2016-04-12 09:22:00

Mchakato wa ujenzi wa amani duniani!


Amani ya kweli kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa inajikita katika toba na wongofu wa ndani; upendo, udugu na mshikamano wa kweli unaosimamiwa na kuongozwa na kanuni auni. Katika jamii inayosimamia msingi wa amani ya kweli hakuna bwana wala mtwana, bali wote ni ndugu wamoja, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Haya ndiyo mambo msingi yanayozingatiwa na Chama cha Pax Christi pamoja na Baraza la Kipapa la haki na amani.

Huu ni mchango ambao umetolewa na Kardinali Peter Turkson, rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani baada ya kusoma ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki wa mkutano wa kimataifa unaojadili Mafundisho Jamii ya Kanisa Katoliki kuhusu vita na amani, ili kuanza mchakato wa kuondokana na dhana ya “vita halali na ya haki”. Mkutano huu umefunguliwa mjini Roma, hapo tarehe 11 Aprili na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 13 Aprili 2016.

Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema kwamba, vita ni unyama na kamwe haiwezi kukubalika kuwa ni sehemu ya mchakato wa kutafuta suluhu ya matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu. Hapa kuna haja ya kuwa na mwelekeo chanya zaidi utakaoisaidia Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walilitaka Kanisa kuhamasisha amani na kustawisha Jumuiya ya Kimataifa kwani amani ni kazi ya haki inayopania ustawi na mafao ya wengi.

Amani ni mchakato unaopaswa kufanyia kazi kila siku ya maisha na kwamba, Serikali zilinde na kudumisha amani na kwamba, amani ni tunda la upendo na mshikamano. Jumuiya ya Kimataifa ishinde kishawishi cha utumiaji nguvu! Wakristo wanapaswa kushiriki kikamilifu katika taasisi za kimataifa ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, udugu na majadiliano. Hili ndilo chimbuko la kuundwa kwa Baraza la Kipapa la haki na amani anasema Kardinali Turkson. Lengo ni kuchochea haki, amani na upendo wa Kristo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na kujikita katika kuhamasisha haki jamii kimataifa!

Utu na heshima ya binadamu; ustawi na mafao ya wengi; haki msingi za binadamu; usawa na mgawanyo sawa wa rasilimali na utajiri wa nchi na maendeleo endelevu! Haya ni mambo msingi ili kudumisha amani duniani. Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika maisha ya kisiasa kwani huu ni wajibu wa kimaadili. Ili kudumisha amani, Wakristo wanapaswa kuwa kweli ni chachu ya majadiliano na wote katika ukweli na uwazi. Ni haki kabisa kuzuia na kuwadhibiti watu wanaotaka kuleta fujo, vurugu na kinzani.

Kardinali Turkson anahitikisha mchango wake kwa kusema, kimsingi Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika: haki, huruma, msamaha, majadiliano mintarafu mwanga wa Injili ya amani katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.