2016-04-11 07:42:00

Dhamana na wajibu wa Taasisi ya Elimu Katoliki!


Ukweli, wema, haki na amani ni tunu msingi ambazo zinaweza kupambana fika na mwelekeo wa binadamu kutaka kumezwa sana na malimwengu, licha ya mchango mkubwa unaoletwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Haya ni mambo makubwa yanayoonekana kutawala ulimwengu mamboleo, kiasi hata cha kuongoza tamaduni na jamii katika nyakati hizi.

Hii ni sehemu ya ujumbe ambao Kardinali Pietro Parolin , Katibu mkuu wa Vatican amemwandikia Kardinali Angelo Scola, Rais wa Taasisi ya elimu ya juu ya Giuseppe Toniolo, wakati wa maadhimisho ya Siku ya 92 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, ambayo imeadhimishwa kitaifa nchini Italia, hapo tarehe 10 Aprili 2016. Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, ulimwengu mamboleo unakabiliwa na changamoto kubwa na tete zinazohitaji rasilimali watu iliyoandaliwa barabara, yenye kuonesha ukomavu na ushindani, ili kujisadaka katika mchakato wa kukabiliana na changamoto hizi katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Hapa Kardinali Parolin anawataka wadau mbali mbali kuandaa nyoyo za watu zitakaoonesha uwepo endelevu wa Kristo katika maisha yao, lakini zaidi katika uhalisia wa maisha ya watu, ili kuwa na mwelekeo mpana zaidi. Kutokana na ukweli huu, vijana wengi wa kizazi kipya wanaishi katika hali ya wasi wasi kijamii na hata katika maisha ya kiroho. Vijana hawa wana haja ya kukutana na watu, taasisi na mahali ambapo wataweza kupata mwanya wa majiundo makini na endelevu yanayomwambata mtu mzima: kiroho na kimwili, tayari kumpatia nyenzo ya majadiliano ya kweli na wazi, katika mchakato wa kuimarisha imani na akili; taaluma na taalimungu.

Kardinali Parolin anasema, Chuo kikuu cha Kikatoliki kina mchango mkubwa, ambacho muasisi wake Padre Agostino Gemelli pamoja na wasaidizi wake alionesha kama jambo msingi na muhimu katika kukuza na kudumisha mchakato wa majiundo kwa vijana wa kizazi kipya katika medani mbali mbali za maisha, ufahamu na taaluma.

Vijana wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya ubinadamu mpya unaopata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu, ili kupambana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo kwa ari na moyo mkuu, badala ya kuziona changamoto hizi kuwa ni vikwazo. Baba Mtakatifu Francisko daima anawahimiza walezi kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kikamilifu dhamana na wajibu wao ili vijana waweze, kuvutika zaidi.

Hii ni dhamana inayopaswa pia kutekelezwa na Jumuiya nzima ya Kikanisa, kielelezo makini kinachotofautisha taasisi ya elimu ya juu inayosimamiwa na kuongozwa na Kanisa Katoliki. Mchakato wa elimu inayotolewa na Kanisa, iwasaidie vijana wa kizazi kipya kujenga na kudumisha mshikamano pamoja na kutoa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, dhana inayopaswa kumwilishwa katika fani zote za elimu inayotolewa na Kanisa katika maisha ya mwanadamu, mfano hai unaoshuhudiwa na Chuo kikuu cha Mtakatifu Agostino Gemelli.

Kardinali Parolin, anahitimisha ujumbe wake kwa kuwataka wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanatoa msaada makini kwa majiundo endelevu yanayoambata chaguzi mbali mbali za maisha ya vijana, kwa kuwaangalia kwa jicho la huruma, vijana wenye akili lakini wanakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi. Ili kuwezesha watoto wa maskini kupata elimu bora, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuchangia kiasi cha fedha katika mfuko huu, ili vijana wanaotoka katika familia maskini waweze kusonga mbele katika masomo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.