2016-04-21 14:35:00

Vijana na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!


Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe vijana kutoka Argentina wanaotembelea Ncha ya Kaskazini, huku wakiwa wametwaa Waraka wa Kitume, “Sifa kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” Laudato si! Pamoja na jani la mti wa Mzeituni alama ya amani. Hii ni safari ya kwanza kabisa kuwahi kutekelezwa na watu kutoka Argentina na Amerika ya Kusini mintarafu athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kusaidia zaidi mchakato wa uragibishaji juu ya utunzaji wa mazingira, nyumba ya wote.

Safari hii inagharimiwa na Mfuko wa “Criteria” unaojipambanua kwa kujikita katika usalama wa binadamu pamoja na mtandao wa kimataifa wa shule “Scholas Occurentes”  ulioanzishwa nchini Argentina, kwa utashi wa Baba Mtakatifu Francisko wakati huo akiwa kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires. Vijana hawa wanasindikizwa na bendera ya “Scholas Occurrentes”. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anakazia umuhimu wa kutambua madhara makubwa yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; uchimbaji haramu wa rasilimali ya dunia pamoja na uchafuzi wa mazingira sanjari na ugawaji tenge wa rasilimali ya dunia.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana hawa kwamba, safari wanayoitekeleza kwa wakati huu ni ushuhuda wau pendo, nguvu na kazi ya pamoja kama timu, jambo ambalo linaweza kusaidia ujenzi wa madaraja ya watu kukutana badala ya kuta za utengano. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kuwatia moyo kwa ujasiri wanaoonesha na kwamba, kila jambo linawezekana. Anazishukuru pia familia zao zinazoendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.