2016-04-14 09:50:00

Iweni mashuhuda wa imani katika matendo!


Jumuiya ya Wascotland mjini Roma, inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 400 tangu Chuo cha Kipapa cha Scotland kilipogeuzwa kuwa ni Seminari kwa ajili ya majiundo na malezi ya majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya maisha na wito wa Kipadre. Tukio hili la kijasiri lilitokea kunako tarehe 11 Machi 1616 wakati ambapo wanaume wa shoka kumi na sita walipoamua kurejea nchini Scotland kama Mapadre ili kutangaza na kushuhudia Injili, maamuzi ambayo yalikuwa yanabubujika kutoka katika damu ya mashuhuda wa imani!

Ushuhuda wa kifodini cha Mtakatifu Yohane Ogilvie kililenga kufunga mdomo imani ya Kanisa Katoliki, lakini kikawa ni chachu ya Wakatoliki kusimama kidete kuendeleza na kulilinda Kanisa, huku wakiwa wameungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ndiyo iliyotamkwa na kushuhudiwa na wanaume kumi na sita wa shoka, miaka mia nne iliyopita, kilikuwa ni kielelezo cha watu waliokuwa wamejiandaa kikamilifu na kudhamiria kurejea nchini Scotland ili kukabiliana na changamoto za maisha zilizokuwa mbele yao, hata ikiwa ni kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake!  Damu ya Mtakatifu Yohane Ogilvie na ushuhuda wa wanaume wa shoka, umezaa matunda mengi nchini Scotland.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 14 Aprili 2016 alipokutana na kuzungumza na Jumuiya Wascoland wanaoishi mjini Roma. Baba Mtakatifu amewakumbusha wanajumuiya kwamba, hata wao wanaishi katika kipindi cha mashuhuda wa imani kwani tamaduni na mazingira mamboleo kwa kiasi kikubwa yamekuwa ni kikwazo kwa ajili ya kuenea kwa Injili ya Kristo, changamoto ya kujitosa bila ya kujibakiza kama walivyofanywa watangulizi wao sanjari na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake. Majando kasisi wawe makini katika mchakato wa majiundo na malezi ya kipadre, ili muda huu wanapokuwa hapa Roma uwasaidie kujiunda vyema, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake wanaporejea nchini mwao! Majandokasisi hawa wakiwa na upendo kwa Kristo, Kanisa na nchi yao kama ndugu zao, miaka mia nne iliyopita, wataweza kuipamba historia ya nchi yao na sadaka ambayo wanaiadhimisha wakati huu.

Majandokasisi hawa watakuwa kweli ni alama kwa wananchi wa Scotland, hususan miongoni mwa vijana, ikiwa kama watafanikiwa kukutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku pamoja na kuwaendelea wale ambao wamejitenga mbali na Kristo. Baba Mtakatifu anawaalika Majandokasisi kuwaonesha watu hawa uwepo endelevu wa Mungu kati yao na kwamba, huruma yake ya dumu milele. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu anawaombea ili waweze kuwa na ari, ujasiri na neema ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao na kwamba, anawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.