2016-04-13 08:43:00

Maisha na utume wa Kanisa Kaskazini mwa Afrika!


Shirikisho la Baraza la Maasofu Katoliki Afrika ya Kaskazini, CERNA, hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mwanzo wa Mwaka uliofanyika huko Tangeri, Morocco kwa kujikita zaidi katika mchakato wa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa ni changamoto kubwa ya kitaifa na kimataifa. Tamko la CERNA lililotiwa mkwaju na Askofu Paul Desfarges, Rais wa CERNA linaliangalia Kanisa Katoliki nchini Tunisia kwa imani na matumaini katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani, maridhiano baada ya mapinduzi yaliyofanyika kunako mwaka 2011.

Licha ya changamoto na magumu yaliyojionesha katika kukabiliana na vitendo vya kigaidi kama yale mauaji ya kinyama yaliyotokea Mwezi Machi 2015 kwenye Makumbusho ya Taifa ya Bardo. Kanisa Katoliki nchini Tunisia linaendelea kutekeleza maisha na utume wake kwa kujikita zaidi sekta ya elimu, huduma za kijamii na mshikamano katika kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu, hususan wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Nchini Morocco, Kanisa linapenda kujielekeza zaidi katika majadiliano ya kidini; utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya na huduma makini kwa watu wanaokabiliwa na hali ngumu ya uchumi na maisha, bila kusahau kwamba, Morocco inakabiliwa pia na changamoto ya uwepo wa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha yao. Algeria kwa upande wake, inakabiliwa na athari za mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa baada ya bei ya nishati ya petroli kuanguka katika soko la dunia.

Kanisa nchini Algeria, bado linasubiri kwa hamu kupata mchungaji mkuu wa Jimbo kuu la Algiers pamoja na Balozi wa Vatican nchini humo! Hata hivyo familia ya Mungu inaendelea kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Charles de Foucald, maadhimisho ambayo yanakwenda sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kanisa pia linawakumbuka Wamonaki wa Tibhirine waliouwawa kikatili, kunako mwaka 1996, takribani miaka 25 iliyopita!

Shirikisho la Baraza la Maaskofu katoliki Kaskazini mwa Afrika linasema, bado kuna changamoto nyingi katika uundaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Libya, lakini kuna cheche za matumaini, ingawa hakuna Askofu kutoka Libya aliyehudhuria mkutano huu. Maaskofu wamefahamishwa hali ngumu ya maisha na utume wa Kanisa nchini Libya; matatizo na changamoto kwa wahamiaji na wakimbizi na kwamba, kuna baadhi ya Mashirika ya kitawa ambayo bado kwa ari na moyo mkuu yanaendelea kutekeleza utume wao miongoni mwa wananchi wa Libya wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha, kielelezo cha mshikamano wa huduma ya upendo. Ni matumaini ya familia ya Mungu nchini Libya kwamba, haki, amani, usalama na utulivu vitaweza kurejea tena nchini humo, ili kutoa fursa kwa wananchi kuendelea na maisha yao ya kawaida!

Jimbo Katoliki la Nouakchott nchini Mauritania, linajiandaa kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na kwamba, familia ya Mungu nchini humo inaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka. Askofu Domenico Mogavero wa Jimbo Katoliki la Mazara del Vallo, Sicilia, nchini Italia ameshiriki katika mkutano huu na kuwaelezea Maaskofu wa CERNA hali halisi ya wakimbizi na wahamiaji wanaohifadhiwa nchini Italia na kwamba, makubaliano yaliyofikiwa kati ya Umoja wa Ulaya na Serikali ya Uturuki ya kuwarejesha makwao wahamiaji na wakimbizi walioingia nchini Uturuki baada ya tarehe 20 Machi 2016 kupitia mipaka ya Uturuki ni kinyume cha haki msingi za binadamu, utu na maisha ya wakimbizi na wahamiaji.

CERNA katika maisha na utume wake, linaihamasisha familia ya Mungu Ukanda wa Afrika ya Kaskazini kuhakikisha kwamba, inajikita katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo yenye mvuto na mashiko, kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam ili kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani, upendo, maridhiano na umoja wa kitaifa. Kanisa Katoliki katika masuala ya kijamii na kiuchumi, linapenda kuonesha upendo na mshikamano wake wa dhati kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Waamini wanachangamotishwa kuonesha upendo na mshikamano kwa kujenga na kushuhudia udugu na upendo wa Kristo Yesu, kati yao; kwa kusikiliza Neno la Mungu na kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa. Ushuhuda huu wa upendo, uwe ni kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! CERNA inakumbusha kwamba, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji ni ya kimataifa na kwamba, hata katika Nchi za Kiafrika kuna wakimbizi wanaohudumiwa kwa hali na mali!

Jumuiya ya Ulaya isidhani kwamba, ndiye pekee yenye changamoto ya wakimbizi na wahamiaji kwa nyakati hizi. Hakuna sababu ya msingi ya kuogopa kuwapokea na kuwakirimia kwa upendo wakimbizi na wahamiaji kutoka dini ya Kiislam kwani hii ni hofu isiyokuwa na tija. Wananchi wa Ulaya waoneshe upendo na ukarimu kwani mengine yote yanapita, lakini upendo hudumu daima. Shirikisho la Baraza la Maaskofu Katoliki Kaskazini mwa Afrika, litafanya mkutano wake wa mwaka, Januri 2017 huko Senegal.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.