2016-04-22 15:33:00

Iweni imara katika imani!


Mpendwa msikilizaji, karibu sana katika kipindi cha Tafakari ya Neno la Mungu. Tunaadhimisha Jumapili ya tano ya Pasaka, mwaka CHE wa Kanisa. Neno la Mungu katika domenika hii limejikita katika kuimarisha roho za wafuasi wa Kristo ili kwa wakati muafaka wapate kuishi katika Mji wa milele, Yerusalemu mpya. Tunasikia kutoka katika simulizi za Matendo ya mitume, namna Paulo na Barnaba walivyona umuhimu wa kuimarisha jumuiya za kikristo na hivyo kuzungukia Makanisa kadha wa kadha wakifanya hivyo. Injili inakualika kuishi kwa upendo na kila mtu ili uweze kuishi milele mbinguni, katika mji wenye  furaha ya pekee pamoja na Mungu, kama inavyosimuliwa katika kitabu cha Ufunuo.

Tafakari.

Mpenzi msikilizaji, baada ya kuipokea Imani kwa Sakramenti ya ubatizo, uliimarishwa kwa mhuli na mapaji ya Roho Mtakatifu kwa Sakramenti ya Kipaimara. Uimara huo ni wa muhimu sababu adui yetu Ibilisi na wafuasi wake, hawalali, wanatafuta kila mbinu kila siku ili kukuangusha. Ibilisi anatumia vivutio vingi sana vyenye kuleta furaha ya muda, mfano mali za mazingira, dhuruma na wizi, ulevi, mapenzi holela na kadhalika, lakini havidumu na mwisho wa yote hukuumiza wewe mhusika na wapendwa wako. Zaidi ya hapo, vinakukosesha mbingu. Vivutio hivyo ni vya kimwili zaidi, lakini unaweza kuvishinda vishawishi hivyo iwapo upo imara rohoni kiimani.

Roho yako inapaswa kuwa imara kwa mapaji ambayo Roho wa Bwana amekutunuku tayari, ikiwa ni pamoja na paji la Imani yenyewe. Katika usemaji na utendaji wako, muda wote tumia hekima na utimamu wa akili katika kuchanganua, uwe na roho ya kushauri wengine, uwe na ujasiri katika kutenda mema, uwe na nguvu ya kiroho kupambana na Ibilisi katika majaribu, usiteteleke wala kukata tamaa na kukubali kushindwa, kujiachia katika dhambi.

Ongeza juhudi ya kufahamu mambo yote, na ufahamu vizuri kile ambacho Mama Kanisa anafundisha juu ya hayo ili uyafuate vema. Uwe mtu wa ibada, zingatia kushiriki kikamilifu katika Misa Takatifu, kuabudu Yesu wa Ekaristi Takatifu, Sala mbali mbali kama vile Rozari, maombi, kusoma na kutafakari Neno la Mungu na kadhalika. Uwe mcha Mungu, yaani uwe na hofu ya kutenda uovu, na uwe mtu wa shukrani kwa Mungu kwa kila jambo maishani, usiwe mlalamishi, au mtu wa kukufuru. Haya yatakufanya uwe imara katika Imani, lakini unapaswa sasa kudumu katika uimara huo.

Viongozi wetu wa kiroho hutukumbusha mambo haya yote kwa msisitizo hasa katika mahubiri, tafakari mbali mbali na ushauri wa kiroho. Mbali na viongozi wa dini, kuna viongozi wa Halmashauri walei, katika ngazi mbali mbali. Kila ambaye amepewa dhamana ya uongozi katika Kanisa, analo jukumu hilo pia la kuendelea kuwakumbusha wengine mafundisho sahihi ya Imani ili wasikengeuke wala kuteteleka. Dhamana hiyo ni ya muhimu sana, na ndio sababu huombewa na viongozi wa dini ili waitekeleze huduma hiyo vyema. Huu ni utamaduni tangu awali kama tunavyosoma katika masimulizi tuliyosikia walivyofanya Paulo na Barnaba “Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila Kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini”.

Kiongozi yeyote, unapotimiza majukumu yako vizuri, wengine huona, watu wema watakuombea Neema kwa Mungu kwa kazi njema ulizozitimiza, na kama anavyofundisha mtume Yakobo “sala ya mtu mwema ina nguvu ya kutenda kazi, ya kutenda miujiza” [Rej., Yakobo 5, 16].

Unapodumu katika uimara rohoni na kuombeana neema, unajipalilia njia ya kuingia na kuishi katika mji ule wa milele, Yerusalemu mpya. Katika mji huo utaishi na Mungu milele sababu ni hamu ya Mungu siku zote aishi pamoja na wanadamu kwa upendo, furaha na Amani. Yohane analiona hilo katika ukamilifu wake mwisho wa nyakati “Tazama maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake”

Ndugu msikilizaji, hata sasa Mungu yupo pamoja nawe kwa kukuminia Roho wake ndani yako, na Roho huyo anakumiminia upendo wa kimungu, anashuhudia Paulo Mtume “Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu, na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” [Rej., Warumi 5, 5]. Zaidi Kristo, nafsi ya pili ya Mungu, amebaki nawe katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Uwepo wa Mungu maishani mwako, rohoni mwako, ni maandalizi ya kuishi nawe milele baadaye. Mungu anakualika ushirikiane naye katika mpango mzima wa kuubadili ulimwengu taratibu tangu sasa sababu katika ulimwengu ujao, Yerusalemu mpya, watu na vitu vitageuzwa ili viwe katika ubora wake “Tazama nafanya yote kuwa mapya”.

Katika kudumu imara kiimani kuna changamoto nyingi, magumu mengi, hata usaliti wa watu wako wa karibu, kama alivyofanya Yuda Iskarioti. Lakini tambua mpendwa msikilizaji ya kwamba, katika changamoto, magumu na usaliti wowote, Bwana atakutukuza, kama alivyomtukuza Kristu. Unapaswa udumu imara rohoni, na uwapende wote hata wanaokusababishia mateso. Ukifanya hivyo, Mungu atatukuzwa ndani yako, maana watu wote watashuhudia ya kuwa kweli wewe umekuwa mwanafunzi wa Kristu. Huu ni ushindi mkubwa wa ufufuko wa roho.

Tambua ya kuwa adha na dhiki ni sehemu ya kuthibitisha, kuimarisha Imani yako, ndio sababu hata Paulo na Barnaba wanawaimarisha wanafunzi kwa kuwahimiza kuwa “imetupasa kuingia katika Ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi”. Hivyo dumu imara, shirikiana na Mungu na sema pamoja naye leo “Tazama nayafanya yote kuwa mapya”, ukiwa na Imani thabiti kuwa baada ya hayo yote, Mungu atafuta kila chozi katika macho yako.

Hitimisho

Mpenzi msikilizaji, kwa niaba ya watangazaji wa Radio Vatican, napenda kukushukuru sana kwa kuwa pamoja name katika kipindi hichi cha Tafakari ya Neno la Mungu. Karibu tena juma lijalo katika kipindi hiki, kwa muda na wakati kama huu. Mi nimenuia ushirikiana na Muumba kwa nafasi yangu na nasema pamoja naye “Tazama nayafanya yote kuwa mapya”, kazi kwako. Kutoka viunga vya Radio Vatican, ni sauti ya kinabii, Padre Celestine Nyanda.








All the contents on this site are copyrighted ©.