2016-04-11 08:40:00

Mwalimu ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu!


Mpendwa Msikilizaji wa Radio Vatican,  tunapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, tuangazie jinsi ambavyo taaluma mbalimbali zinaweza kuimwilisha huruma ya Mungu. Kwa nafasi hii tumtazame mwalimu mwenye kumsadiki Kristo anavyoitwa naye kuitangaza huruma ya Mungu. Tutakumbuka kwamba, huruma ya Mungu humjenga mwanadamu, humlinda, humuinua na kumpa hadhi na thamani yake kama mwanadamu. Huruma ya Mungu humjalia mwanadamu mambo yaliyo mema, yenye kuchangia hali njema ya kiroho na kimwili. Ni kwa mantiki hii, sisi tunaona kwamba, kila taaluma ya mwanadamu inapaswa kulenga kuimwilisha huruma ya Mungu.

Tunapo mfikiria Mwalimu kama mjenzi wa huruma ya Mungu; tunatazama hasa lengo la taaluma yake kwa familia ya Mwanadamu. Ili kweli mwalimu aweze kutimiza vizuri wito wake na kuchangia katika safari ya ujenzi wa wasomi, anapaswa daima kuendelea kujielimisha na yeye mwenyewe pia. Asiridhike tu na yale aliyonayo kichwani. Mwalimu akisahau kujielimisha, atajikuta amepitwa na wakati. Ni sharti mwalimu ajiunde hivi ili aweze kufaa kizazi cha leo na kile kijacho; huku akilenga kumkomboa mwanadamu kiroho na kimwili.

Kwa sisi walimu tunaomsadiki Kristo, tunashiriki kazi ya Kristo mwenyewe aliye mwalimu wa kweli na wa ukweli. Kristo, aliwafundisha watu maisha adili, aliwafundisha watu juu ya tunu mbalimbali za maisha, kama vile, upendo, unyoofu, haki, huruma, uwajibikaji, uaminifu, na kuishi kwa busara. Ni kwa mambo hayo, alimjenga mwanadamu, ili aweze kuishi vema na wanadamu wenzake. Hali kadhalika, kila mwalimu anaalikwa kufundisha kwa bidii bila kusahau kurithisha kwa wanafunzi tunu hizo za utu wema, ili tuweze kupata wasomi waadilifu na wasomi wanaofaa. Wasomi hao wanaofaa, ndio haswa watachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza maumivu na mahangaiko katika maisha ya Mwanadamu.

Rai kwa walimu katika mwaka huu wa Jubilei, kulenga zaidi katika ufanisi. Tukijua kwamba waalimu tunachangia kwa kiasi kikubwa sana kujenga jamii ya kesho, basi tujibidishe kuwaandaa vema wanafunzi wetu huko madarasani, ili wakihitimu wawe wameelimika kweli. Mwalimu mwenye huruma, ni yule ambaye anamjengea mwanafunzi wake mazingira mazuri ya kesho; kwa kufundisha vizuri, ili mwanafunzi apate elimu bora na afaulu mitihani yake. Mwalimu bora hapimwi tu kwa kufaulisha mitihani wanafunzi wengi; bali hupimwa kwa uwezo wake wa kuelimisha wanafunzi. Ili mtu awe mwalimu bora anayemwakilisha Kristo aliye mwalimu wa kweli anapaswa kuzingatia yafuatayo:-

Kwanza kabisa  anapaswa kuipenda kazi ya ualimu kwa moyo wote. Kazi yoyote ile huwa njema kwa mtenda kama inafanywa kutoka moyoni. Kwa upendo huo, waalimu tujue kuwa tumekabidhiwa dhamana ya taifa la kesho. Tunaandaa wasomi na watumishi wa kesho katika sekta mbalimbali. Kikwepe kabisa kishawishi cha kutaka kujilegeza na kutafuta umaarufu kwa wanafunzi, kwa kutoweka mkazo katika mambo ya msingi. Hapo tujue kuwa tunachangia katika uangamizi wa taifa la kesho.

Pili, anapaswa kuzingatia maadili ya ualimu. Mwalimu ni mzazi, mwalimu ni kiongozi, mwalimu ni kioo, mwalimu ni dira, mwalimu pia ni kitabu. Tukumbuke kwamba, pamoja na kufundisha mambo yaliyoko katika mtaala kwa kutumia vitabu mbalimbali; wanafunzi pia wanamsoma mwalimu; wanamuiga hata namna zake za kufanya mambo. Kumbe hapa mwalimu anaalikwa kweli kuimarika kimaadili ili asadie pia kuadilisha wanafunzi wake.

Tatu, mwalimu bora ni yule anayejua kutenda kazi kwa ushirikiano na wenzake. Mtu asiyetafuta makuu, wala sifa, wala umaarufu mwepesimwepesi, wala faida yake binafsi. Tuelewe kwamba, hata kama mtu akiwa na akili na vipaji vingi kiasi gani, hawezi yeye peke yake kuwa ndiyo shule. Lazima kukubali kutenda kazi kwa ushirikiano, na kuweka mbali kila aina ya malumbano na migogoro kazini; kwani migogoro, majungu na uzushi mahali pa kazi hupunguza nguvu ya kazi na huleta mfano mbaya kwa wanafunzi.

Mwisho, tunapenda kuwaalika walimu wote, tusikose kufundisha kwa maneno na matendo juu ya tunu za utu wema. Tufanye hivyo ili tuunde wasomi wenye utu, wasomi wenye hofu ya Mungu, na wasomi wenye kujua, kujali na kulinda heshima ya mwanadamu. Ni kwa njia hiyo tu, na sisi walimu tutakuwa kweli ni vyombo vya huruma ya Mungu.

Tunakutakia baraza za Mwenyezi Mungu katika Mwaka huu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kukuletea salamu hizi kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Br. Celestin Bundu OSB, kutoka Abasia ya Roho Mtakatifu Mvimwa, Sumbawanga.








All the contents on this site are copyrighted ©.