2016-04-09 07:39:00

Mchango wa mshikamano wa huruma na upendo kwa Ukraine


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu alitangaza nia maalum ya mshikamano wa upendo na huruma kwa ajili ya wananchi wa Ukraine ambao wameathirika kwa kiasi kikubwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini humo. Kutokana na nia hii, Majimbo Katoliki Ulaya, tarehe 24 Aprili 2016 yatakusanya mchango maalum kutoka kwa waamini ili kuwasaidia wananchi wa Ukraine ambao wameguswa na kutikiswa sana na athari za vita.

Mchango huu utajumlishwa na kiasi cha fedha kitakachotolewa na Baba Mtakatifu kwa ajili ya wananchi wa Ukraine kama kielelezo na ushuhuda wa matendo ya huruma yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Walengwa na wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum ndani na nje ya mipaka ya Ukraine. Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, limepewa dhamana hii ya kuratibu na kusimamia mchango huu kwa kushirikiana Tume maalum itakayokuwa imeundwa kwa ajili ya kutekeleza lengo hili.

Monsinyo Giampietro dal Toso, Katibu mkuu wa Cor Unum anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini Ukraine, mwishoni mwa mwezi Aprili, 2016. Wananchi wengi wanahitaji msaada wa chakula cha dharura; huduma makini katika sekta ya afya; maji na malazi bora zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.