2016-04-12 15:02:00

Askofu mkuu Christophe Pierre ateuliwa kuwa Balozi mpya wa Vatican USA!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Christophe Louis Georges Pierre kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Marekani. Hadi uteuzi huu mpya Askofu mkuu Pierre alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Mexico. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Pierre alizaliwa kunako tarehe 30 Januari 1946. Baada ya masomo na majiundo yake ya kipadre, tarehe 5 Aprili 1970 akapewa Daraja Takatifu la Upadre. Kunako mwaka 1977 akajiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican.

Taarifa zinaonesha kwamba, tangu mwaka 1977 alitekeleza utume wake nchini New Zealand, Msumbiji, Zimbabwe, Cuba na Brazil. Alikwishawahi kufanya utume wake pia kwenye Ofisi za mwakilishi wa kudumu wa Vatican mjini Geneva na Uganda. Kunako tarehe 12 Julai 1995 Papa Yohane Paulo II akamteua kuwa Askofu mkuu na kumtuma kuwa mwakilishi wa Vatican nchini Haiti. Tarehe 24 Septemba 1995 akawekwa wakfu na Kardinali Angelo Sodano.

Tarehe 22 Machi 2007, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Mexico. Askofu mkuu Christophe Pierre ndiye aliyeandaa na kukamilisha hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Mexico, sasa amepangiwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Marekani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.