2016-04-15 15:17:00

Huduma na mshikamano na maskini ni mambo muhimu kwa jamii!


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 15 Aprili 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Juan Evo Morales Ayma wa Bolivia, ambaye baadaye pia amekutana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Viongozi hawa wawili katika mazungumzo yao, wameridhika na hali ya uhusiano mwema uliopo kati ya Vatican na Bolivia na baadaye, wamejielekeza zaidi katika masuala ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Baba Mtakatifu na Rais Evo Morales wamejikita zaidi katika mahusiano kati ya Kanisa na Serikali kwa kutambua na kuthamini Mapokeo ya Kikristo ambayo yamekuwemo nchini Bolivia kwa kipindi cha muda mrefu sanjari na mchango wa Kanisa katika maisha, ustawi na maendeleo ya wengi. Viongozi hawa baadaye wamegusia masuala muhimu katika maisha ya mwanadamu kama vile elimu, afya na msaada kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baadaye, wameangalia pia masuala ya kikanda na kimataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.