2016-04-21 06:53:00

Wana michezo ni wajumbe wa nguvu ya umoja na kioo cha jamii!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 20 Aprili 2016 amekutana na kuzungumza na Shirikisho la wanamichezo wa kuteleza kwenye barafu kutoka Austria. Amewapongeza na kuwakumbusha kwamba, michezo ya kuteleza kwenye barafu ni maarufu sana nchini mwao na kwamba, wananchi wanawaonea fahari pale wanaposhinda kwenye michezo. Wanamichezo, kimsingi ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa kwa vijana wengi wa kizazi kipya. Wao ni mfano wa ushirikishwaji si tu katika masuala ya michezo, lakini zaidi kutokana na karama na tunu msingi zinazofumbatwa katika michezo.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, wanamichezo wanatambua kwamba, michezo ni: dhamana inayohitaji udumifu; nia thabiti, uhakika, mshikamano na moyo wa timu. Kwa mifano ya maisha yao bora, wanamichezo wanachangia katika mchakato wa majiundo ndani ya jamii. Wanamichezo wanahimizwa kuwa wajumbe wa nguvu inayowaunganisha watu katika michezo pamoja na ukarimu. Wanamichezo wanapaswa kuwa ni watunzaji bora wa mazingira na kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu. Baba Mtakatifu amewashukuru wote kwa moyo wao wa ukarimu na hasa zaidi kwa kuamua kumtembelea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.