2016-04-09 08:09:00

Ukifanya kazi gizani utaambulia patupu!


Ndugu zangu, ulimwengu umeendelea sana kisayansi, kiuchumi hata kisiasa, nk. Kuna wataalamu, kuna watawala na wafanyakazi wakubwa wanaotumia nguvu za akili na mwili kuujenga ulimwengu huu ili uweze kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi. Katika harakati na maendeleo haya yote tungetegemea kuwa na ulimwengu wenye maisha ya raha, ya utulivu, ya amani, ya haki na upendo. Kinyume chake ulimwengu umejaa vurugu mtupu, yaani dunia imekuwa ni vurugu mechi! Patashika nguo kuchanika! Woga na wasiwasi vimekithiri. Njaa na umaskini vimepamba moto. Hapo binadamu unapigwa butwaa na kushangaa: “Kwani kuna nini kati ya binadamu na ulimwengu wake?”Zote hizi ni dalili za binadamu kukengeuka na kudhani kwamba anaweza kujitegemea kwa kumweka Mungu kandoni mwa maisha yake!

Leo utachoka zaidi kushangaa utakapowaona wafuasi wa Yesu wanavyoshangaa: Kwamba mara kadhaa baada ya ufufuko, Yesu anapojitokeza kati yao, wanamshangaa kama vile hawamjui kabisa. Waswahili husema ukitaka kushangaa nenda Manzese Bwana, huko nguo zinaanikwa bila kufuliwa! Kwa mfano katika Injili ya leo, asubuhi kweupe kabisa, “Yesu alisimama ufuoni; walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu.” Nafasi kama hizo zilitokea karibu mara tatu. Kadhalika kuhusu uvuvi wa leo eti wanashangaa, kumbe, ukifuatilia mwenyewe kwa utaratibu utagundua kuwa nafasi kama hizi za uvuvi zilishatokea kabla karibu mara tatu. Mathalani pale Petro: “aposhikwa na ushangao, yeye na wote waliokuwa pamoja naye kwa sababu ya wingi wa samaki walioupata.” (Luka5:9). Ama kweli wakati mwingine unaweza ukawadhania vibaya wafuasi hawa kuwa labda walikuwa wanaumwa ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu. Leo tunawashangaa zaidi kuwaona Mitume hawa walioishi na Yesu miaka mitatu, eti wanapanganika kwenda kuvua samaki badala ya kwenda kuhubiri Injili kama walivyoagizwa. Kushangaa huku kutusaidie kuitafakari Injili ya leo na kufaidika nayo.

Kabla kujionesha kwake leo, Yesu alishajidhihirisha tayari kwa wanafunzi wake tena ilikuwa mara mbili. Mara ya kwanza ni jioni ya siku ile ya kwanza ya juma yaani dominika, alipofufuka wanafunzi wakiwa wamejifungia chumbani bila ya Tomaso. Mara ya pili ni baada ya siku nane ilikuwa tena dominika pindi sasa yuko Tomaso.  Wakristo tungesema kwamba mara zote mbili alizojidhihirisha Yesu zilikuwa siku za dominika yaani Pasaka ndogo. Kwa kawaida dominika “Dies Domini kama inavyojulikana kwa Kinyaturu! ni Siku ya Mungu; Siku ya Kristo, Siku ya Kanisa, Siku ya Binadamu na Siku ya kutafakari mambo ya nyakati! Hii ni siku wakristo tunakusanyika kanisani kusali. Humo tunakutana na Yesu mfufuka katika Neno lake, katika komunio takatifu (Ekaristi).

Lakini usishangae kuona kwamba Yesu anajidhihirisha pia kwa wafuasi wake katikati ya juma, katika maisha ya kawaida, siku wanapojizamisha katika shughuli za kawaida. Kwa hiyo leo tunatafakarishwa jinsi ya kukutana na Yesu mfufuka siku ya kawaida tunapozama katika shughuli zetu za kila siku na mapato yake. Yaani, pindi watu wamejikita katika shughuli zao za kawaida kama za uganga, ukulima, walimu, wanafunzi, wavuvi, wafanyakazi ofisini, nk. Ndivyo inavyoanza Injili ya leo:“Baada ya hayo Yesu anajidhihirisha tena kwa wanafunzi wake penye bahari ya Tiberia.”Aidha tunaambiwa: “naye alijidhihirisha hivi.”

Mara nyingi wafanyakazi wanakuwa katika kikundi, lakini kila mmoja ana tabia yake. Ndivyo ilivyokuwa Wafuasi hawa. Walikuwa kundi la watu saba, namba inayoonesha ukamilifu kumaanisha jumuia yote inayomfuata Kristu. Lakini kila mmoja anatajwa jina: “Simoni Petro, Tomaso aitwaye Pacha na Natanaeli wa Kana ya Galilaya, wana wa Zebedayo na wengine wawili wa wanafunzi wake, walikuwapo pamoja.” Tuangalie kifupi tabia ya kila mwanajumuia ya mitume na kulinganisha na muundo wa wanajumuia zetu.

Simoni Petro, alikuwa na kichwa kigumu cha kuelewa mambo, hadi Yesu alimwitwa shetani, na aliingia kwa taabu sana katika jumuia ya Yesu. Je, katika jumuia zetu hatuna watu aina hiyo? Tomaso aliyeitwa Pacha. Huyu anampenda Yesu lakini anajitenga na jumuia, halafu anajiunga tena, yaani hakubaliani sana na jumuia yenye woga. Je, Tomaso hana pacha wake kati ya wakristu wengi wa leo?  Natanael ni mwisraeli halisi yaani ana moyo safi. Anayo mashaka mengi, lakini akitambua anachokifuata hapo anajitoa kabisa kukifuata. Je, hauingii hapa? Halafu wana wa Zebedayo Wanaitwa pia wana wa ngurumo. Wakurupukaji wakubwa. Hawakopeshi mambo, hapo unaweza kumeza au kutema, shauri yako!. Hawana uvumilivu. Walimtaka Yesu aagize moto mara moja kuangamiza wana kijiji. Je, hakuna wakristu wa mtindo huo, wakereketwa kama watoto wa Zebedeo, wakristu motomoto wenye siasa kali ya dini. Kisha kuna wafuasi wengine wawili ili kupata namba saba kamili lakini hawatajwi majina. Hawa ni wafuasi wale wasio na majina ya kikristu, yaani siyo wakristu kabisa lakini wanafuata roho ya kikristo.

Wafuasi hawa saba ndiyo waliokuwa na mang’amuzi ya kukutana na Kristu mara mbili siku ya dominika. Sasa leo wako tena pamoja katika shughuli za kawaida za kila siku. Kuonesha kwamba ilikuwa shughuli ya kawaida unamwona Petro anatoa wazo la kurudia kazini: “Mimi ninaenda kuvua samaki.” Kazi ya uvuvi inawakilisha kazi zetu za kawaida za kujikimu na maisha. Kuvua ni kama kujikwamua kutoka hali ya ngumu (bahari) ya maisha na kuyaweka katika uzima (nchi kavu) na kuyaweka sawa. Mitume wengine wanamwiga: “Sisi nasi tutakwenda nawe.” Wanaenda kuvua usiku bila mwanga kadiri ya mazoea na mang’amuzi ya kazi ya uvuvi. Mapato yake “Usiku ule hawakupata chochote.”Hawakuambulia hata chembe ya samaki; watu waliokuwa na elimu, ujuzi na maarifa ya uvuvi, leo wanatoka kapaaaa!

Sasa tufuatilie mambo yalivyokuwa kinyume chake. “Hata asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama ufuoni: walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu.” Ufuoni ni mpaka wa maji na ardhi kavu, ni sawa na hatima ya utendaji kazi kiulimwengu. Asubuhi kulipokucha kuna mwanga yaani Yesu Kristo. Amesimama yaani  mfufuka anaingilia utendaji kazi wa ulimwengu. Yesu alikwisha kufahamu kwamba mitume wake wamechemsha! Ili kuwasanifu anawauliza: “Wanangu mna kitoweo” Nao wakamjibu kikavu kikavu tu: “La!” Hapo Yesu akawaambia: “Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki.” 

Hadi hapa unaona kuna aina mbili tofauti za kufanya kazi. Aina ya kwanza ni ya kufanya usiku bila mwanga wa Injili ya Kristo na kukosa mapato. Hayo ndiyo matokeo ya shughuli za kila siku hata kama zinafanyika kwa nia njema na zinafuata mantiki ya kazi, lakini haziongozwi na Mungu. Kumbe, baada ya kukutana na Mfufuka, shughuli hiyohiyo inafanyika kwa vigezo na thamani zilizoangazwa kwa mwanga wa Neno la mfufuka, mapato yake ni makubwa na ya mastaajabu.

Kwa hiyo tukitaka kuboresha maisha, lazima tukubali kuongozwa na mantiki ya Injili yaliyojaa haki, upendo na huruma. Hiyo ndiyo sehemu nzuri inayoitwa upande wa kuume: “Litupeni jarife upande wa kuume. Hapo tutajenga jambo kubwa la maisha yaani: “nanyi mtapata.” Kisha huo wingi wa samaki unaotajwa ni ukamilifu wa  mapato: “wakapata samaki kwa wingi,” yaani kujenga utu na ubinadamu. Mfuasi yule tu anayempenda Bwana ndiye anayeweza kutambua siri ya mafanikio ya uwepo wa mfufuka. Ndiye aliyesema: “ni Bwana.”

Simon Petro baada ya kusaidiwa na mwanafunzi huyu anapata wito. Anakumbuka shuka asubuhi. Anavaa nguo na kuingia majini. Kuvaa nguo haimaanishi alikuwa uchi wa nyama, la hasha alikuwa na nguo kwani usiku kulikuwa na baridi. Tendo la kuvaa nguo lililotumika hapa kwa kigiriki ni diezōsato, maana yake ni kujitanda. Ni tendo lile lile la diezōsen kujitanda taulo alilofanya Yesu wakati wa kuwaosha miguu mitume kwenye karamu ya mwisho. Kwa hiyo baada ya kusaidiwa na mwanafunzi aliyempenda Bwana, sasa Petro anatambua anachokitaka Bwana, anaamua kujitanda vazi la kutumikia na yuko tayari kuosha miguu ya ndugu. Anajitupa majini, yaani kubatizwa na kuibuka mtu mpya aliyemvaa Kristo. Hapa Petro amefuata mawaidha ya Kristu. Wanafunzi wengine wanakusanya samaki wote 153 kama alama tu kuonesha wingi wa jumuia. Wafikapo nchi kavu wanakuta tena samaki na mkate kwenye mkaa, ni alama ya kile alichokiishi Yesu maisha yote yaani samaki na mkate ni Yesu mwenyewe ni kitafuno kilichoiva na kiko tayari kwa kuliwa. Kwa hiyo jumuiya ya kikristo inakutana na Bwana, aliyejitoa mwenyewe katika Ekaristi Takatifu. Wingi wa samaki huwakilisha mapato mazuri ya shughuli za jumuiya ya Kikristo inayofuata maelezo ya mwalimu yaani ulimwengu wa utu uliojaa furaha.

Kwa hiyo leo tunaalikwa kumtambua mfufuka na kusikiliza Neno lake siyo tu dominika, bali kila siku za kawaida, kuweka thamani ya kiutu katika kazi. Tufanye shughuli zetu katika mwanga wa Pasaka na kadiri ya Neno la Kristo. “Bwana asipoijenga nyumba, waijengao wanafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji yeye aulindaye akesha bure.”

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.