2016-04-16 16:23:00

Hakuna kulala, hadi kieleweke!


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaambia watendaji na wadau wa mradi Mabasi Yaendayo Haraka wa jijini Dar es Salaam (BRT) kuwa hawana muda wa kulala wa kupumzika na akawataka wakamilisha haraka vipengele vichache vilivyobakia ili mradi huo uweze kuanza kazi mapema iwezekanavyo.  Ametoa agizo hilo Ijumaa, Aprili 15, 2016 wakati akizungumza na wakuu wa taaasisi, watendaji wakuu na wadau wa mradi huo kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam. “Watu wa DART, UDA-RT hakuna muda wa kulala tena. Nanyi wa eGA, MAXCOM, POLISI NA SUMATRA inabidi mfanye kazi kama timu moja na wenzenu ili maeneo yaliyobakia yaweze kukamilika katika muda mfupi na kikubwa ni kuhakikisha mnatoa elimu ya kutosha,”alisisitiza.

Akielezea utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Bw. Ronald Rwakatare amesema miundombinu ya mradi huo imekamilika na utoaji huduma unatarajiwa kuanza hivi karibuni kwani hivi sasa wanamalizia ufungaji wa mfumo wa ukusanyaji nauli na uendeshaji wa mabasi hayo. Pia aliwataka wananchi kutunza miundombinu ya mradi huo na kuwa makini na matumizi ya barabara wakati mradi huo ukiwa kwenye majaribio na hatimaye kuanza kazi rasmi. Alisema watakuwa na karakana itakayotumika kwa ajili ya hayo mabasi ambayo itakuwepo eneo la Jangwani na kwamba ofisi za mradi pia zitakuwa eneo hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UDA Rapid Transit (UDA-RT), Bw. Robert Kisena amesema mpango wa kuanza kwa mradi huo umekamilila na tayari mabasi yote yamelipiwa kodi pamoja na bima. UDA-RT ni kampuni ya muunganiko wa UDA na wamiliki wa daladala ya kutoa huduma ya usafiri katika miundombinu ya mabasi yaendayo haraka. Bw. Kisena amesema kesho wataanza majaribio ya mradi huo kwa kutumia mabasi 10 na watakuwa wanaongeza mabasi 10 kila siku hadi yafikie 50 hivyo amewataka wananchi kuondoa shaka juu ya mradi huo.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Maxcom Africa, Bw. Juma Rajab amesema mabasi hayo yatakuwa yanatumia kadi za kielektroniki zitakazokuwa zinalipiwa kwa kutumia mitandao mbalimbali ya simu za mkononi. Bw. Rajab amesema Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kuanza kutumia mfumo huo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba fedha za mteja zitakuwa salama na hata kama atakapopoteza kadi yake.  “Mtu akinunua kadi yake anapaswa atunze namba ya usajili iliyoko kwenye kadi hiyo kwani itatumika kurudishia fedha zake kupitia namba yake ya simu ya mkononi,”alisema.

Amesema Maxcom Africa ndio wakusanyaji wa nauli kwa kushirikiana na UDA-RT ambapo watatumia mawakala wa MaxMalipo hivyo kila mwananchi atapata fursa ya kununua kadi yake kwa urahisi. Alisema taarifa za kila mtumiaji zitaunganishwa na simu yake ya mkononi ambapo mhusika ataweza kujua kwa urahisi salio la fedha lililomo kwenye kadi yake.

DART YAHIMIZWA KUELIMISHA WAKAZI WA DAR

Zikiwa zimebaki siku chache kabla ya mradi wa mabasi yaendayo kasi kuanza, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa taasisi zinazohusika na utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha wanatoa elimu kwa umma ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza. “Katika kipindi hiki cha majaribio, ambacho madereva wameanza kutumia barabara za BRT, hakikisheni mnatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu namna ya kuvuka barabara, kuzuia wenye bodaboda kutumia barabara hizo kuelezea na matumizi ya taa za barabarani kwa madereva wote,”amesema.

Ametoa agizo hilo Ijumaa, Aprili 15, 2016 wakati akizungumza na wakuu wa taaasisi, watendaji wakuu na wadau wa mradi huo kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam. Waziri Mkuu aliwataka watendaji wa wakuu wa taasisi wahakikishe wanapanua wigo na kutumia vyombo vya habari vingi kadri iwezekanavyo pamoja na mitandao ya kijamii katika kuelimisha raia juu ya zoezi hilo. Akifafanua kuhusu hatua zilizofikiwa kwenye mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale alisema miundombinu kwa ajili ya mradi huo imekamilika na usafiri huo utaanza hivi karibuni. Mhandisi huyo ametumia fursa huyo kutoa wito kwa wananchi kutunza miundombinu ya barabara hizo kwa sababu imeigharimu Serikali fedha nyingi.

Naye Mrakibu wa Polisi (SP), John Shawa kutoka Makao Mkuu ya Trafiki alisema kuanzia kesho zoezi la majaribio kwa mabasi yaendayo haraka litaanza hivyo amewaomba wananchi kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani. "Kuanzia kesho linapoanza zoezi la majaribio kwa mabasi yaendayo haraka ni vema watu wakatumia vizuri barabara hasa madereva wa bodaboda na madereva wengine watambue kuwa hawaruhusiwi kupita katika barabara hizo," alisema.

Imetolewa na Ofisi ya Waziri mkuu wa Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.