2016-04-19 10:22:00

Marehemu Askofu Isuja, alikuwa maskini jeuri!


Mhashamu Askofu Mathias Isuja Joseph ni mtoto wa mzee Joseph Chundu na Mama Odilia Mbula. Alizaliwa tarehe 14/08/1929 katika Kijiji cha Haubi Wilayani Kondoa. Alisoma shule ya Msingi Kondoa na Bihawana kuanzia mwaka 1942-1948. Mnamo mwaka 1949-1953 alichaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari katika Seminari ya Bihawana. Mwaka 1953-1955 alijiunga na Seminari ya Tosamaganga, Jimbo Katoliki Iringa kwa elimu ya Faslsafa. Mwaka 1956-1960 alijiunga na Seminari kuu ya Kibosho kwa elimu ya Taalimungu. Alitunukiwa daraja ya upadre mwaka 1960, Decemba 24 katika Parokia ya Kondoa.

Mara baada ya kupewa Daraja Takatifu la Upadre, Padre Mathiasi Isuja alitumwa Parokia ya Kibakwe kuwa Paroko 1961-1963 Septemba. Mwaka 1963-1969 aliteuliwa kuwa katibu wa Elimu Jimbo. Mwaka 1966-1971 aliteuliwa kuwa Makamu wa Askofu (Vicar General) huku akiendelea na nafasi yake ya katibu wa elimu Jimbo Katoliki Dodoma. Mwaka 1971-1972 Juni aliteuliwa kuwa msimamizi wa kitume Jimbo la Dodoma.

CHANGAMOTO

Akiwa Padre mpya, Padre Mathias Isuja alipelekwa Parokia ya Kibakwe iliyokuwa ngumu kwa mzingira na watu wake, lakini aliendelea kufanya utume kwa muda wa miaka miwili. Baadaye aliteuliwa kuwa Katibu wa elimu Jimbo na kurudishwa Jimboni. Akiwa katibu wa elimu aliweza kusimamia shule za msingi, 75, shule za kati (milldle school) 6, na sekondari moja ya Bihawana zilizokuwa na jumla ya walimu 300. Padre Mathias akiwa anaendelea na kazi yake ya katibu wa elimu ndipo alipoteuliwa kuwa Makamu wa Askofu. Alifanya kazi nyingi alizotumwa na Askofu wake. Kwa sababu hiyo alifahamu magumu  na mepesi yote yaliyompata Askofu wake. Kwa mfano matatizo ya fedha na rasilimali watu aliyafahamu vizuri.

KUTEULIWA NA KUWA ASKOFU NA KUWEKWA WAKFU

Kufuatia kifo cha Askofu wa kwanza Jimbo la Dodoma, Mha. Antonio Geremia Pesce, tarehe 20,Desemba 1971, Juni 26, 1972 Padre Mtthias Isuja Joseph aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Dodoma na Papa Paulo wa sita. Aliwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo la Dodoma tarehe 17/09/1972, akiwa ni Askofu wa pili na pia Askofu wa kwanza mzalendo Jimboni.

KAZI ZA KIASKOFU.

Akiwa mchungaji mkuu wa Jimbo la Dodoma, Askofu Isuja alifuata vema nyayo za mtangulizi wake huku akijiwekea mikakati ya kupambana na dhana potofu ya utegemezi. Katika kipindi cha Uaskofu wake aliweza kuanzisha Parokia kadhaa ili kuhakikisha waamini wanapata huduma za kiroho. Parokia hizo ni Mlali, Rudi, Chipogoro, Kinyasi, Chalinze, Nzali, Hombolo, Handali, Mlowa Bwawani, Mpwayungu, Chikopelo, Haneti, Veyula, Miyuji Mbwanga, Kiwanja cha Ndege, Nkuhungu na Makole.

Hivyo mara baada ya kuwa Askofu alifungua Seminari ndogo ya Bihawana kwa ajili ya kuongeza idadi ya Mapadre na kuhimiza kilimo cha zabibu ili kupambana na tatizo la uchumi. Aliwahimiza waamini wake kulitegemeza Kanisa kwa njia ya matoleo badala ya kutegemea wahisani kutoka nje. Katika elimu alifanikiwa kuwaendeleza Mapdre wake kadiri ya uweze wake. Katika juhudi hizo alifanikiwa kutoa Maaskofu wawili. Akiwa Askofu Jimbo na hata baada ya kung’atuka ametoa Daraja Takatifu la Upadre kwa mapadre 102.

KATIKA UONGOZI WAKE TAASISI MBALIMBALI ZILIANZISHWA.

Bihawana seminari, Nyumba ya malezi ya waseminari wa Jimbo – Miyuji, Chuo cha ufundi Mpwapwa-Magogo, Chuo cha Ufundi Veyula, Chuo cha ufundi cha JohnBosco, Seminari ya chuo cha walimu cha Wasalesiani, Sekondary ya wasichana ya Masista wa Huruma, Kituo cha watoto walemavu Mlali, Kituo cha watoto wenye mtindio wa Ubongo (Cheshire Home Miyuji), Vyuo vya kilimo Ipala na Chikopelo, Holy Cross Centre, Hospitali ya Masista wa Mtakatifu Gemma Galgani Miyuji, Kituo cha Hija Mbwanga (Podium) Hostel ya Mapadre Kondoa, Nyumba ya watoto yatima Kondoa, Nyumba mpya ya Askofu na Ofisi za Jimbo.

MASHIRIKA YA KITAWA JIMBONI.

Licha ya kupokea na kuyaenzi mashirika ya kitawa yaliyokuweo Jimboni, Askofu Isuja alikaribisha mashirika mbalimbali ya kike na ya kiume ili kusukuma gurudumu la uchungaji. Mashirika hayo ni Jesuiti, Wasalesiani, Mapadre wa Damu Takatifu ya Yesu, Mabruda wa Upendo, Mabruda wa Mitume wa Yesu na Maria na kuanzishwa Shirika la Mabruda wa Jimbo wa Maria Mama wa Mkombozi (FIAT BROTHERS). Pia alialika Masista Wamissionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta, SMI, Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu, Waabuduo Ekaristi Takatifu, Watawa wenye huruma, Ursuline, na Habari Njema. Hawa wote waliendeleza utume wakishirikiana na mashirika ya Wakapuchini, Wapasionist, IVREA, Misericordia na Gemma Galgani ambao ndio Masita wa Jimbo la Dodoma na ambayo yalikuwepo kabla yake.

UTUME WAKE KWENYE BARAZA LA MAASKOFU

Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa tume ya haki na amani, Utume wa Walei, Idara ya Afya, Idara ya Fedha, na makamu Mwenyekiti wa T.E.C ni miongoni pia mwa Maaskofu waanzilishi wa majengo ya T.E.C ya Kurasini katika sura inayoonekana sasa kwa wakati huu. Askofu Mathias Isuja Joseph alistaafu mwaka 2004 na kumkabidhi Jimbo Baba Askofu Yuda Thaddeus Ruaichi mnamo February 20, 2005. Tangu wakati huo ameendelea kufanya kazi chini ya Askofu na pamoja na Askofu. Amekuwa mtii kwa Maaskofu wake, na alikubali kukabidhiwa kigango cha Ntyuka cha Parokia ya Kanisa Kuu. Amekihudumia kwa muda wote hadi sasa ni Parokia Teule.

Ameendelea kutoa ushauri, mafungo na mara nyingi hujisomea walau masaa mawili kwa kila siku. Askofu Mathias Isuja Joseph anapenda kuitwa “Mng’atuka” na siyo “Mstaafu”. Sababu ni kwamba Kung’atuka inamaanisha “Kupisha madaraka kwa wengine” kwa mujibu wa sheria na kanuni za Kanisa Katoliki.

Na mwandishi maalum toka Jimbo Katoliki Dodoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.