2016-04-21 11:50:00

Itifaki ya Makubaliano ya Paris, COP21 kutiwa sahihi, Umoja wa Mataifa!


Jumuiya ya Kimataifa Ijumaa, tarehe 22 Aprili 2016 kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani inaweka sahihi kwenye makubaliano ya itifaki ya kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, matokeo ya mkutano kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi uliofanyika Jijini Paris, Ufaransa, Desemba 2015. Tukio hili litaongozwa na Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa. Lengo ni kupunguza kiwango cha nyuzi joto 2°C. Itifaki hii itakuwa wazi kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa hadi kufikia mwaka 2020 na utaanza kutekelezwa siku 30 baada ya asilimia 55 ya Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutia sahihi itifaki hii inayopania pamoja na mambo mengine kupunguza hewa ya ukaa!

Makubaliano haya yanahitaji mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa ili kufanikisha utekelezaji wake, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi hazichagui wala kubagua nchi maskini wala tajiri, wote wanaathirika ingawa kwa viwango tofauti. Hii ni changamoto ya kuwekeza katika teknolojia rafiki na mazingira. Utekelezaji huu ni hatua kubwa katika mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuwatumbukiza mamilioni ya watu katika umaskini wa hali na kipato.

Wanasayansi na watetezi wa mazingira wanasema, utekelezaji wa itifaki hii unaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, tayari kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu. Jambo la msingi ni kupunguza hewa ya ukaa sanjari na kudhibiti uchafuzi wa mazingira. Kila nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa anapaswa kuhakikisha kwamba anachangia kwa hali na mali katika mchakato huu katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa, bila kusita na kutumbukia tena kwenye uchafuzi wa mazingira. Hii ni changamoto kwa Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba wanatekeleza kwa dhati Ajenda ya Maendeleo Endelevu Ifikapo mwaka 2030.

Utekelezaji wa Itifaki hii unajikita kwa namna ya pekee katika utashi wa kisiasa unaopania kukuza na kudumisha mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Kushindwa kutekeleza itifaki hii athari zake zitaendelea kujionesha katika chumi na maendeleo ya watu duniani na ikumbukwe kwamba, waathirika wakuu ni wananchi wanaotoka katika nchi maskini zaidi duniani! Itifaki hii inajikita katika utekelezaji wa sheria na maamuzi yaliyofikiwa. Lakini wachunguzi wa mambo wanasema, sehemu kubwa ya itifaki hii haizifungi nchi wanachama, jambo ambalo ni udhaifu mkubwa wa itifaki hii. Kwa mfano mchango unaopaswa kutolewa katika ngazi ya kitaifa.

Nchi zinazoendelea duniani zinaendelea kuhamasisha Mataifa tajiri zaidi kutekeleza itifaki hii kwa kuzingatia usawa na haki; kwa kuzingatia uwezo na mazingira ya kila taifa. Hadi sasa nchi 186 wanachama wa Umoja wa Mataifa wamekwisha wasilisha mchango wao kadiri ya kiwango cha kitaifa. Mkataba wa Paris ni chachu ya uwajibikaji katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kupunguza kiwango cha joto duniani pamoja na hewa ya ukaa. Makubaliano ya Paris ni hatua kubwa katika ushuhuda na mshikamano wa kimataifa. Wachunguzi wa mambo wanakaza kusema, kuna uhusiano mkubwa kati ya athari za mabadiliko ya tabianchi na mchakato wa maendeleo endelevu. Lengo ni kutokomeza umaskini wa hali na kipato; kuendeleza mchakato wa maboresho ya uchumi; kudumisha ulinzi na usalama.

Hadi sasa kuna jitihada za makusudi zinazofanywa na Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa pamoja na sekta binafsi katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu! Utekelezaji wa Itifaki ya Paris ni muhimu sana kwa wakati huu kwani katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Jumuiya ya Kimataifa imeshuhudia athari kubwa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, kiasi cha kuwagusa na kuwatikisa wananchi wengi, matajiri na maskini! Kuchelewesha utekelezaji wake, kuna maanisha kukwamisha ukuaji wa uchumi; mapambano dhidi ya umaskini; uboreshaji wa huduma za afya, ustawi na maendeleo ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa imejipanga vyema kuangalia mchango wa nchi wanachama na zile ambazo zimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na Itifaki ya Paris.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.