2016-04-11 07:57:00

Kanisa linaendelea kutangaza Ujumbe wa Kristo Mfufuka!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 10 Aprili 2016, ametafakari kuhusu juu ya Yesu Kristo Mfufuka kuwatokea wafuasi wake kwa mara ya tatu wakiwa wanavua samaki kwenye Ziwa Galilaya. Baada ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu, Mitume wanarejea tena katika maisha yao ya kila siku, kwani ilikuwa ni vigumu kulifahamu Fumbo la Pasaka, kwani wengi wao walidhani kwamba, yote yalikuwa yamekwisha!

Lakini, Injili inaonesha kwamba, Yesu Mfufuka bado alikuwa anawatafuta wanafunzi wake na kuwakuta wakiwa kazini, huku wameambulia patupu baada ya kufanya kazi usiku mzima, hali inayoonesha uzoefu na mang’amuzi ya maisha yao na Yesu waliyemfahamu, wakaamua kuacha yote na kumfuasa wakiwa na matumaini makubwa, lakini sasa wanaambulia patupu! Ni kweli walishuhudia kwamba, amefufuka, lakini akatoweka na kwenda zake, kiasi cha Mitume kubaki kana kwamba, wanaota ndoto ya mchana!

Alfajiri na mapema, Yesu anajionesha mbele ya wanafunzi wake, lakini wao hawakumtambua; akawaambia watupe nyavu zao upande wa kulia! Mitume wakamwamini na matokeo yake ni kupata samaki wengi, kiasi cha kupigwa na mshangao mkuu. Yohane, mwanafunzi aliyekuwa anapendwa na Yesu, akamtambua na kumwambia Petro ni Bwana!

Mtume Petro akajifunga vazi lake na kujitupa baharini, huo ukawa ni mwanzo mpya wa furaha ya Pasaka ya Bwana ambayo ilifuta kabisa wasi wasi, simanzi na majonzi yaliyokuwa yamejikita katika nyoyo za Mitume. Uwepo wa Yesu Kristo Mfufuka ukawa ni chachu ya mabadiliko; giza likatoweka na mwanga ukang’ara; wakaona matunda ya kazi ya mikono yao; uchovu na hali ya kutelekezwa vikatoweka na wanafunzi wakaonja uwepo endelevu wa Yesu miongoni mwao! Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kwamba, hali hii ndiyo inayolihamasisha Kanisa, Jumuiya ya Kristo Mfufuka.

Wakati mwingine inaweza kuonekana kana kwamba giza la mauti na mahangaiko ya maisha ya kila siku yanazidi kushika kasi kubwa zaidi, lakini Kanisa linatambua kwa uhakika kwamba, wale wanaomwamini na kumfuasa Kristo Mfufuka wanaangaziwa mwanga na mbiu ya Pasaka ya Kristo Mfufuka inaendelea kutangazwa nyoyoni mwao kwa kuwakirimia furaha na matumaini yasiyoshindwa kamwe, kwani Kristo amefufuka kweli kweli!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata leo hii Kanisa linatangaza Mbiu ya Pasaka: furaha na matumaini yanaendelea kupita katika nyoyo, nyuso, matendo na maneno ya waamini. Wakristo wote wanahamasishwa kutangaza na kushuhudia ujumbe wa Ufufuko kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku, hususan wanaoteseka, wapweke, maskini, wagonjwa, wakimbizi na wahamiaji pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wote hawa waonje mwanga wa Kristo Mfufuka, alama ya nguvu ya huruma yake. Kristo Mfufuka awasaidie Wakristo kupyaisha imani ya Pasaka, kwa kutambua zaidi utume wao wa kutangaza na kushuhudia Injili kwa ndugu zao; awajaze Roho wake Mtakatifu, huku wakiwa wanasindikizwa na tunza pamoja na sala ya Bikira Maria na Kanisa zima waweze kutangaza ukuu wa upendo na huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.