2016-04-18 07:40:00

Onesheni huruma kwa watu wa Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jumapili ya Kristo mchungaji mwema sanjari na maadhimisho ya Siku ya 53 ya Kuombea Miito Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Kanisa ni mama wa miito yote” ametoa Sakramenti ya Daraja Takatifu la Upadre kwa Mashemasi kumi na mmoja waliofundwa na kulelewa katika Jimbo kuu la Roma, changamoto na mwaliko wa kujitahidi kufanana la Kristo, Kuhani mkuu anayeunda taifa takatifu na ukoo wa kikuhani.

Mapadre wapya wanapaswa kukumbuka kwamba, wameteuliwa kutoka miongoni mwa watu ili kuwagawia watu wa Mungu Mafumbo ya Kanisa sanjari na kuendeleza kazi ya Kristo: Mwalimu, Kuhani na Mchungaji mwema, tayari kutumwa kwenda ulimwenguni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mapadre ni wasaidizi wa kwanza wa Maaskofu wanaoitwa na kutumwa kuwahudumia watu wa Mungu.

Mashemasi hawa baada ya kusali na kufundwa barabara, sasa wanainuliwa kuwa ni Mapadre, ili kuendeleza huduma ya Kristo: Mwalimu, Kuhani na Mchungaji mwema; daima wakishiriki kikamilifu katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, Watu wa Mungu na Hekalu la Roho Mtakatifu. Mapadre wapya watafananishwa n ana Kristo, Kuhani mkuu wa Agano la Milele; wao ni Makuhani wa Agano Jipya; hadhi inayowaunganisha na Maaskofu wao mahalia. Mapadre wanatumwa kutangaza na kushuhudia Injili; wanapaswa kuwa wachungaji wema wa Watu wa Mungu kwa njia mifano bora ya maisha; wataadhimisha Mafumbo ya Kanisa, lakini zaidi Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sadaka endelevu ya Kristo Msalabani.

Mapadre wanashiriki katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kufundisha na Kuhubiri Neno la Mungu ambalo wao wenyewe wamelipokea kwa furaha, kumbe, wanapaswa kudumisha kumbu kumbu na zawadi hii waliyopewa kupitia kwa wazazi, ndugu na jamaa zao; Makatekista na Kanisa katika ujumla wake. Watapaswa kuamini kile wanachosoma, kufundisha kile ambacho wanaamini na kuishi, kile wanachofundisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Watambue kwamba, wanapaswa kubeba ndani mwao kifo cha Kristo, tayari kutembea katika upya wa maisha unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba kielelezo makini cha sadaka ya Yesu mwenyewe.

Wawe ni viongozi wenye furaha, kwa kuwaenzi waamini wao, ili kwa njia ya mifano bora ya maisha, wasaidie kujenga na kulidumisha Kanisa la Mungu. Kama Mapadre, wataendeleza kazi ya kutakatifuza na kutoa sadaka takatifu kwa niaba ya Kristo na mchumba wake Kanisa. Kamwe mapadre wasichoke kuwa na huruma na kwa njia ya Mafuta Matakatifu watawafariji wagonjwa. Ni wajibu wao kushiriki kikamilifu katika Sala ya Kanisa, ili kuendelea kuwa ni sauti ya Mungu kwa waja wake. Mapadre watambue daima kwamba, wameteuliwa kutoka kati ya watu kwa ajili ya watu kwa mambo matakatifu, ili kumpendeza Mungu!

Baba Mtakatifu anawakumbusha Mapadre wapya kwamba wanashiriki katika utume wa Kristo, Kichwa na Mchungaji mwema, dhamana ambayo inawaunganisha na Maaskofu wao mahalia, ili kujenga na kudumisha mchakato wa umoja wa familia ya Mungu na kwamba, wao ni wahudumu wa umoja wa Kanisa, ili kuwapeleka watu kwa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu na Roho Mtakatifu. Mbele ya macho yao, waone daima mfano wa Kristo mchungaji mwema, aliyekuja kuhudumia na wala si kuhudumiwa na kutoa maisha yake, ili yawe ni fidia kwa wengi! Wawe na ujasiri wa kutoka na kuwaendea wale waliopotea!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.