano ya udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi yaliyofikiwa mjini Paris, Ufaransa.

Itakumbukwa kwamba, itifaki hii itaweza kuanza kutekelezwa ikiwa kama nchi wanachama 55 wa Umoja wa Mataifa watatia sahihi kwenye mkataba huo ambao ni muhimu sana kwa mustakabali na maendeleo ya wengi. Tamko la viongozi hawa wa kidini limewasilishwa hivi karibuni mjini New York kwa Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa Bwana Mogens Lykketoft, kutoka Denmark. Tamko hili lina sahihi za viongozi mashuhuri wa dini mbali mbali kama vile: Askofu Marcelo Sànchez Sorondo, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Elimu na Sayansi Jamii, Askofu mkuu mstaafu Desmond Tutu wa Kanisa Anglikan, Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Imam mkuu Maulana Syed Muhammad Abdul Kharib Azad, Mkuu wa Marabi wa Kiyahudi Sheah Yashuv Cohen na wengine wengi!

Viongozi wa kidini wanakaza kusema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni wajibu fungamanishi unaojikita katika kanuni maadili kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote sanjari na matamko mbali mbali yaliyokwisha tolewa na viongozi wakuu wa kidini duniani. Viongozi hawa wanaikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kwamba, hewa ya ukaa imekwishapita kiwango cha usalama na ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitachukua hatua za dharura, madhara yake ni makubwa kwa familia ya binadamu.

Viongozi wa kidini wanawataka viongozi wakuu wa Serikali kutenda kwa ujasiri na uadilifu kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Itifaki hii iwe ni mwanzo wa mchakato wa mageuzi ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kujikita katika teknolojia rafiki kwa mazingira sanjari na mabadiliko makubwa ya mtindo wa maisha! Changamoto kubwa ni kuwa na mageuzi makubwa mintarafu utamaduni wa ulaji unaopelekea katika uharibifu mkubwa wa mazingira. Lengo ni kuwa na matumaini kwa mazingira bora zaidi kwa siku za usoni. Hapa Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushirikiana kwa dhati kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiutu na kibinadamu kwa kuweka kando mambo yote yanayowagawa na kuwasambaratisha wanadamu katika ulimwengu mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.