2016-04-13 07:23:00

Mapambano ya biashara haramu ya binadamu!


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe ili kupambana fika na wimbi la biashara haramu ya binadamu matokeo ya uhalifu wa kutumia nguvu. Ili kufanikisha azma hii kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa dhati katika mapambano haya sanjari na kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kulinda na kudumisha haki msingi za waathirika wa biashara hii, licha ya changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa kuwatambua na kuwasaidia!

Huu ni mchango uliotolewa na Monsinyo Janusz Urbanczyk, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye mkutano wa kumi na sita wa Shirikisho la Usalama na Ushirikiano Ulaya, OSCE ambaye amekazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa kuheshimu na kuthamini haki msingi za binadamu kama zinavyobainishwa na Tamko la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Biashara haramu ya binadamu ni uhalifu dhidi ya ubinadamu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Uhalifu huu unapaswa kutambuliwa na Jumuiya ya Kimataifa, ili kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu!

Wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi, linaloendelea kuzua changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa si tu kwamba, haya ni matokeo ya vita, nyanyaso na dhuluma; kinzani na mipasuko ya kisiasa na kijamii sanjari na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu, lakini pia ni matokeo ya biashara haramu ya binadamu inayoendelea kuwanufaisha wajanja wachache ndani ya jamii.

Biashara hii ina madhara makubwa kwani inapokonya nguvu kazi na rasilimali muhimu katika ujenzi na ukuaji wa uchumi! Sababu mbali mbali zinaendelea kuchangia mchakato wa uhamiaji wa hiyari pamoja na ule wa nguvu! Changamoto hii inahitaji kuwa ni sheria na mielekeo mipya ili kuweza kukabiliana na wimbi hili, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watoto, ambao baadaye wanajikita wakiwa wameingizwa katika vitendo vya kihalifu.

Biashara haramu ya binadamu inakua na kukomaa miongoni mwa maskini na watu waliokata tamaa; watu wanaotaka kusalimisha maisha yao kutokana na vita pamoja na hali ngumu ya maisha. Ndiyo maana Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutafuta ufumbuzi muafaka wa changamoto hii badala ya kujenga kuta za ubaguzi na utengano kati ya watu. Sera makini inahitajika ili kupambana fika na donda ndugu la biashara haramu ya binadamu duniani. Haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kuheshimiwa na wote!

Wakati huo huo, Monsinyo Janusz Urbanczyk, akichangia mada kwenye mkutano wa mshikamano dhidi biashara haramu ya binadamu anakaza kusema, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika mfumo wa biashara haramu ya binadamu inayoendelea pia kujikita katika uhalifu na udhalilishaji wa utu na heshima ya binadamu! Anatambua kwamba, mchakato wa uhamiaji ni dhana pevu inayoambata changamoto na magumu mengi ya maisha ambayo wakati mwingine yanaacha athari za kudumu katika maisha ya watu!

Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kupongeza juhudi zinazofanywa na mashirika yasiyo ya kiserikali katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na kwamba, umefika wakati wa kuratibu shughuli hizi katika kiwango cha kimataifa pamoja na kuwa na sheria maalum kuhusu changamoto hii! Ni vyema ikiwa kama watu watafahamu mchakato unaoweza kuwatumbukiza katika biashara haramu ya binadamu na hatimaye, kugeuzwa kuwa ni vyombo vya uhalifu wa kimataifa. Hapa kuna haja ya kuwa na kanuni na taratibu za kawaida kwa ajili ya wahamiaji na wakimbizi ili kuepuka athari za uhamiaji wa kulazimishwa!

Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu pamoja na kuwasaidia waathirika wa biashara hii. Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na sera na mikakati ya kukabiliana, kuwahudumia pamoja na kuwasaidia waathirika wa biashara haramu ya binadamu! Vatican inaunga mkono mchakato wa uundwaji wa ushirikiano wa kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu!

Monsinyo Janusz Urbanczyk anakaza kusema, kuna haja ya kutambua na kuthamini haki msingi za waathirika wa biashara haramu ya binadamu; kwanza kabisa kwa kuwatambua na hatimaye kuwalinda. Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika huduma hii kwa waathirika wa biashara haramu ya binadamu. Wahanga hawa wamekuwa wakitumbukizwa katika biashara haramu ya viungo vya binadamu, utumwa mamboleo, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na vitendo vya uvunjaji wa sheria.

Waathirika wakubwa ni watoto na wanawake, changamoto inayopasa uwajibikaji makini! Hapa kuna haja ya kuwa na sera na vyombo ambavyo vitasaidia kuwatambua, kuwalinda na kuwahudumia waathirika wa biashara haramu ya binadamu mipakani. Ili kufanikisha azma, wataalam waliobobea katika shughuli hii wanahitajika haraka iwezekanavyo sanjari na kujenga moyo wa mshikamano ili watu hawa wanapokombolewa waweze kupata huduma makini.

Ni matumaini ya ujumbe wa Vatican kwamba, Jumuiya ya kimataifa itaweza kuibua mbinu mkakati na sera makini zitakazotumika katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu katika ngazi ya Kikanda na Kimataifa. Hapa juhudi zaidi zielekezwe katika kuzuia, kuboresha hali ya maisha ya watu, kutambua na kuwahudumia waathirika wa biashara haramu ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.