2016-04-09 14:39:00

Umwilisho wa huruma ya Mungu katika maisha ya Mkristo!


Ndugu mahujaji wenzangu, Msingi wa imani yetu sisi Wakristo ni very simple. This is just one sentence. Sentensi moja tu! Kanuni nyingine zote za imani yetu hutegemea hii moja.

Ni kanuni gani? Ni msingi gani? Kila kitu kinachotufanya tuamini, tuwe Wakristo, tuwe Wakatoliki, tuwe na furaha na matumaini katika maisha yetu, tuwe na bidii ya kutenda mema na kuepuka mabaya na kushika kwa dhati mafundisho ya Habari Njema, kujitahidi kujirekebisha na kulinganisha maisha yetu, mawazo, maneno na matendo yetu na mfano wa Kristo mwenyewe na Maandiko Matakatifu ni ukweli huu - Yesu Kristo amefufuka, yu hai! Yeye ndiye Habari Njema tunayotangaza bila kuchoka, kwa bidii na shauku kubwa kwa takriban miaka 2000 sasa. Yesu Hai ni sababu ya kushikilia imani yetu kwa dhati na kukubali hata kumwaga damu yetu kwa moyo radhi kwa ajili ya imani hiyo. Yesu ni Nafsi, Yesu alitwaa mwili akakaa kwetu, alitukomboa kwa kafara yake msalabani, akafa, akafufuka, akabuni mbinu za kuhakikisha kwamba hata kama anarudi kwa Baba mbinguni, bado anaendelea kubaki na kuwa pamoja nasi - Mungu - Emmanueli, Mungu - Pamoja - Nasi. Huruma ya Mungu - Pamoja - Nasi.

Kila kitu tunachokifanya, mambo yote yanayounda kanuni zetu za imani - kitovu chao ni ukweli kwamba Yesu yu Hai, hafi tena, mauti haimtawali tena na anaishi miongoni mwetu mpaka mwisho wa nyakati. Hakuna Jina jingine ambalo kwalo tunapata ukombozi na uzima wa milele. Ni Yeye tu. Naye Yesu ni yule yule - jana leo na hata milele - ni Yeye tu. Nasi si watoto yatima, na wala hatujisikii kwamba Mungu wetu yuko mbali mbinguni na alituacha sisi humu ulimwenguni peke yetu tuhangaike wenyewe na kutangatanga. Hapana! Yesu yu Hai na yu pamoja nasi. Tunaweza kukutana naye, tunaweza kumsikia, tunaweza kuongea naye, tunaweza kumgusa, tunaweza kumpokea na kuwa kitu kimoja naye. Yeye yu Hai, ni Mzima, hafi tena, mauti haimtawali tena, Ufalme wake hauna mwisho, na alituahidi kwamba tutaishi milele tukiambatana naye hapa duniani. Naye ni Mkweli, na analotamka anatimiza mia kwa mia.

Ukishaamini hayo, maisha yako yatajaa furaha ya ajabu na amani ambayo haipatikani duniani hata kama ungeitafuta kwa gharama yoyote ile. Yesu yu Hai, yupo hapa, nami naweza kuwasiliana naye, kukutana naye, kumgusa, kuongea naye, kumsikia akiongea nami, kumpenda na kupendwa naye kwa upendo wake wa pekee. Yesu ni Mungu-Pamoja-Nasi. Tunaweza kukutana naye wapi? Na kuongea naye kwa njia ipi? Na kumsikia kwa namna gani? Na kuungana naye kwa mbinu gani?

I - KUSANYIKO TAKATIFU

a) Kwanza kabisa, Yesu anatueleza fumbo hili - ‘Ikiwa wawili watatu wamekusanyika kwa Jina langu, mimi nipo katikati yao…’ Kumbe, kusanyiko letu lolote ikiwa lengo lake litakuwa ni kukutana kwa Jina la Kristo Bwana wetu, basi litakuwa Kusanyiko Takatifu na Yesu Hai atakuwepo miongoni mwetu akituunganisha na kutufanya kuwa Kanisa lake Takatifu lililokusanyika mahali fulani. Tena tukiwa Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume. Tukisali pamoja kwa Jina lake, tunazungumza naye moja kwa moja, naye anatusikia na kutufundisha na kutulea kwa nguvu ya Roho Mtakatifu Mfariji, Roho Mtakatifu - Uvuvio wa Huruma ya Mungu. Ndiyo maana tunafundisha daima na kuwakumbushia waamini ukweli kwamba ibada na sala za pamoja - katika familia zetu, Jumuiya Ndogondogo za Kikristo, kanisani na kadhalika - ni muhimu mno na ni bora zaidi kuliko sala zetu binafsi. Hapo tunaweza kujihoji na kujitafiti - Je, sala za pamoja tunazipa kipaumbele katika maisha yetu ama tunazikwepa?

b) Huruma ya Mungu katika Kanisa Takatifu - Watoto wote wa Kanisa hawana budi kukumbuka ya kuwa hadhi waliyonayo haitokani na stahili yao, bali neema ya Kristo" (Mtaguso wa Pili wa Vatikano, Mwanga wa Mataifa, 14). Kwa mujibu wa maneno ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano, Kanisa ni „ishara na chombo cha wokovu“. Mungu mwenye Huruma „aliupenda mno ulimwengu hata akamtoa Mwanaye wa pekee“. Baada ya kujifanya mwanadamu, Mwana wa Mungu „alilipenda mno Kanisa na akajitoa kwa ajili yake“. Kanisa, ambalo lilizaliwa na Huruma ya Mungu, ni ishara inayoonekana ya Upendo wenye Huruma wa Mungu kwa binadamu  aliyeanguka, na ndani ya upendo huo mna   nafsi na tabia ile ile ya Yesu.

Kristo Mwenyewe „alieleza kinaganaga umuhimu wa imani na Ubatizo (taz. Mk 16:16; Yn 3:5); na kwa kufanya hivyo, alisisitiza umuhimu wa Kanisa kama mlango ambamo binadamu huingia anapobatizwa. Hivyo, wale wanaokataa makusudi kuingia au kubaki katika Kanisa, huku wakijua kwamba Kanisa Katoliki lilianzishwa na Mungu kupitia kwa Yesu kama chombo muhimu, hawataokolewa“ (Mwanga wa Mataifa, 14).

II - NENO LA MUNGU (MAANDIKO MATAKATIFU)

a) Maandiko Matakatifu ni barua ya upendo ya Mungu Baba kwetu sisi, watoto wake. Tusikilize Neno la Mungu:

Mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alipokuwa liwali wa Uyahudi, na Herode mfalme wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake, mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene, wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, Neno la Mungu lilimfikia Yohane, mwana wa Zakaria, jangwani. Akafika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi, kama ilivyoandikwa katika chuo cha maneno ya nabii Isaya, ‘Sauti ya mtu aliaye myikani, itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake. Kila bonde litajazwa, na kila mlima na kilima kitashushwa; palipopotoka patakuwa pamenyoka, na palipoparuza patalainishwa; na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu.’” (Lk 3:1-6)

Tafsiri ya kiswahili haileti maana halisi ya matini halisi ya Injili ya Luka. Tunasoma - ‘Neno la Mungu lilimfikia Yohane’. Lakini maana halisi ya sentensi hii ni zaidi - ‘Neno la Mungu limekuwa ndani ya Yohane, limetwaa mwili ndani ya Yohane, limepata mahali pa kulipukia na kutimiza malengo na kazi iliyokusudiwa na Mungu. Kumbe, Neno alilotamka Mungu karne nyingi kabla ya Yohane kuzaliwa, na Neno hilo liliandikwa na nabii Isaya katika kitabu chake, hatimaye limepata mwili na utekelezaji wake ndani ya Yohane. Neno limegeuka kuwa tukio. Neno hilo la Mungu lililongoja ndani ya Biblia Takatifu kwa muda mrefu hatimaye limempata Yohane, mtu wa Mungu aliyeweza kulipokea, kulielewa na kuliishi, na Neno hilo ndani yake limeacha kuwa Neno tu, Maandiko Matakatifu.

Neno hilo kwanza alilipokea nabii Isaya na kuliweka kwa maandishi: “Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni nyikani njia ya Bwana, nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu.” (Is 40:3) Baada ya hapo Neno lilingoja kwa zaidi ya miaka mia sita lipate kutwaa mwili ndani ya maisha ya yule aliyetabiriwa katika Neno hilo. Hatimaye Neno limetwaa nafsi ya mtu, Neno limemtwaa Yohane, na Yohane amelitwaa Neno na kulifanyia kazi. Neno la Mungu likapata maana halisi na utimilifu wake. Neno si Neno tena, Neno si maandishi tena. Neno ni tukio la kiwokovu kwa watu wote, na si kwa Yohane peke yake.

b) Somo hili linatufundisha nini?

Mungu daima anatamka Neno lake. Nyakati zote. Mungu daima anazungumza na watoto wake. Neno lake ni Kristo mwenyewe. Na daima Neno lake linawapata watu ambao ndani yao Neno hilo linakuwa tukio, tendo. Neno la Mungu pia linapata nyakati maalum na mahali pa pekee ambapo hutegemea kwamba litawakuta watu ambao wataweza kulifanyia kazi na ndani mwao na katika maisha yao Neno hilo litapata utumilifu wake, maana yake na utekelezaji wake kwa faida ya Kanisa zima.

Mwenyezi Mungu ametujalia wakati maalum kama huo sasa katika Maadhimisho ya Sherehe ya Huruma ya Mungu hapa katika Kituo cha Hija Kiabakari. Hija yetu si wakati wa kusikiliza na kutafakari Neno la Mungu tu. Hata kama wengi wanapenda kutumia msamiati huu - Padre ametulisha Neno la Mungu. Naamini kwa dhati kabisa kwamba wakati huu wa hija ni nafasi anayotujalia Mwenyezi Mungu kwa huruma yake ili katika mafundisho yote yanayotolewa katika juma lote hili, Neno fulani, Neno moja litwae mwili katika nafsi ya kila mmoja wetu na kugeuka kuwa tukio la kiwokovu katika maisha yetu na kupitia kwetu  - katika maisha ya Kanisa.

Tufanyeje basi tunapokuwa hapa wakati huu? Tumuruhusu Mungu Neno lake litutafute na litupate. Neno la Mungu lina subira. Lilimtafuta Yohane kwa karne sita lipate kutwaa mwili na kugeuka kuwa tukio ndani mwake. Tukiwa hapa Mlimani kwa Mungu wa Huruma, Neno la Mungu linatutazama kwa umakini mkubwa - kila mmoja wetu na kumtafuta mtu ambaye hatapenda kulisoma na kulistudy tu. Neno la Mungu linamtafuta mtu miongoni mwetu ambaye ataliruhusu kugeuka kuwa tukio la kiwokovu ndani mwake. Inawezekana kwamba baada ya juma zima, baada ya mfululizo wa ibada na mahubiri na mafundisho ya kila aina - Neno litarudi kwa Mungu bila mafanikio. Inawezekana. Mungu anaongea nasi kwa muda wote wa mafungo na hija yetu, lakini ni nani kati yetu atakayethubutu kuliruhusu Neno lake kumtwaa na kumtumia kwa kutimiza Mapenzi ya Mungu kama litakavyo?

c) Turudi kwenye somo la Injili ya Luka nililosoma. Inastua sana kuona kwamba katika sentensi yake ya kwanza kabisa wanatajwa wapinzani wote wa Neno la Mungu - Pontio Pilato, Herode, Filipo, Anasi, Kayafa. Hawa watu wote ndio watakaomuua Yesu wa Nazareti. Neno la Mungu hata kabla halijatwaa mwili na kugeuka kuwa tukio la kiwokovu ndani ya Yohane, tayari linakuja katika mazingira ya upinzani mkali. Neno halijatwaa mwili ndani ya Yohane na tayari limezungukwa na maadui wake. Neno ambalo linatamani kuwa tukio linajua kwamba litakutana na upinzani mkali sana.

Mt. Agostino alisema siku moja katika homilia yake juu ya ndoa: “Watu wanakataa kutenda yanayoagizwa na Neno la Mungu. Zaidi ya hayo - wanaliona Neno la Mungu kama adui wao kwa vile linatoa amri. Nami kwa sababu ninarudia Neno hilo hilo, nahofia kwamba baadhi ya watu hao wataniona na mimi kuwa adui wao. Lakini kwa vyovyote vile - hili linanihusu vipi? Mungu anayeniimarisha ananihamasisha nihubiri Neno lake pasipo hofu ya kukataliwa na watu. Walipende Neno, wasilipende, mimi nitasema tu.” (Mt. Agostino, Homilia IX juu ya ndoa, namba 3)

Ndivyo ilivyokuwa wakati ule wa Yohane. Na ndivyo itakavyokuwa wakati wa Sherehe yetu hii. Neno la Mungu linalotutafuta na linatamani lituingie na kutwaa mwili ndani mwetu na kugeuka kuwa tukio la kiukombozi, linakutana na maadui ambao ni sisi wenyewe. Si rahisi kushirikiana na Neno la Mungu lipate kutuingia na kutugeuza na kututumia kutimiza mpango wa Mungu. Ni rahisi sana kukaa na kusikiliza Neno la Mungu. Ni kazi ngumu kuliruhusu kufanya kazi ndani mwetu na kugeuka kuwa tukio katika maisha yetu. Tunaishi katika mazingira iliyojaa maadui wa Neno la Mungu. Ulimwengu wetu tunamoishi umejaa akina Pontio Pilato, Herode, Filipo. Hao wanaweza kuwa ndugu zetu wa karibu, mme wako, mke wako, watoto, viongozi wa serikali, wanasiasa, mastaa wa filamu na muziki, wapinzani wa Kanisa Takatifu, matajiri waishio hovyo kinyume cha sheria ya Mungu lakini unawaonea wivu na unatamani uwe kama wao. Hao wanaweza kuwa hata viongozi wa Kanisa kama Anasi na Kayafa - Makuhani Wakuu, mapadre, masista, viongozi wa halmashauri ya Parokia, ya JNNK na vyama vya kitume na kadhalika. Maadui wa Neno la Mungu wanaotuzunguka ni wengi mno.

Lakini kusema ukweli adui nambari wani wa Neno la Mungu ni sisi wenyewe. Ni utumwa wetu wa dhambi na shetani katika maisha yetu tunaochagua sisi wenyewe kwa hiari yetu, ni “tamaa ya macho, ni tamaa ya mwili, ni kiburi cha uzima” (taz. 1 Yn 2:16), ni minyororo mingi sana ambayo tunafungwa kwa watu, vitu, mambo na hali mbalimbali ya maisha ama tunajifunga sisi wenyewe kwa kupendwa kwetu tu. Yohane aliishi katika mazingira iliyojaa akina Pontio Pilato, Herode na wengineo. Kwake walikuwa wanakuja watu wa kila aina lakini waliofanana kwa kitu kimoja - wote walikuwa wafungwa wa dhambi na tamaa zote hizo nilizozitaja. Hakuwafuata bali aliwasaidia kwa kuwaweka huru kwa ubatizo wa toba na mafundisho sahihi ya Mungu. Kwa sababu aliruhusu Neno lililompata lifanye kazi iliyokusudiwa ndani mwake kwa ajili ya wokovu wa wote.

d) Katika Sherehe ya Huruma ya Mungu katika Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu tuliruhusu Neno la Mungu kututafuta na kutupata. Tusifikiri kwamba Neno hili litafanya kazi kiurahisi ndani mwangu na ndani mwako. Hapana. Neno litakutana na upinzani mkubwa ndani mwangu na ndani mwako. Tukumbuke lakini hatima ya Injili. Japo Herode alimuua Yohane, lakini ndiye Yohane anayeishi ndani yake Kristo daima na si Herode. Herode si kitu. Yohane ni mwalimu wa mataifa hadi sasa ndani ya Kristo na ndani ya Kanisa lake. Neno la Mungu lililotwaa mwili ndani ya nafsi yake lilimpa uzima wa milele, uzima wenye nguvu kuliko mauti.

Injili tunayohubiri ni Injili ya Matumaini. Mafungo yetu na hija ni wakati wa Matumaini. Neno la Mungu linatutafuta na likishatupata na tukishalikubali na kuliruhusu kufanya kazi ndani mwetu na pamoja nasi, litageuka kuwa maisha yetu mapya, litageuka kuwa tukio la kiwokovu, litatupa uzima wa milele wa ajabu. Hata kama tutakuwa tuleta upinzani kwa Neno hilo. Hata kama tutakuwa tunabishana nalo. Tuliruhusu Neno la Mungu kututwaa na kutwaa mwili ndani mwetu. Tumwombe Mungu iwe hivyo. Kristo - Neno wa Mungu - apate mwili ndani mwetu na kututumia kwa kutimiza kazi ya Baba. Kazi inayotupa matumaini ya kufika salama mbinguni.

III - EKARISTI TAKATIFU

a) Ekaristi Takatifu - ni njia na ni namna bora ya kukutana na Yesu wa Huruma katika Fumbo la Moyo wake Mtakatifu. Ekaristi ni Yesu mwenyewe. Unaweza kumgusa, unaweza kumbusu, unaweza kumpokea na kuwa kitu kimoja naye.

Kushiriki katika Ekaristi ni pamoja na kuishi Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo unaookoa. Ili kushiriki katika utume wa wokovu wa kimungu, binadamu anatakiwa kushiriki vema: kujitahidi kuwa na moyo safi, kutolea altareni matunda ya jasho lake, mateso, furaha na magumu ya kila siku katika maisha yake. Yaani, mtu binafsi hana budi kushirikana na Yesu katika kujitoa kwa Baba. “Hivyo, Kanisa, linatamani sana kwamba waamini wa Kristo, wanaposhiriki katika fumbo hili kuu la imani, hawapaswi kuwa kama watazamaji au wageni. Kinyume chake, kwa kuzielewa vema desturi, mapokeo na sala, hawana budi kushiriki katika tendo takatifu, wakitambua wanalofanya, kwa uchaji na kwa kushirikiana na waamini wengine. Wanapaswa kulizingatia Neno la Mungu, na kushibishwa kwa Mwili wa Bwana kwenye meza yake. Wanapaswa kumshukuru Mungu. Hawana budi kujifunza kuzitoa sadaka nafsi zao, huku wakitoa sadaka ya Mwanakondoo asiye na doa, si tu kwa mikono ya padre bali pia kwa kushirikiana naye. Siku hadi siku, kwa njia ya Kristo, aliye mshenga wetu kwa Baba, hawana budi kuunganishwa na Mungu na kuwa katika umoja kamili naye na baina yao, ili hatimaye Mungu awe yote kati ya yote” (Mtaguso wa Pili wa Vatican, Sacrosanctum Concilium, 48)

Katika Misa takatifu, Yesu anatualika kwenye meza mbili: “kwenye meza ya Neno la Mungu” na kwenye “meza ya Ekaristi”. Anapenda kuzishibisha roho za binadamu kwa Neno lake na Mwili wake. Neno la Mungu huhuisha na kuisimika imani yetu, kwani hutuelekeza katika kutenda mema. Kuupokea Mwili wa Kristo hutuwezesha kumpenda zaidi Mungu na binadamu; vile vile hutuongezea ukarimu katika kuwahudumia wengine na kuwa na ushirika nao. Mtakatifu Paulo, anasema:“ Kwa sababu mkate ni mmoja, nasi, ingawa tu wengi, tunashiriki mkate huo huo mmoja”.

Kwa kuwa Ekaristi ndiyo tunu bora, ni vigumu kuzungumzia wajibu wetu wa kushiriki katika Misa Takatifu. Mtu ambaye anatambua uwepo wa Kristo katika Misa, hana wajibu; bali ana upendo tu. Kwa hiyo, kwa mtu huyu, Misa ni jambo ambalo haliwezi kufunikwa wala kusogezwa pembeni katika ratiba yake ya kila juma. Kwa nguvu ya imani hai na tendo la Roho Mtakatifu, Ekaristi huwavuta watu kwake kwa mvuto usiokatalika. Vile vile, inauongezea moyo tamaa ya kumpenda Mungu apitaye fahamu zetu, ambaye pia hujidhiri na kujinyenyekeza kwa kutujia katika maumbo ya mkate na divai.

b) Komunyo Takatifu - “Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na kuelemewa na mizigo; nami nitawapumzisha” (Mt 11:28)

Tunashiriki kikamilifu katika Liturujia ya Misa Takatifu tunapolisikiliza Neno la Mungu kwa imani, tunapojitolea kwa Baba wa mbinguni “kwa njia ya Kristo, pamoja na Kristo na katika Kristo” na tunapoipokea Komunyo Takatifu. Katika Tafrija hii ya Kipasaka, tunampokea Bwana Yesu. Roho zetu hujazwa neema, na tunaonja mapema raha ya ufufuko mtukufu na uzima ujao. Yesu anatuhakikishia kwamba, “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, ana uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho” (Yn 6:54).

c) “Mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari” (Mt. 28:20)

 Tukishalishwa na kutiwa nguvu na Neno na Mwili wa Kristo, tunarudi katika shughuli zetu za kila siku tukiwa tumegeuka katika hulka yetu ya kuwa Wakristo. Sisi si Wakristo tu, bali ni Mitume wa Huruma ya Mungu tunaoeneza Huruma yake kwa neno, sala na matendo yetu. Ekaristi hutuwezesha kuwa Mitume wa Kristo Mfalme wa Huruma na kuwahudumia vema zaidi jirani zetu katika dunia hii, bila kujali mazingira ya maisha na kazi zetu. Maisha yetu ya kikristo yanapaswa kuongozwa na tabia hiyo ya kitume; ndiyo maana ni jambo muhimu sana kwetu kuwa karibu sana na Bwana Yesu, Mfalme wa Huruma, kama walivyotuonyesha na kutufundisha Mitume Wakuu wa Huruma ya Mungu - Mt. Sista Faustina, Mt. Yohane Paulo II na Mwenye Heri Padre Michał Sopoćko - muungamishaji na baba wa kiroho wa Sr. Faustina wakati wa uhai wake. Yesu yupo pamoja nasi wakati wote; hivyo, ni vema tuufaidi uwepo wake. Tujiunge naye katika sala, tuanze na kumaliza kila kazi pamoja naye, tumshukuru kazi zinapokamilika. Tumwendee tunapoteseka, ili tumtolee mateso hayo kwa ajili ya wokovu wetu, kwa ajili ya wokovu wa familia zetu na dnia nzima. Kwa njia ya maazimio, matendo mema, na kwa ujuzi mpendevu wa uwepo wake, kwa njia ya mambo hayo yote, kila siku ya kawaida yaweza kugeuzwa zawadi ya Huruma ya Mungu kwa ajili yetu, wakati wa kufaidi neema na mwanzo wa furaha ya milele hata hapa duniani. Hivi ndivyo Mitume Wakuu wa Huruma ya Mungu  walivyoishi, katika maisha magumu yaliyojaa uchovu, changamoto na taabu nyingi.

 

IV - NAFASI YA BIKIRA MARIA KATIKA FUMBO LA UMWILISHO WA HURUMA YA MUNGU KATIKA MAISHA YA MKRISTO

a) Tumegusia nafasi ya Mitume Wakuu wa Huruma ya Mungu katika kulielewa na kuliishi ipasavyo Fumbo la Umwilisho wa Huruma ya Mungu katika maisha ya Mkristo. Lakini katika somo hili na fumbo hili hatuwezi kumsahau Mama Bikira Maria Mtakatifu, Mama wa Yesu Kristo, Mfalme wa Huruma.

b) Njia zote tatu za Yesu-Emmanueli, Yesu - Mungu-pamoja-nasi, Yesu-Umwilisho -wa-Huruma-ya-Mungu zimetimia kikamilifu ndani mwake Mama Bikira Maria pasipo mfano. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu ni mfano bora kabisa kwetu sote na kielelezo hai cha maana yake halisi kabisa ya fumbo la “Neno kutwaa Mwili” katika maisha ya kibinadamu. Ni nini kama si Neno kutwaa mwili tumboni mwa Mama Bikira Maria na kugeuka kuwa tukio la kiwokovu kwa ajili yetu sote?

Yesu alitwaa Mwili tumboni mwake - “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana, na iwe kwangu kama ulivyosema” (Lk 1:38). Maria akawa tabernakulo ya kwanza katika historia ya dunia.

Licha ya hayo - Maria alikuwa mwanafunzi wa kwanza na msikivu kuliko wote wa Yesu - aliweka maneno na matendo yote ya Yesu moyoni mwake, na kuyawaza, kuyaelewa, kuyapenda na kuyafanyia kazi katika maisha yake yote - “Mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake” (Lk2: 51b).

Maria hazuii Neno lifanye kazi katika maisha yake peke yake. Kinyume chake - Maria, mwanafunzi bora kabisa wa Neno aliyetwaa Mwili tumboni mwake humleta Yesu kwa haraka kwa Shangazi yake Elizabeti. Naye alimsifu kwa tabia hiyo akitamka neno la sifa - ‘Naye heri aliyesadiki, kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana!” (Lk 1:45)

c) Sifa hizi za Mama Bikira Maria hatukupewa ili tuzishangae na kustaajabia tu, bali tuweze kuzitafuta na kuzilea katika nafsi zetu sisi wenyewe. Tukumbuke jibu la Yesu kwa mwanamke fulani aliyepaza sauti katika mkutano na kutamka yafuatao: “Heri tumbo lililokuzaa na matiti uliyonyonya!” Yesu alimjibu hivi: “Afadhali, heri walisikiao Neno la Mungu na kulishika” (Lk 11:27-28) Maana yake - uhuru na hadhi aliyopewa Mama Bikira Maria - tupewa na sisi katika Ubatizo Mtakatifu kama mbegu ambayo tunatakiwa kuifanyia kazi - kuiotesha katika maisha yetu ya kikristo, kuishughulika, kuilinda na kuhakikisha inazaa matunda.

d) Mungu Mwenyezi ametupatia njia kuu na za uhakika za kukutana na Mwanaye na neema zake katika maisha yetu kama Wakristo. Kusanyiko Takatifu, Neno lake Hai na Ekaristi Takatifu. Usijidanganye kwamba utaweza kuishi katika neema ya Mungu, kuiishi kama Mkristo hai endapo hutaingia katika mazingira haya Mungu aliko na kama utaendelea kukwepa njia hizi za kukutana na neema ya Kristo Hai katika maisha yako kwa kujaribu kuishi mbali na Kanisa Takatifu mahalia - Parokia yako, Jumuiya Ndogondogo ya Kikristo, jumuiya ya Mapadre, jumuiya ya Watawa.

e) Kumbuka, uhuru wetu wa Wana wa Mungu umekuja bure, bila gharama. Tumepewa uhuru huo kama tunu, kama zawadi ya Mungu katika Ubatizo Mtakatifu. Lakini bila kuishi katika uhusiano wa karibu na Yesu Kristo Hai katika maisha yetu kama Wakristo kwa kuyakita maisha hayo katika njia hizo tatu kuu, hamna jinsi - uhuru huo tutaupoteza tu na kurudi tena katika maisha ya kale ya utumwa wa dhambi.

Na PadreWojciech Adam Koscielniak

Kituo cha Hija, Jimbo Katoliki Musoma








All the contents on this site are copyrighted ©.