2016-04-16 14:38:00

Wananchi wa Ugiriki wapongezwa kwa kuonesha mshikamano wa upendo!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Ugiriki, Jumamosi, tarehe 16 Aprili 2016, amempongeza na kumshukuru Bwana Alexis Tsipras, Waziri mkuu wa Ugiriki kwa moyo wa ukarimu na upendo unaooneshwa na kushuhudiwa na wananchi wa Ugiriki, hata katika umaskini wao! Amemwambia Waziri mkuu kwamba, yuko nchini Ugiriki ili kuzungumzia hali ya utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Nchi ya Ugiriki imekuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anawatia shime wananchi wa Ugiriki kama alivyofanya kwa wananchi wa Lampedusa, takribani miaka mitatu iliyopita! Mazungumzo ya viongozi hawa wawili anafafanua Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican kwamba, yamejikita katika masuala ya wakimbizi na wahamiaji, hali tete wanayokabiliana nayo Kisiwani Lesvos, huko Ugiriki.

Viongozi hawa wamekaza kusema, wahamiaji na wakimbizi ni changamoto ya kimataifa inayohitaji majibu muafaka na makini; kwa kuheshimu sheria za Jumuiya ya Ulaya pamoja na Sheria za Kimataifa. Baba Mtakatifu amewasifu na kuwashukuru kwa mara nyingine tena wananchi wa Ugiriki kwa kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi licha ya kukabiliwa na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa.

Wananchi wameshuhudia mshikamano na tunu msingi katika maisha ya binadamu! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, inalinda maisha ya watu, ili wasihatarishe maisha yao kwa kuzamia baharini ambako hawana uhakika wa usalama na maisha yao. Kuna haja pia ya kusimama kidete kupambana na biashara haramu ya binadamu ambayo inajificha pia katika wimbi la wakimbizi na wahamiaji wanaolazimishwa kuyakimbia makazi na nchi zao. Kuna biashara haramu ya magendo na safari hatarishi ambazo zinapaswa pia kudhibitiwa sanjari na kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Ulaya inaanzisha mchakato wa makazi salama kwa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.