2016-04-15 15:40:00

Majandokasisi 11 Kupewa Daraja Takatifu la Upadre, Roma!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya  nne ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Yesu Kristo Mchungaji mwema, ambayo inaadhimishwa tarehe 17 Aprili 2016, majira ya saa 3:15 za asubuhi kwa saa za Ulaya anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoa Daraja Takatifu la Upadre kwa Mashemasi 11 kutoka Jimbo kuu la Roma ambao wamepata masomo na majiundo yao Kipadre mjini Roma.

Hii pia ni Siku ya 53 ya Kuombea Miito Duniani ambayo kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu “Kanisa ni Mama wa Miito”. Mwenyezi Mungu anawaita wote na kwamba, miito inazaliwa na kuibuliwa ndani ya Kanisa; inakua, inakomaa na kuimarishwa ndani ya Kanisa, changamoto kwa waamini kutambua na kuthamini umama na ubaba wa Jumuiya za waamini katika mchakato wa malezi, majiundo na makuzi ya Kipadre!

Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambamo Mapadre wanakumbushwa kwa namna ya pekee kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaokoa. Kumbe, wanapaswa kujivika fadhila ya huruma na kutenda kama Baba mwenye huruma katika maisha na wito wao wa Kipadre! Mapadre ni watumishi waaminifu wa huruma na msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa kutambua uzito wa maadhimisho Siku ya 53 ya Kuombea Miito Duniani, Jimbo kuu la Roma limefanya mkesha ili kusali kwa ajili ya kuombea miito mbali mbali ndani ya Kanisa, huku waamini wakiongozwa na Zaburi ya 17: huruma yako imenisaidia kukua na kukomaa; nyayo zangu zimeshikamana na njia zako! Ni kipindi cha katekesi ya kina kuhusu maisha na utume wa Mapadre kama vyombo na mashuhuda wwa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.