2016-04-15 08:37:00

Kanisa ni mama wa miito yote!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku ya 53 ya Kuombea Miito Duniani, ambayo kwa mwaka 2016 inaadhimishwa Jumapili tarehe 17 Aprili 2016, maarufu kama Jumapili ya Kristo Mchungaji mwema sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema, kila wito ndani ya Kanisa unapata chimbuko lake kutoka kwa Yesu Kristo anayemwangalia mja wake wa jicho la huruma! “Mwenyezi Mungu anatuita” ndiyo kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa ajili ya Siku ya kuombea miito mbali mbali ndani ya Kanisa, changamoto ya kukua na kukomaa katika maisha ya Kikristo, ili hatimaye kupewa dhamana na wito maalum wa kuweza kutekeleza katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, anawaalika waamini kutambua kwamba, wito wowote ule unapata chimbuko miongoni mwa watu wa Mungu na kwamba, hii ni zawadi ya huruma na udongo mzuri ambamo miito mbali mbali inaweza kuzamisha mizizi yake na kuzaa matunda mengi. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa na shukrani kwa jumuiya ya kitume sanjari na kumshukuru Mungu kwa wito wa kila mmoja wao. Mwenyezi Mungu anasamehe dhambi na kuwakirimia waja wake mwelekeo mpya wa maisha kama wafuasi wanaoshiriki utume wake.

Kila wito ndani ya Kanisa anasema Baba Mtakatifu unapata chimbuko lake katika jicho la huruma na mapendo kutoka kwa Yesu na kwamba, wongofu na wito ni sawa na chanda na pete; mambo yanayoambatana daima katika maisha ya mmissionari. Mwenyeheri Paulo VI, katika Waraka wake wa Kitume, Evangelii nuntiandi anafafanua kwa kusema kwamba, hatua ya kwanza ya mchakato wa Uinjilishaji ni kuwa sehemu ya Jumuiya ya Kikristo, mahali ambapo mwamini anapokea ushuhuda wa imani na utangazaji wa huruma ya Mungu.

Kuingizwa katika Jumuiya ya Kikristo kunaambatana na utajiri unaojikita katika maisha ya Kikanisa, hususan katika Sakramenti. Kanisa ni mahali ambamo waamini wanaamini lakini pia ni mahali ambapo waamini wanakiri Imani yao kwa Kanisa. Mwenyezi Mungu kwa njia ya wito anawaalika waamini kuwa ni sehemu ya Kanisa na baada ya kufikia ukomavu fulani, wanapewa wito maalum, dhamana wanayoshiriki pamoja na ndugu zao katika imani kwa Kristo Yesu.

Mwelekeo huu ni kinyume kabisa cha ubinafsi na hali ya kubeza na badala yake umoja na upendo vinajengeka na kuimarishwa ili kumwezesha mwamini kusadaka maisha yake kwa ajili ya huduma mintarafu mpango wa Mungu, kwa kuambata mazingira ya historia ya watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwajibika kikamilifu katika kutunza na kung’amua miito, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo. Jumuiya ya Kikristo haina budi kusali kwa bidii kwa ajili ya mang’amuzi, majiundo na mwendelezo wa miito.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa kuombea Siku ya Miito Duniani anakaza kusema, miito inazaliwa na kuibuliwa ndani ya Kanisa, kumbe, hapa kuna haja ya kuwa na mwelekeo wa Kikanisa na kwamba, wote wanaitwa kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa zima kwani karama yoyote ile ina mwelekeo wa Kikanisa na kwamba, ina uwezo wa kumwilishwa kwa amani katika maisha ya watu wa Mungu, kwa mafao ya wote. Kwa dhana hii, vijana wa kizazi kipya wataweza kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa Kikanisa kwa kuwa na mang’amuzi makubwa zaidi kuhusu karama na hivyo kuwa na mang’amuzi bora zaidi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa mwono huu, Jumuiya inakuwa ni nyumba na familia mahali ambamo miito mbali mbali inazaliwa! Watakaji wafanye tafakari ya kina na kutambua umuhimu wa Jumuiya katika maisha yao kwa siku za usoni. Wajifunze kuwafahamu na kuwapenda ndugu zao wanaofuata njia tofauti ya miito, lakini waimarishwe na vifungo vya umoja.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, wito unakua na kukomaa ndani ya Kanisa, kwa ajili ya mafao ya Jumuiya, jambo linalohitaji uzoefu na mang’amuzi kutoka kwa wanajumuiya wengine. Mfano kama huu unaweza kutolewa na Makatekista wanaoshirikisha kwa kiasi kikubwa ujumbe wa Kikristo bila kusahau Jumuiya za Kitawa ili kupata mang’amuzi ya Unjilishaji pembezoni mwa jamii, kwa kuonja maisha ya: Wamonaki; kwa kugundua hazina ya tafakari, kwa kushirikiana na Wamissionari ili kutambua dhamana na changamoto za Uinjilishaji wa awali; kuwa miongoni mwa Wakleri wa Jimbo ili kuzamisha zaidi uzoefu wa shughuli na maisha ya kichungaji. Kwa wale vijana ambao wako katika mchakato wa malezi na majiundo wanapaswa kutambua kwamba, Jumuiya ni msingi wa mazingira ya majiundo ya mtu, kumbe, anapaswa kuwa na moyo wa shukrani!

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, miito inaimarishwa ndani ya Kanisa kwa kuwa hapa Kanisa linaendelea kumfunda mwamini kuendelea kukuza utashi wake wa kuhudumia na kuendelea na mchakato wa majiundo endelevu. Na kwa wale ambao tayari wamekwishajisadaka katika maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake, wawe tayari kutumwa popote pale ambapo kuna mahitaji ya Kanisa, kwa kufuata mfano wa Mtakatifu Paulo na Barnaba. Wamissionari wanatumwa na kuungwa mkono na Jumuiya inayoendelea kuwa rejea ya daima na usalama kwa wale wanaosafiri kwenye maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu Francisko anasema katika shughuli za kichungaji, Wakleri wanao mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa, kwani wao wanapaswa kuwa ni mfano wa Kristo mchungaji mwema na kwamba, ukuzaji wa miito mitakatifu ni sehemu ya wajibu wao msingi sanjari na kuwasindikiza waamini katika mchakato wa kufanya mang’amuzi sahihi ya miito yao pamoja na kuwasaidia wale waliokwisha kusadaka maisha yao kwa ajili ya huduma kwa Mungu na Jumuiya kuendelea kudumu katika njia na nia hii njema.

Waamini walei wanahamasishwa na Mama Kanisa kutambua na kuthamini mwelekeo endelevu wa miito mbali mbali ndani ya Kanisa, ili Jumuiya za waamini kwa mfano wa Bikira Maria, ziweze kuwa ni Tabernakulo ya miito, kwa njia ya sala, malezi pamoja na kuwasindikiza vijana katika miito yao kutoka kwa Mungu. Umama wa Jumuiya ya waamini unajionesha kwa namna ya pekee katika kuwachagua wale wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya wito wa Kipadre na maisha ya kuwekwa wakfu. Kanisa ni mama wa miito yote kutokana na wajibu wake endelevu wa kuwatunza wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao.

Baba Mtakatifu Francisko anawaombea wale wote ambao wanajitaabisha katika njia ya kutafuta wito wao kuwa na utambuzi kwamba wao ni sehemu ya Kanisa; Roho Mtakatifu awaimarishe viongozi wa Kanisa na waamini walei ili waweze kutambua umuhimu wa umoja, mang’amuzi na tasaufi ya ubaba na umama.

Baba Mtakatifu Francisko anakamilisha ujumbe wake wa Siku ya 53 ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2016 kwa Sala maalum kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya huruma, kuwaimarisha waamini wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na Jumuiya; tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya pamoja na kuwakirimia hekima na busara ya utambuzi wa wito wao. Jumuiya za Kikristo ziwe kweli chimbuko la miito ya ukweli kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.