2016-04-14 16:03:00

Balozi mpya wa San Marino awasilisha hati za utambulisho kwa Papa!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 14 Aprili 2016 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mama Maria Alessandra Albertini, Balozi mpya wa Jamhuri ya Watu wa San Marino, mjini Roma. Balozi Albertini alizaliwa kunako tarehe 14 Machi 1961, ameolewa na amebahatika kupata watoto wawili katika maisha yake.

Katika maisha yake ya kidiplomasia, kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 1993 alikuwa ni mfanyakazi katika Idara ya ushirikiano na mambo ya nchi za nje ya San Marino. Kunako mwaka 1993 akateuliwa kuwa mshauri wa balozi katika Idara ya mambo ya nchi za nje, kitengo cha siasa. Kunako mwaka 1997- 2014 alikuwa ni Kamishina wa UNICEFU, San Marino. Kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2005 alikuwa ni Makamu wa Rais Pan- Europe, huko San Marino.

Amewahi kuwa ni Mwakilishi wa San Marino nchini Malta na Cyprus kuanzia mwaka 2000. Baadaye alikuwa ni mfanyakati katika idara mbali mbali za shughuli za kitamaduni, masuala ya watoto kimataifa na mratibu wa shughuli za mahusiano na Jumuiya ya Ulaya, kazi ambayo ameifanya kati ya mwaka 2012- 2014. Baadaye akateuliwa kuwa Mkurugenzi mkuu wa masuala ya kisheria kama waziri wa Sheria katika Idara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa kuanzia mwaka 2014.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.