2016-04-20 07:19:00

Vita na athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto za kitaalimungu!


Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Cantebury, Uingereza ambaye pia ni mkuu wa Kanisa Anglikani akichangia mada kwenye mkutano wa Baraza la Ushauri la Kanisa Anglikani uliofunguliwa hapo tarehe 8 Aprili na kuhitimishwa, tarehe 19 Aprili 2016 huko, Lusaka Zambia anasema uhalifu na vita ni changamoto kubwa katika tafakari za kitaalimungu zinazofanywa na Wakristo kwa wakati huu.

Kumekuwepo na mashambulizi ya kigaidi ambayo yanagubikwa na chuki za kidini, uchu wa mali na madaeaka. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya changamoto ambazo zinamwandama mwanadamu katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Changamoto hizi zinapaswa kupembuliwa kwa kina na mapana ili hatimaye, kupata ufumbuzi wake kabla ya mambo hayajaharibika zaidi.

Matukio ya mashambulizi ya kigaidi kutoka sehemu mbali mbali za dunia yanaonesha kwamba, walimwengu wanaishi katika kipindi cha vita, vurugu na chuki ambazo hazina mvuto wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya watu. Takwimu zinazonesha kwamba, waathirika wakubwa wa vita na mashambulizi ya kigaidi ni Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia, hususan, huko Mashariki ya Kati, Asia na Afrika na Ulaya.

Askofu mkuu Welby anakaza kusema, athari za mabadiliko ya tabianchi ni changamoto nyingine kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kwani inagusa na kutikisa uchumi na maisha ya watu wengi. Matokeo yake ni mipasuko na kinzani za kijamii; ukosefu wa haki na usawa wa kijamii pamoja na ongezeko kubwa la umaskini wa hali na kipato. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni matokeo ya maafa asilia.

Changamoto hizi zinaweza kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kitaalimungu na sera makini zitakazosaidia kufutilia mbali ubinafsi na utaifa usiokuwa na mashiko. Wakristo wanapaswa kuchota katika utajiri wa hazina na amana yao ya kitaalimungu ili kusaidia walimwengu kuweza kukabiliana na changamoto hizi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mwenyezi Mungu, binadamu, ustawi na mafao ya wengi. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinawagusa wengi, hata kama si moja kwa moja, changamoto ya kukabiliana na athari hizi, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi hata kwa kizazi kijacho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.