2016-04-12 10:32:00

Silaha za sumu zina madhara makubwa kwa binadamu!


Monsinyo Ivan Jurkovic, mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, hivi karibuni wakati akichangia mada kwenye mkutano wa kimataifa wa wataalam wa Mfumo wa Silaha za Sumu zinazojiendesha zenyewe anasema, hii ni mada nyeti ambayo imekuwa ikijadiliwa kwa takribani miaka mitatu kwa mfululizo, changamoto kwa wajumbe kushirikisha kikamilifu mawazo yao ili hatimaye, kuwa na maamuzi mazito wakati wa mkutano wa kimataifa wa kuangalia upya Mfumo wa Silaha za sumu, unaotarajiwa kufanyika Desemba 2016.

Monsinyo Jurkovich anasema, mwelekeo sahihi ni kuzuia utengenezaji na usambazaji wake kwani historia na uzoefu vinaonesha kwamba,  silaha nyingi zimekuwa ni chanzo cha majanga katika maisha ya binadamu kama inavyojionesha kwa silaha za kinyuklia, mabomu ya kutegwa ardhini. Madhara yake kwa maisha ya binadamu ni makubwa pale ambapo udhibiti unachelewa. Kumbe, kuna haja ya kuvunjilia mbali mzungo wa mashindan ya teknolojia na nguvu yake ya kusababisha madhara kwa maisha ya binadamu. Hii ni njia sahihi ya kudumisha sheria za binadamu kimataifa!

Madhara ya silaha za sumu zinazojiendesha zenyewe ni makubwa kwani hapa mashini inaachiwa uwezo wa kuamua kuhusu hatma ya maisha ya mwanadamu pasi na kuwajibika. Hapa mkazo ni kutaka kujenga na kudumisha mchakato wa kuimarisha amani badala ya kujikita katika vita, kwa kuwa na mawazo sahihi; mataifa kuheshimiana badala ya watu kujenga wasi wasi na hofu. Kanuni maadili inayojikita katika upendo na udugu ni muhimu sana kati ya mahusiano ya kimataifa.

Monsinyo Jurkovich anaendelea kufafanua kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwezeka zaidi katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano; kudhibiti vitendo vya kigaidi; kwa kudumisha haki msingi za binadamu, kuheshimu makundi madogo madogo pamoja na kujenga mazingira ya kuwashirikisha wananchi wengi katika masuala ya kisiasa na maendeleo yao.

Matumizi ya sheria kudhibiti uzalishaji wa silaha za sumu zinazojiendesha zenyewe kamwe hayatasaidia kupata ufumbuzi wa kudumu. Umefika wakati wa kudhibiti sheria ambazo zinaweza kumtumbukiza mwanadamu katika majanga. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya maamuzi  magumu ya kuzuia utengenezaji wa silaha za sumu zinazojiendesha zenyewe, kama ilivyowahi kufanya kwa miaka ya nyuma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.