2016-04-08 07:34:00

Wakatoliki na Wamethodist kutembea pamoja


Baba Mtakatifu Francisko Alhamis  kabla ya adhuhuri,  alikutana na ujumbe kutoka Baraza la Dunia la Wamethodisti, wakiongozwa na  Askofu Oliveira na Mchungaji Powell ambao walitoa salaam kwa Papa kwa niaba ya Wamethodist.  Katika hotuba yake Papa alionyesha kufurahia ugeni huu hasa akisema umemtembelea wakati muafaka, ikiwa  bado ni kipindi cha maadhimisho ya Pasaka, ambamo sherehe za Ufufuko wa Bwana bado mwangwi wake unasikika duniani.  Na kwamba wanakutana wakiwa wameunganishwa na imani moja kwa Yesu,  Bwana na Mungu aliyefufuka kutoka katika wafu. Imani ya ubatizo mmoja, wenye kuwajenga katika umoja wa kidugu waume kwa wake. Baba Mtakatifu pia aliitumia nafasi hiyo kupeleka salaam zake za matashi mema kwa dunia ya Wamethodist (Baraza la Dunia, Baraza la Ulaya na Makanisa ya Kimethodist). 

Aidha Baba Mtakatifu alipokea kwa mikono miwili taarifa ya kufunguliwa kwa Ofisi ya Kiekumeni ya  WaMethodist hapa Roma , akiitaja kuwa ni ishara ya kukua katika kukaribiana, na hasa  hamu ya wote  ya kutembea pamoja katika njia inayoelekea  umoja kamili. Papa alieleza na kuomba  Bwana abariki kazi za Ofisi hiyo , na kupafanya kuwa mahali ambapo Wakatoliki na Wamethodisti  wanaweza kukutana, na kukua katika kutathmini imani ya zingine, kusaidia makundi ya mahujaji na  wale walio katika maandalizi ya kuwa wahudumu wa kitume na viongozi wa  jumuiya  yao. Ofisi hiyo iweze pia kuwa  mahali ambapo maendeleo yaliyopatikana kwa njia ya mazungumzo  kiteolojia, yaweze kutambuliwa vyema , kupokewa na kupiga hatua mbele. Baba Mtakatifu alieleza hayo kwa kutazama matunda ya mazungumzano yaliyo fanyika kwa karibia kipindi cha miaka hamsini iliyopita.

Alionyesha matumaini yake akisema, bado kuna mengi ya kujadili kutokana na  kutofautiana katika masuala kadhaa ma hasa juu ya utoaji wa Madaraja Matakatifu na mapokeo.Hata hivyo, Makanisa haya mawili yatandelea kutembea katika njia hii ya mazungumzo kwa kuzingatia heshima na udugu  wenye kuimarisha jumuiya zote mbili. Na alirejea hati inayoandaliwa inayotazamiwa kuchapishwa baadaye mwaka huu , akisema ni  ushahidi wa wazi, unaoshuhudia  jambo hili. Na kwamba, . Wakatoliki na Wamethodisti wana mengi ya kujifunza mmoja kwa  mtu mwingine katika jinsi sisi kuelewa utakatifu na jinsi gani ya kuuishi. Na kwamba wote wana haja ya kushiriki katika mikutano inayoandaliwa , tena kukutana mara kwa mara, kama msaada katika kujuana na  kutiana moyo katika  kumtafuta Bwana na neema yake.

Aidha Papa alikumbusha katika dunia ya leo yenye  taabu na maovu mengi  pengine kuliko ilivyowahi kuwa, inakuwa ni muhimu kwa Wakristo, kutoa ushahidi wa pamoja  wakiongozwa na mwanga wa Pasaka, katika kuwa  ishara ya upendo wa Mungu uliofunuliwa katika ushindi wa  Yesu Mfufuka. Huenda upendo huu, pia kupitia huduma ya  unyenyekevu na ujasiri wa kufikia moyo na maisha ya udugu na mshikamano , unaweza kugusa mioyo ya   wengi ambao wanautafuta  upendo  hata ya kujua.  Papa alifunga hotuba yake kwa Kumshukuru Mungu , anayewapa  ushindi  wa kutembea pamoja  katika njia ya Bwana  Yesu Kristo. 








All the contents on this site are copyrighted ©.