2016-04-07 14:17:00

Papa Francisko kwenda Kisiwani Lesbos, tarehe 16 Aprili 2016


Baba Mtakatifu Francisko amekubali na kupokea mwaliko kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox pamoja na Rais Paulopoulos wa Jamhuri ya Watu wa Ugiriki na hivyo ameamua kutembelea Kisiwa cha Lesbos, Jumamosi tarehe 16 Aprili 2016. Baba Mtakatifu Francisko akiwa Kisiwani hapo, atajiunga na Patriaki Bartolomeo wa kwanza na Askofu mkuu Jerome II wa Kanisa laAthens na Ugiriki nzima kukutana na kuzungumza na wakimbizi wanaohifadhiwa Kisiwani hapo!

Akifafanua zaidi kuhusu uamuzi huu wa Baba Mtakatifu Francisko, Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Papa amekuwa akiguswa sana na mahangaiko ya maskini, wakimbizi na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii hasa kwa nyakati hizi kutokana na sababu mbali mbali. Hawa ni watu wanaopaswa kuoneshwa moyo wa upendo na mshikamano; watu wanaohitaji msaada na faraja kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu alipochaguliwa tu, safari yake ya kwanza kuifanya nje ya Vatican ilikuwa ni kutembelea Kisiwa cha Lampedusa, kilichoko kusini mwa Italia, ili kuonesha mshikamano wa upendo na huruma kwa wakimbizi na wahamiaji waliokuwa wanapoteza maisha yao kila kukicha kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania. Wengi wa wakimbizi na wahamiaji hawa ni wale wanaokimbia vita, nyanyaso, dhuluma,umaskini na kinzani za kijamii.

Padre Lombardi anasema, Ugiriki ni eneo ambalo kwa kiasi kikubwa liko chini ya Kanisa la Kiorthodox, linalosimamiwa na kuendeshwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza na Askofu mkuu Jerome II wa Kanisa la Athens na Ugiriki nzima. Uwepo wa Baba Mtakatifu ni kielelezo cha mshikamano wa kiekumene unaojikita katika matendo ya huruma na mapendo, kielelezo cha imani tendaji. Huu ni mwaliko na dhamana kwa wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanatekeleza wajibu wao barabara ili kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji hawa.

Padre Lombardi anakaza kusema, ushuhuda na mshikamano wa Baba Mtakatifu si kwa mafao ya kisiasa, bali ni sehemu ya utekelezaji wa matendo ya kiutu, kimaadili na kidini; mambo yanayowawajibisha watu wote kila mtu kadiri ya dhamana na wajibu wake ndani ya jamii husika. Hii ni changamoto kwa wanasiasa  kuhakikisha kwamba, hata wao wanatekeleza dhamana na wajibu wao katika medani za kisiasa, kwa kutafuta suluhu ambazo zinajikita katika utu na heshima ya binadamu; kwa kukazia mshikamano na watu wanaoteseka katika ulimwengu mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.