2016-04-09 07:19:00

Utumwa mamboleo ni donda ndugu katika Jamii!


Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni kati ya majanga makubwa yanayomsibu mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Hivi ni vitendo dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Hivi ndivyo anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliowaandikia washiriki wa mkutano uliokuwa unajadili kuhusu biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo hivi karibuni huko New York Marekani, kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Baba Mtakatifu katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, ametumia nafasi hii kuwapongeza wajumbe wa mkutano huu, ambao wameshirikiana na Kikundi cha Mtakatifu Martha ambacho ni Mtandao wa Wakuu wa Jeshi la Polisi pamoja na Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za duniani, wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika jamii huku wakipania kung’oa kabisa ndago za biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika viongozi wa Kanisa kuwasaidia waathirika wa vitendo hivi vya kidhalimu  kwa kuwaweka katika sera na mikakati yao ya shughuli za kichungaji.

Itakumbukwa kwamba, Kikundi cha Mtakatifu Martha, Hosteli ambayo kwa sasa inatumiwa na Baba Mtakatifu Francisko kama makao yake makuu, kilikutana kwa mara ya kwanza mwezi Aprili 2014 kwa kusema kwamba, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni “donda ndugu” katika maisha ya jamii mamboleo. Kikundi hiki kimekutana mara kadhaa kunako mwaka 2014, Jijini London, Uingereza na mwaka 2015 mjini Madrid, Hispania.

Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wanachama wa Umoja wa Mataifa pamoja na wadau mbali mbali wanaoendelea kusimama kidete kupambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; uhalifu dhidi ya ubinadamu. Baba Mtakatifu anawahimiza katika tafakari yao, kuendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa ushirikiano na mawasiliano, ili kukomesha kabisa tatizo la biashara haramu ya binadamu, linalodhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa kuwageuza kuwa kama ni bidhaa sokoni!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, tatizo hili linapaswa kushughulikiwa katika ngazi mbali mbali za maisha ya kijamii; kwa kuibua mbinu mkakati wa kuzuia ili watu wasitumbukizwe katika biashara hii haramu. Hii pia ni changamoto ya Jumuiya ya Kimataifa inapojielekeza katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ifikapo mwaka 2030. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuwa imetokomeza kazi za shuruti, biashara ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na kupiga rufuku ajira za watoto wadogo; hasa wale wanaopelekwa mstari wa mbele ifikapo mwaka 2025.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake anakaza kusema, majadiliano yote haya katika ngazi mbali mbali yanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maskini wajengewe uwezo wa kupambana na maisha yao, kwani hawa ndio wahanga wakubwa wa uhalifu huu dhidi ya binadamu. Baba Mtakatifu anawahakikishia washiriki wote wa mkutano huu uwepo endelevu wa Kanisa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo sanjari na kuwahudumia waathirika wa nyanyaso hizi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.