2016-04-14 11:21:00

Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi Duniani!


Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis limehitimisha mkutano wa siku tatu, uliowajumuisha wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi miongoni mwa watoto wadogo, mkutano uliofanyika kwa ushirikiano mkubwa na Hospitali ya Bambino Gesù inayosimamiwa na kuongozwa na Vatican. Lengo la mkutano huu, lilikuwa ni kutoa changamoto kwa makampuni ya dawa kusaidia mchakato wa kutoa dawa za kurefusha maisha kwa watoto ambao wameathirika kwa virusi vya ugonjwa wa Ukimwi!

Monsinyo Robert Vitillo, mtaalam mshauri wa masuala ya Ukimwi, Caritas Internationalis katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Jumuiya ya Kimataifa imepiga hatua kubwa katika kutoa dawa za kurefusha maisha kwa watu ambao wameathirika na Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi, lakini bado kuna idadi kubwa ya watoto wanaoendelea kupoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Ukimwi, kwa kukosa dawa za kurefusha maisha. Bila kuwa na mbinu mkakati wa kuwapatia watoto hawa dawa za kurefusha maisha, wengi wao watafariki dunia wangali wachanga! Takwimu zinaonesha kwamba, ni asilimia 32% ya watoto wanaopata dawa za kurefusha maisha, lakini asilimia nyingine 68% hawana fursa hii ambayo ingewasaidia kuishi kwa matumaini zaidi. Jambo la msingi ni kukuza huduma ya upimaji na hatimaye, kuwaingiza katika mpango mkakati wa kupatiwa dawa za kurefusha maisha.

Itakumbukwa kwamba, Caritas Internationalis kunako mwaka 2009 ilizindua kampeni ya kinga ya maambukizi ya virusi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, changamoto iliyofanyiwa kazi baadaye na Umoja wa Mataifa kama sehemu ya mchakato wa kupambana na maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi anasema Monsinyo Vitillo. Caritas na UNAIDS vinashirikiana kwa karibu sana katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi duniani. Kutokana na mkakati huu, maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto yamepungua na kwamba, huu ndio mkakati ambao kwa sasa unafanyia kazi na Jumuiya ya Kimataifa.

Monsinyo Vitillo anakaza kusema, ufanisi wa mkakati huu unategemea kwa kiasi kikubwa upimaji wa watoto ili kuangalia kwa kiasi gani wameathirika kwa virusi vya Ukimwi, tayari kuwaanzisha dawa za kurefusha maisha na aina ya dawa ambazo wanapaswa kupewa. Hapa wamiliki wa maduka makubwa ya dawa wanahamasishwa kuonesha upendo na ukarimu kwa watoto walioathirika kwa virusi vya Ukimwi, kwa kufanya tafiti za kina pamoja na kutoa msaada wa dawa kwa ajili ya huduma kwa watoto.

Monsinyo Vitillo anasema, Umoja wa Mataifa mwezi, Juni, 2016 utafanya mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Ugonjwa wa Ukimwi Duniani, changamoto ya Caritas Internationalis kwa kushirikiana na mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki ni uragibishaji “advocacy” ili kuzihamasisha Serikali na Makampuni makubwa ya dawa ili kuongeza juhudi katika mchakato wa kupambana na ugonjwa wa Ukimwi. Caritas Internationalis inatarajia kushiriki kikamilifu katika mkutano huu kwani ni mdau mkubwa na mtetezi wa maskini na wanyonge duniani. Mkutano huu unatarajiwa pamoja na mambo mengine, kutoa tamko la kisiasa katika mapambano dhidi ya virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi Duniani na kwama, Serikali zitapaswa kujihusisha kikamilifu katika utekelezaji wa mkakati huu kama sehemu ya kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.