2016-04-07 11:53:00

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma kwa binadamu!


Sura ya 15 ya Injili ya Mt. Luka imo kati ya sehemu zilizo bora kabisa katika Agano Jipya. Picha na ujumbe tunaopata katika sura hii ni huruma ya pekee ya Bwana wetu Yesu Kristo. Katika sura hii tunasoma mifano mitatu au masimulizi matatu ya Huruma ya Mungu. Simulizi mojawapo - lile la Baba wa Huruma na wanaye wawili - tumekwishatafakari katika ibada yetu ya mwezi wa tatu. Leo tutazame kwa karibu na kutafakari mifano au masimulizi mawili yaliyobaki:

I - Injili ya Luka 15:1-10:

Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao. Akawaambia mfano huu, akisema, Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone? Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi. Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea. Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu. Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione? Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea. Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.

 

  1. Matabaka mbalimbali ya wadhambi

Nyakati za Yesu, matabaka manne au aina au makundi manne ya wadhambi yalikuwa yanajulikana kwa Wayahudi - kutokana na sifa zao za kimwili, kikabila, kijamii na kimaadili. Inaonekana Yesu alijihusisha na makundi yote manne ya wadhambi.

a) Tabaka la kwanza la wadhambi ni wale wenye ulemavu wa aina yoyote. Kwa Wayahudi, ulemavu wa kimwili ulisababishwa na dhambi na si kwa ugonjwa au hitilafu tu ya kimwili. Tunakumbuka katika muujiza wa Yesu aliyemponya kipofu na akaona, wafuasi wake Yesu walimhoji wakitaka kufahamu kama upofu wake ulikuwa umesababishwa na dhambi ya kipofu mwenyewe au na dhambi ya wazazi wake (taz. Yn 9:1-2).

Wayahudi waliamini kwamba Mungu peke yake anaweza kusamehe dhambi, hivyo yeyote aliyekuwa amepona au ameponywa kimuujiza, ilibidi taratibu za kutakaswa kwa mtu aliyepona au kuponywa zifanyike katika Hekalu la Yerusalemu - kwa kutambua kwamba hiyo ilikuwa ni kazi ya Mungu mwenyewe. Yesu anajitwalia mamlaka ya kuwatakasa watu kutoka katika hali ya dhambi zao - jinsi tunavyoona katika mfano wa mtu aliyepooza aliyeshushwa na watu mbele ya Yesu kupitia kwa dari iliyotobolewa nao (taz. Mk 2:3-12). Mashuhuda wa muujiza huo waliokuwepo pale walikwazwa kabisa na tendo la Yesu kumsamehe dhambi mgonjwa huyo.

b) Tabaka la pili la wadhambi ni watu wa kabila tofauti ya Wayahudi - Wasamaria na wapagani walioishi katika Nchi Takatifu. Kwa sababu hawakufuata dini ya Wayahudi, walitazamwa kama wadhambi. Walipokuwa wanaongoka na kuamini na kutahiriwa na kupokea imani ya kiyahudi, basi, walikuwa wanatakaswa kwa wongofu wao na dhambi hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Musa. Ndiyo maana Wasamaria na wapagani hawakuruhusiwa kabisa kuingia Hekaluni Yerusalemu. Yeyote aliyekiuka katazo hilo, alikuwa anauwawa kwa kupigwa mawe hadi kufa.

c) Tabaka la tatu la wadhambi ni wanajamii ya Wayahudi waliojihusisha na kazi chafu zilizokuwa zinawatia unajisi - kwa mfano - watoza ushuru. Mara nyingi kazi hiyo ya kukusanya kodi za Kaisari zilihusiana na rushwa na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Lakini Yesu alijihusisha pia na kundi hili. Tena alimteua Lawi, mwana wa Alphayo, aliyefanya kazi katika ofisi ya kutoza ushuru amfuate kama mwanafunzi wake (taz. Mk 2:14). Aidha, kwa kusisitiza kwamba wokovu wa Mungu unapatikana kwa wadhambi wa namna hii, Yesu aliwasimulia watu mfano wa Mfarisayo na Mtoza Ushuru hekaluni (taz. Lk 18:9-14). Aliyehesabiwa haki alikuwa ni mtoza ushuru!

d) Tabaka la nne la wadhambi walikuwa ni Wayahudi walioishi kinyume cha maadili ya kiyahudi - kwa mfano - majambazi, wezi na malaya. Inasadikiwa kwamba mwanamke aliyeosha miguu ya Yesu karamuni nyumbani kwa Mfarisayo, alikuwa ni mdhambi wa tabaka hili. Mfano mwingine wa mdhambi wa aina hii ni Mwanamke Msamaria ambaye Yesu aliongea naye kisimani - licha ya kuwa na waume watano kabla, aliishi na mwanaume ambaye hakuwa mme wake halali (taz. Yn 4:7-30).

Yesu anadai alitumwa na Baba wa Huruma kwa wadhambi wote na hakuna hata mmoja asiyehusika na msamaha na huruma hiyo. Na kwa sababu Yesu alitumia muda mwingi kushinda na wadhambi wa aina zote tulizozieleza, Yeye mwenyewe alituhumiwa kuwa mdhambi (taz. Yn 9:24). Lakini miujiza anayotenda Yesu inathibitisha kwamba Yeye si mdhambi, maana mdhambi hawezi kutenda miujiza. Na kwa kutumia mifano mbalimbali ya huruma, Yesu anaeleza sababu za kujihusisha kwake na wadhambi.

2. Mchungaji na Kondoo Aliyepotea

Yesu si wa kwanza aliyezungumza kuhusu uhusiano kati ya mchungaji na kondoo zake na kuutumia kama mfano wa kueleza uhusiano wa Mungu na watu wake. Kwa mfano Nabii Ezekieli anaongea kwa kirefu kuhusu uovu wa wachungaji wa Israeli na Yesu aliweza kutumia maneno yake katika mfano wake:

Neno la Bwana likanijia, kusema, Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo? Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo. Wagonjwa hamkuwatia nguvu, wala hamkuwaponya wenye maradhi, wala hamkuwafunga waliovunjika, wala hamkuwarudisha waliofukuzwa, wala hamkuwatafuta waliopotea; bali kwa nguvu na kwa ukali mmewatawala. Nao wakatawanyika, kwa sababu hapakuwa na mchungaji; wakawa chakula cha wanyama- mwitu, wakatawanyika. Kondoo zangu walitanga-tanga katika milima yote, na juu ya kila kilima kirefu; naam, kondoo zangu walitawanyika juu ya uso wote wa dunia; wala hapakuwa na mtu aliyewaulizia, wala kuwatafuta. Basi, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana; Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, kwa sababu kondoo zangu walikuwa mateka, kondoo zangu wakawa chakula cha wanyama-mwitu wote, kwa sababu hapakuwa na mchungaji, wala wachungaji wangu hawakutafuta kondoo zangu, bali wachungaji walijilisha wenyewe wala hawakuwalisha kondoo zangu; kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana; Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo zangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo zangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao.

Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia. Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo zake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo zangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza. Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu. Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli. Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU. Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.” (Eze 34:1-16)

Pamoja na unabii huo wa Ezekieli, mfano wa Yesu unashangaza. Mchungaji anaacha kondoo tisini na tisa nyikani na kuondoka kwenda kutafuta kondoo mmoja aliyepotea bila kuwa na uhakika kwamba atampata kweli. Na hapo hana hakika kama wale waliobaki nyikani peke yao bila uangalizi watakuwa salama na atawakuta atakaporudi. Hakuna mchungaji duniani mwenye akili timamu ambaye angefanya kitu hicho. Mchungaji baada ya kumpata kondoo aliyepotea, anarudi na kufanya sherehe kubwa kwa ajili ya furaha yake ya kupatikana kwa kondoo aliyepotea.

Ujumbe wa mfano huu ni kama ifuatavyo - watu wanaodhani kwamba wako salama  na hawana dhambi ni kama wale kondoo tisini na tisa. Wanaweza kufikiri aliyepotea na anayehitaji ukombozi ni yule mmoja aliyepotea wakati kwa kweli wenyewe wanahitaji msaada! Furaha ya Baba wa Huruma kwa ajili ya kumpata mwanaye mpotevu ni kubwa mno kuliko kuwa na watu ambao wanadhani wako vizuri na hawahitaji ukombozi. Mfano huu unatufundisha wazi kwamba wongofu wa mtu si mastahili yake au tunda la jitihada zake mwenyewe bali ni juhudi za Mungu mwenyewe anayemtafuta kondoo aliyepotea. Wongofu daima ni neema ya Mungu ambaye anatutafuta na kutuweka mabegani na kupeleka nyumbani kwake.

Na kwa sababu wongofu ni neema ya Mungu tunayopewa bure, tunatakiwa kuwashirikisha wengine neema hiyo. Mafarisayo na Masadukayo pamoja na waandishi walikuwa na uhuru wa kuwashirikisha wadhambi wa matabaka yote manne neema hiyo. Lakini waliibana kwa ajili yao tu. Walidhani wao wameokoka, wao ni watakatifu, wao wako salama. Wengine wote wamelaaniwa, wadhambi. Kumbe, wao ni kama kondoo tisini na tisa waliobaki nyikani bila mchungaji! Ni wazi kwamba sisi wanadamu si watiifu kama kondoo, ndiyo maana wongofu wetu unahitaji ushirikiano wetu na uhiari wetu kwa upande wa utashi wetu. Lakini pamoja na hayo - mfano wa mchungaji na kondoo aliyepotea unaonyesha wazi na kusisitiza kwamba wongofu wetu inatokana na Huruma ya Baba na ni kazi ya Mungu. Ukweli unaonekana wazi zaidi katika mfano wa pili katika sura ya 15 ya Injili ya Mt. Luka - mfano wa mwanamke na shilingi iliyopotea.

3. Mwanamke na shilingi iliyopotea

Mfano wa mwanamke aliyepoteza shilingi moja na anafanya juu chini aipate unatusaidia kuelewa vizuri zaidi ujumbe wa mfano wa mchungaji na kondoo aliyepotea.  Mfano huu kwa ujumla wake tungesema unafanana na ule uliotangulia. Tunaweza kusema kwamba shilingi kumi ni kama kondoo mia, mwanamke ni kama yule mchungaji, furaha mbinguni ni kubwa vilevile kwa ajili ya kumpata dhambi mmoja aliyeongoka. Lakini pamoja na ufanano huo, mfano huu unasisitiza juhudi kubwa kabisa na nia thabiti ya mwanamke ya kuipata ile shilingi iliyopotea ambayo thamani yake ilikuwa ndogo mno ukilinganisha na thamani ya kondoo. Wakati ule wa Yesu, shilingi moja (katika Injili ya Luka inatumika neno - drachma - fedha za Kigiriki) ilikuwa na thamani ya dinari moja ambayo ilikuwa ni posho ya kibarua kwa siku moja tu.

Japo kitu kinachotafutwa kina thamani ndogo mno ikilinganishwa na thamani ya kondoo, tunamwona mwanamke huyo akihangaika na kupekua na kufagia nyumba nzima bila kuchoka hadi kuipata tena shilingi iliyopotea! Mahangaiko na hamu ya mama huyo ya kuipata tena shilingi yake ndiyo inayoleta thamani ya pekee kwa shilingi hiyo! Na kwa sababu sarafu si kiumbe hai, ni kitu tu, basi, ujumbe na maana wa mfano huu ni mzito zaidi. Wongofu wetu hautokani na jibu letu kwa pendekezo la Mungu la kutukomboa, bali ni kazi ya neema ya Mungu mwenye Huruma peke yake!

Na zaidi tena, katika mfano huu shilingi iliyopotea haina uhusiano na shilingi nyingine alizo nazo mama huyo. Hivyo, tutafundishwa hapa kwamba kila mdhambi ana thamani kubwa kwa Mungu na hata kama angekuwa mmoja tu duniani, Mungu atafanya juu chini ili aweze kumpata na kumkomboa na kushangilia mbinguni!

4. Yesu na Jumuiya yenye sura ya Mchungaji

Tukisoma kwa makini Injili, tutakuta kwamba Yesu anajifananisha na kujitambulisha kama mchungaji mwema na mzuri - kwa mfano katika Injili ya Mt. Yohane, sura ya 10:1-16:

Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi. Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje. Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake. Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni. Mithali hiyo Yesu aliwaambia, lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia. Basi Yesu aliwaambia tena, Amin, amin, nawaambieni, Mimi ndimi mlango wa kondoo. Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho. Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. Mimi ndimi mchungaji mwema.

Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake. Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.

Kinachotufautisha mchungaji na mtu wa mshahara ni msimamo wao mbele ya hali ya hatari. Mbwa-mwitu akija - mtu wa mshahara hukimbia maana hajali hali na usalama wa kondoo. Mchungaji mwema yuko tayari hata kutoa uhai wake kwa ajili yake - kama tunavyoona katika Pasaka ya Bwana wetu. Yesu ni mchungaji mwema na mzuri anayemwaga damu yake azizi kwa ajili ya uzima wa watoto wa Mungu.

Katika Injili ya Mt. Mathayo, sura ya 18, aya ya 12 hadi 14, simulizi la mchungaji mwema linapata maana nyingine tena, maana hapo Yesu anazungumza kuhusu Kanisa lake: “Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea? Hata akipata kumwona, amin, nawaambia, amfurahia huyo zaidi, kuliko wale tisa na tisini wasiopotea. Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.”

Kabla ya swali hili aliliuliza Yesu katika sura hiyo hiyo ya 18 ya Injili ya Mt. Mathayo, Yesu alizungumza kwa msisitizo kuhusu hitaji la Kanisa na jumuiya ya waamini la kuwapokea na kuwatunza na kuwajali wadogo na wanakanisa kwa ujumla wao kuwa kama wadogo mbele ya Baba wa mbinguni:

Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na ye yote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi; bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari. Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini ole wake mtu yule aliletaye jambo la kukosesha! Basi mkono wako au mguu wako ukikukosesha, ukate ukautupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima hali umepungukiwa na mkono au mguu, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele. Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ukalitupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima una chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika jehanum ya moto. Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kukiokoa kilichopotea.]” (Mt 18:1-11)

“Haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.”

Kama Kanisa tunawajibika kutimiza agizo hili la Baba wa mbinguni - kuhakikisha hakuna hata mmoja wa wadogo kupotea. Ni jukumu letu kulifanya Kanisa kuwa na sura ya Baba wa Huruma anayemjali, kumlinda, kumlisha na kumwokoa kila mmoja wetu na kuwaweka wadogo katikati ya Kanisa lake. Jukumu hili linajumuisha kupokea na kulinda uhai wa mtoto ambaye hajazaliwa, matunzo na malezi ya watoto wadogo katika mazingira mazuri, Ubatizo wao wakiwa wadogo kabisa, katekesi katika familia, fursa za kupata elimu bora na malezi bora katika utoto wao. Mazingira ya kuwasaidia kuendeleza vipaji na karama zao. Kuwasaidia familia zao na wazazi wao kuwa na maisha ya matumaini na ajira bora. Namna na njia ni  nyingi. Ni sisi tu kujihusisha na kuwajibika. Katika Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu - ambapo Baba Mtakatifu anatuasa tukumbuke na kutenda matendo ya huruma kwa mwili na kwa roho - tunapaswa kuyaelekeza kwa mujibu wa tafakari ya Neno la Mungu ya leo kwa wadogo tulio nao.

 

Na Padre Woyciech Adam Koscielniak

Kituo cha Hija ya Huruma ya Mungu, Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.