2016-04-16 15:46:00

Salam na matashi mema kwa wakuu wa nchi mbali mbali!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea Kisiwa cha Lesvos nchini Ugiriki, Jumamosi asubuhi, tarehe 16 Aprili 2016 amewatumia salam na matashi mema wakuu wa Nchi ya Italia, Albania na Ugiriki, akiwatakia heri na matashi mema. Katika salam zake kwa wakuu wa nchi hizi, Baba Mtakatifu Francisko amesema kwamba, alikuwa anakwenda kuwafariji wakimbizi na wahamiaji. Amewaomba wakuu hawa wa nchi kumsindikiza katika sala na sadaka yao.

Kwa namna ya pekee, amewaombea wananchi wa Italia kuendelea kushikamana kwa dhati ili kukabiliana na changamoto za nyakati hizi! Kwa wananchi wa Albania, amewaombea amani na ustawi, kama ilivyokuwa pia kwa wananchi wa Ugiriki. Alipowasili kwenye Uwanja wa ndege wa Mytilene, nchini Ugiriki, Baba Mtakatifu Francisko amelakiwa na viongozi wa Serikali na Makanisa, wakiongozwa na Bwana Alexis Tsipras, Waziri mkuu wa Ugiriki.

Baba Mtakatifu Francisko, baada ya kuhitimisha hija ya upendo na mshikamano na wakimbizi pamoja na wahamiaji, akiwa njiani kurejea kutoka Kisiwa cha Lesvos, amewatumia tena salam na matashi mema wakuu wa Nchi ya Ugiriki, Albania na Italia. Amewashukuru wananchi wa Ugiriki kwa upendo na ukarimu wao. Ameahidi kuendelea kuwakumbuka wananchi wa Albania katika sala na sadaka yake na kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia, amemwelezea kwamba, huko Lesvos amekutana uso kwa uso na mahangaiko na matumaini ya wakimbizi na wahamiaji; wanaotamani kuona amani, utulivu na maendeleo yakishika mkondo kati ya watu wa mataifa! Amewatakia wananchi wa Italia kuendelea kuambata mafao na ustawi wa wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.