Mkristo asiyevutwa na upendo wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo, ni Mkristo anayeishi katika hali ya upweke wa yatima asiyekuwa na Baba . Ni mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko , wakati wa Ibada ya Misa, mapema Jumanne, katika kanisa dogo la Mtakatifu Marta . Papa ameuzungumzia moyo mgumu usiotaka kuelewa ujumbe wa Mungu, akitaja kwamba huko ni kukosa imani.Moyo wenye kusikiliza sauti ya Mungu, ni moyo wenye kujifunua wazi kwa Mungu, na huisikia habari njema inayoletwa na Roho Mtakatifu.
Papa alieleza akilenga katika jinsi binadamu anavyokuwa na moyo mgumu katika kusadiki, moyo wenye kudai kwanza ishara na miujiza na bado huendelea kuhoji iwapo ni kweli ni Kristo anayetenda miujiza. Alilenga katika somo la Injili ambamo Mafarisayo na Waandishi wanamwuliza Yesu swali, hadi lini ataendelea kuwaweka katika hali ya kusubiri , walitaka kufahamu mara moja kama kweli ndiye Kristo, wanayemsubiri. Hawakusadiki miujiza na ishara nyingi zilifofanywa na Yesu, bado walitaka awaambie waziwazi kama ndiye Masiya. Papa ameeleza swali hili la Waandishi na Mafarisayo la mara kwa mara, kimsingi linatokana na upofu wa moyo. Upofu wa imani. Yesu aliwaambia waliokuwa wakimhoji kwamba hawawezi kuelewa kwa sababu hawakuamini. Na bila imani wanakuwa si sehemu ya wanakondoo wake, si sehemu ya Kundi la Mungu maana kuwa mmoja wa Kundi la Mungu inahitaji kuwa moyo ulio wazi , moyo wenye kusikia sauti ya Mungu na kuitikia wito.
Na kwamba Kondoo wake huisikia sauti yake, naye anawajua na humfuata. Na yeye huwapatia uzima wa milele; nao hawatapotea milele, na hakuna mtu awezaye kuwapokonya kutoka mkono wake. Kondoo hao wamejifunza kumfuata Yesu na wanaamini. Na ni Baba yake aliye mkuu ndiye aliyempa , na ni yeye Baba anayewapa moyo unaowavutia kwa Yesu.
Papa alieleza na kuitaja mioyo migumu ya waandishi na Mafarisayo, ambao waliona Yesu akitenda lakini hawakuamini kama yeye ndiye Masiha , waliona kama vile Yesu anafanya mchezo wa kuigiza hadi kumpeleka katika njia ya Kalvario. Papa alieleza na kusema hata baada ya ufufuko waliendelea kutosadiki, wakisema maaskari walinda kaburi walilala usinginzi na kisha wanafunzi wake wakauiba mwili wa Kristo. Walikataa kusadiki ushuhuda wa kusisimua uliotolewa juu ya Yesu Kufufuka . Walibaki katika maisha yao ya giza kama yatima wapweke, wakikataa kusadiki neno la Baba.
Licha ya kuwa walimu wa sheria mioyo yao ilibaki imefungwa katika mambo yao ya kale, kwa kweli, walikuwa yatima, kwa sababu hawakuwa na uhusiano na Baba. Walizungumzia, ndiyo, wahenga wao , Abraham, Isaka na wengine lakini mioyo yao ikiwa mbali na ukweli unaoelezwa na Kristo kuwa ndiye Masiya waliyekuwa wakimsubiri. Mioyoni mwao waliendelea kuishi katika hali ya yatima.
Papa alikamisha homilía yake kwa kutoa mwaliko kwamba kuwa mfuasi wa Yesu, ni lazima sisi wenyewe tuvutiwe na Upendo wa Baba katika kumwelekea Yesu. Ameitaja sala ya unyenyekevu wa mwana, tunayotakiwa sisi kuitoa , kumwomba Baba atupeleke kwa mwana, kwa kumtuma Roho Mtakatifu mwenye uwezo wa kufungua mioyo na kutuongoza kwa Yesu . Mkristo asiyevutwa na upendo wa Baba, huyo huishi maisha ya kiyatima. Ambapo Wakristo wa kweli si yatima maana wanaye Baba.
All the contents on this site are copyrighted ©. |