2016-04-13 10:53:00

Jumapili ya Kuombea Miito Mitakatifu nchini Tanzania!


Ndugu wapendwa katika utume wa Kimisionari, Katika siku hii Baba Mtakatifu Francisko anatualika wabatizwa wote kujisikia furaha ya kuwa sehemu ya Kanisa kwa sababu wito wetu wa ukristo ni zawadi kutokana na upendo wa huruma ya Mungu. Ni zawadi tuliyopewa na Mungu bila mastahili yetu. Kupitia Kanisa, zawadi hii imekua na kustawi. Hivyo, Baba Mtakatifu anatualika kutafakari juu ya wito wetu wa Kikristo na kutoa shukrani kwa fursa ya jumuiya katika safari yetu ya kiwito ya kila mtu.

Baba Mtakatifu Francisko anatualika katika siku hii ya miito tuone umuhimu wa Kanisa kama jumuiya ya Wakristo kusaidia na kuimarisha miito mitakatifu. Mwito wa Mungu hutujia kwa njia ya tafakari ambayo ni ya kijumuiya. Mungu hutuita ili kuwa sehemu ya Kanisa. Baba Mtakatifu anatualika pia kuwa na familia nzuri ambapo miito itachipuka kupitia vyama vya kitume kwa watoto na vijana. Baba Mtakatifu anatualika kuwa siku ya kuombea miito itukumbushe wajibu wetu wa kuitunza, kuifadhili na kuwa na mang’amuzi ya kutambua miito. Miito huzaliwa na kukua ndani ya Kanisa. Hivyo Kanisa ni mama wa miito kama ilivyo kauli mbiu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Dominika ya kuombea Miito Duniani mwaka huu, 17 Aprili 2016.

Familia zetu ziwe Kanisa dogo la Mungu ambamo ndani yake miito huzaliwa. Baba Mtakatifu anawaalika wanafunzi walio katika malezi kukomaa vyema katika wito wao kwani wameitwa ili kuwa tayari kutumwa ndani ya Kanisa mahalia na wawe tayari kutumwa sehemu yo yote ya Ulimwengu wanapohitajika. Baba Mtakatifu anawaalika Mapadri kama walezi wa miito Mitakatifu kuwa wanawajibika katika utume wao wa kutimiza mwito wa Bwana Yesu Kristo anayesema “Mimi ndimi mlango wa kondoo”. “Mimi ndimi mchungaji mwema” (Yoh. 10: 7-10). Mapadri wajue kuwa wao ni nguzo muhimu katika kukuza na kulea miito kwa maneno na mifano yao ya ushuhuda wa maisha yao.

Mapadri wanawajibika kusaidia katika mang’amuzi ya wito, pia kusaidia kiroho wale wote waliojiweka wakfu kumtumikia Mungu na jumuiya ya waamini. Tunaalikwa kufuata mfano wa Bikira Maria kuitikia wito wetu kwa Mungu, (Lk 1:35-38, Mdo. 1:14”). Wote walio katika safari ya wito wajue kuwa wito ni zawadi ya Mungu waliyopata bila mastahili yao na wawe na uelewa wa kina kuwa wito ni mali ya Kanisa na Kanisa ni mama wa Miito.

Maadhimisho muhimu katika Kanisa la Tanzania: Tunapoendelea kuadhimisha Jubilei ya pekee ya Huruma ya Mungu tunawaalika kufanya maandalizi ya kutosha ya maadhimisho ya miaka 150 ya Mlango wa Imani Uinjilishaji Bagamoyo Tanzania. Ni Jubilei ya miaka 150 ya Kanisa la Tanzania 1868-2018. Hivyo kilele cha maadhimisho yetu ya miaka 150 ni mwaka 2018, Jubilei ya Imani pia kwa Kanisa la nchi za Afrika Mashariki. Ni miaka 150 ya shukrani, Neema na Baraka ya Mungu kwa Kanisa la Tanzania. Ni zawadi ya ukomavu wa Imani yetu kwa Kristo Mfufuka katika Kanisa lote la Tanzania. Tunaelekea kuadhimisha kilele cha jubilee ya miaka 100 ya Daraja la Upadri kwa Kanisa la Tanzania, kwani kwa mara ya kwanza Daraja la Upadri lilitolewa katika maeneo ya Vikarieti ya Kanda ya ziwa Victoria (1917-2018). Wakleri wote tuendelee kufanya tafakari juu ya kutoa ushuhuda wa wito wetu kama tulivyoazimia (2016 – 2017).

JUMAPILI YA KUOMBEA MIITO DUNIANI

Ni kipindi cha kutathmini juu ya wito wa huduma ya Daraja la Upadre na wajibu wetu kwa Mungu na Kanisa. Maadhimisho yote ya Kikanisa tuyafanyayo kuelekea kilele cha Jubilei ya miaka 150 ya Mlango wa Imani tuyaweke mikononi mwa Mungu kwa maombezi ya Bikira Maria Malkia wa Mitume, Malkia wa amani, na mwombezi wa Taifa letu la Tanzania. Pamoja na maadhimisho mengine tuliyo nayo Mwaka huu tuna Maadhimisho ya miaka 100 ya Shirika la Kipapa la umoja wa Wamisionari ( The Pontifical Missionary Union). Shirika hili lilianzishwa mwaka 1916. Hivyo ni kipindi cha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake 1916 – 2016.

Lengo kuu la Shirika hili ni kuhamasisha roho ya kimisionari miongoni mwa mapadri wazalendo wa Kanisa mahalia, Watawa wa kike na wa kiume, Waseminari, Seminari Kuu, Makatekista na Walei waliowekwa wakfu, Watumishi wa Uchungaji na wale waliojikita katika Katekesi na mafundisho ya dini. Kauli mbiu ya Shirika hili: “Sisi sote ni Wamisionari”. Shirika hili katika mazingira ya Kanisa la Tanzania, huunganisha RSAT ( Mashirika ya Kitawa ya wanaume); TCAS ( Mashirika ya Kitawa ya wanawake) na UMAWATA (Mapadri wa Jimbo Tanzania), Mapadri wa Mashirika Tanzania, Fidei Donum na Walei wote kufanya kazi ya Uinjilishaji. Kutokana na ubatizo wetu tunaalikwa kutangaza Habari Njema kwa Mataifa yote (1Pet 2:9) tukishuhudia Imani tuliyoipokea.

SHUKRANI: Dominika ya nne ya Pasaka ni siku ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya miito Mitakatifu. Ni siku tunapotolea shukurani zetu kwa Mungu kwa zawadi ya kazi ya Shirika la Kipapa la Kimisionari la Mtakatifu Petro Mtume. Malengo ya Shirika hili ni: Kuhamasisha miito ya Upadre wa Kanisa mahalia na wa maeneo ya Misioni Duniani. Kuwaalika waamini ili washiriki kikamilifu katika kutoa ukarimu wa hali na mali kwa ajili ya malezi ya waseminari na watawa wanawake na wanaume katika nchi za Misioni. Kuhamasisha roho ya Kimisionari miongoni mwa walelewa.

Mwaliko: Baraza la Maaskofu Katoliki linatualika sisi sote wadau wa Shirika la Kipapa la Kimisionari la Mtakatifu Petro Mtume: Kusali bila kukoma kwa ajili ya Miito ya Mapadri wa Jimbo na wamisionari kwa mujibu wa Tamko la Yesu “Mwombeni Bwana wa Mazao awatume watu kwa ajili ya mavuno yake” Mt. 9:37-38. Tunaalikwa kuadhimisha Dominika ya Miito au Dominika ya Nne ya Pasaka au Dominika ya Mchungaji Mwema kwa sala, mazoezi ya kiroho na kutoa ukarimu kwa michango yetu kwa Seminari na nyumba za malezi ya kitawa. Kutoa au kulipia ada za masomo ya mseminari mmoja mmoja, vifaa na mahitaji mbali mbali ya elimu katika Seminari zetu ndogo na kubwa. Kuwadhamini waseminari hadi wapatapo daraja la Upadre. Kugharimia ujenzi au uendeshaji wa Seminari mpya, ukarabati mkubwa wa majengo ya zamani ya Seminari na miundo mbinu yake. Kwa niaba yangu na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania tunachukua nafasi hii kuwashukuru sana wote mliotoa ukarimu wenu kwa kuchangia mfuko wa pamoja wa Miito Mitakatifu na kutegemeza Miito Mitakatifu 2015.

Ukarimu wetu kwa Kanisa lote la Mungu unaongezeka mwaka hadi mwaka kama mnavyoona kwenye takwimu zilizo mwishoni mwa ujumbe huu. Ukarimu wetu unaendelea kuimarika mwaka kila mwaka. Tunapenda kutumia nafasi hii kwa niaba yangu mwenyewe na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kutoa shukrani zetu kwa Majimbo yote, Mashirika ya kitawa, taasisi za elimu ya juu, seminari zetu ndogo na Kubwa, familia, watu binafsi na wote wenye mapenzi mema kwa ukarimu wenu. Tunawaalika kutoa ukarimu wenu katika mfuko wa pamoja kwa mahitaji ya nchi zetu za misioni na mahitaji yetu katika Kanisa letu mahalia, kama tunavyoalikwa na Baba Mtakatifu katika Ujumbe wake. Mahitaji katika seminari zetu za majimbo na nyumba za malezi ya kitawa na taasisi zinazohitaji kusaidiwa kupitia mfuko huu wa Uinjilishaji zinaongezeka.

Tukumbuke kuwa wale waliosaidia kufadhili shughuli wamepungua sana au hawapo kabisa. Tunapoadhimisha miaka 150 ni ishara kuwa Kanisa la Tanzania limekomaa kiasi cha kushiriki kikamilifu kutegemeza mfuko huu wa pamoja na kujitegemeza sisi wenyewe katika kulea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa letu. Tunawaalika pia wale wote ambao hamjaweza kupata fursa ya kuchangia Mfuko huu wa Pamoja tushiriki kikamilifu ili kuitikia mwaliko wa Baba Mtakatifu kupitia ujumbe wake katika Dominika ya kuombea Miito Mitakatifu duniani 2016. Asanteni sana kwa ukarimu wenu na Mungu Mwema azidi kuwabariki. Kheri nyingi kwa sherehe ya Pasaka Wenu katika huduma ya Utume wa Kimisionari

+Damian D. Dallu Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Songea Na Mwenyekiti wa Tume ya Kimisionari Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.