2016-04-14 07:06:00

Mageuzi ndani ya Vatican yaanza kupata sura mpya!


Padre Frederico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Mkutano wa kumi na nne wa Baraza la Makardinali washauri uliokuwa unaongozwa na Baba Mtakatifu Francisko umehitimishwa na kwamba, ushauri aliopewa Baba Mtakatifu sasa unaanza kupata sura mpya ya utekelezaji wake, kwa kuchapisha Katiba mpya itakayokuwa ni dira na mwongozo wa shughuli za Sekretarieti ya Vatican.

Mkutano huu umehudhuriwa na Makardinali nane, isipokuwa Kardinali Gracias ambaye hakuweza kuhudhuria kutokana na sababu za kiafya. Sehemu kubwa ya ushauri uliotolewa unagusia Mabaraza ya Kipapa ambayo tayari yamekwisha jadiliwa, lakini kwa namna ya pekee, wamegusia: Baraza la Kipapa la nidhamu na Sakramenti za Kanisa; Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu pamoja na Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu ya Kanisa.

Makardinali washauri wamehitimisha mchakato wa kuundwa upya kwa Mabaraza mawili ya kipapa yaani: Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha; Pili ni Baraza la Kipapa la haki, amani na uhamiaji. Baraza hili litashughulikia na kuratibu misaada ya Kanisa Katoliki pamoja na shughuli za kichungaji kuhusiana na masuala ya afya. Makardinali baada ya ushauri wao wa mwisho, sasa Baba Mtakatifu Francisko amechiwa dhamana ya kufanya maamuzi na utekelezaji wake!

Makardinali wamejadili pamoja na mambo mengine nyeti katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuangalia vigezo muhimu kwa ajili ya wakleri wanaoweza kuteuliwa kuwa Maaskofu mahalia mintarafu utambulisho wao, utume na shughuli zao za kichungaji. Makardinali wamegusia maana na umuhimu wa Mabalozi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali George Pell, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya uchumi ya Vatican pamoja na KardinaliSeàn Patrick O’Malley, Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa ya Ulinzi kwa watoto wametoa taarifa zao kwa Baraza la Makardinali washauri. Mwishoni, Makardinali washauri wamekusanya na kuhariri michango mbali mbali ili kutengeneza muswada utakaowasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko, tayari kutekeleza mchakato wa mageuzi ya Sekretarieti kuu ya Vatican.

Taarifa inaonesha kwamba, Makardinali washauri katika kipindi cha mwaka 2016 watakuwa na mikutano yao tarehe 6- 8 Juni; tarehe12- 14 Septemba na tarehe 12- 14 Desemba, 2016. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itaendelea kukujuza yale yanayojiri katika mchakato wa mageuzi haya yanayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Makardinali katika vikwao vyao elekezi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.