2016-04-07 07:53:00

Muhtasari wa Injili ya Familia


Furaha ya upendo ndani ya familia “Amoris laetitia” ndiyo wosia wa kitume kutoka kwa Baba Mtakatuifu Francisko, matunda ya maadhimisho ya Sinodi mbili za Maaskofu kuhusu: wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo. Wosia huu wa kitume unazinduliwa rasmi Ijumaa tarehe 8 Aprili 2016. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu kwa muda wa mwaka mzima, amefanya tafakari kuhusu ndoa na familia. 

Leo Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukushirikisha kwa muhtasari mawazo makuu ya Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu maisha ya ndoa na familia! Mwenyezi Mungu kwa Fumbo la Umwilisho, alianza kuandika ukurasa mpya wa historia ya Ukombozi; tukio ambalo lilikita mizizi yake katika familia ya Nazareti! Yesu akazaliwa, akakua na kulelewa ndani ya familia ya binadamu! Hii ndiyo Familia Takatifu ya Yesu Maria na Yosefu.

Mtoto anapozaliwa ndani ya familia anakuwa kweli ni chemchemi ya furaha na kwamba hii ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ndani ya familia ndugu wanajifunza kupendana, kushirikiana, kuheshimiana na kusaidiana. Daima watoto wanakumbuka kwamba, katika safari ya maisha yao, wameonja huruma na ukarimu wa ndugu zao. Hili ndilo Fumbo la Umwilisho ambalo Mama Kanisa anaadhimisha kila mwaka wakati wa Sherehe za Noeli.

Ikumbukwe kwamba, mtu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Dhambi na mapungufu ya kibinadamu ndiyo chanzo kikuu cha tofauti na kinzani zinazojitokeza kati ya mwanaume na mwanamke na matokeo yake familia inakuwa si tena shule ya wema na utakatifu wa maisha, bali uwanja a fujo na vurugu! Haya ndiyo yanayojitokeza kwenye Jamii ambazo bado zinaendekeza mfumo dume na kwamba, mwanamke alionekana kuwa ni kijakazi tu, mtu asiyekuwa na thamani anasema Baba Mtakatifu.

Mwanamke amekuwa ni kichokoo ambacho vyombo vya habari vimetumia mwili wake kwa ajili ya kuuza matangazo ya biashara. Mambo haya yanaendelea kushika kasi kubwa katika ulimwengu mamboleo, kwa kutowajali wala kuwaheshimu wanawake; tofauti za kijinsia si mali kitu! Watu wanataka usawa usiozingatia kanuni maadili na utu wema; mambo msingi katika kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Tofauti kati ya mwanamke na mwanaume ni sehemu ya mpango wa Mungu, ili waweze kukamilishana na kusaidiana katika hija ya kuelekea kwenye utakatifu wa maisha!

Hapa Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja kwa jamii kujenga na kuimarisha utambuzi na heshima ya tofauti za kijinsia, vinginevyo, watoto hata wale ambao hawajazaliwa wanaweza kukiona cha mtema kuni kwani Jamii mamboleo inapenda kukumbatia sana utamaduni wa kifo. Ni wajibu na dhamana ya waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutoa ushuhuda wa Injili ya familia kwa kuonesha heshima na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia! Familia ni dira na mwongozo kwa vijana katika maisha yao ya mbeleni! Lakini, vijana wengi kwa sasa wanaogopa kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kwa kuogopa kukosea! Wanashindwa kufunga Sakramenti ya Ndoa Kanisani, kielelezo cha upendo na mshikamano kati ya Bwana na Bibi hadi mauti itakapowatenga. Kwa njia hii wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa imani.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya kutangaza Injili ya familia kwa kuonesha ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Kwa kuonesha upendo wa dhati! Hapa, Jamii inapaswa kubadilika kwa kuonesha usawa katika ajira na mishahara ya wafanyakazi wote bila kujali jinsia zao! Inasikitisha kuona kwamba, mwanamke ndiye anayeteseka zaidi katika sheria na sera kandamizi ndani ya jamii. Jamii inapaswa kutambua na kuthamini utajiri unaofumbatwa katika maisha ya wanawake na wanaume wanaokamilishana; kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto wao!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Sakramenti ya Ndoa ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha imani na upendo; kichocheo kikuu cha ushuhuda wa uzuri, upendo na utakatifu wa maisha ya ndoa kadiri ya mpango wa Mungu. Sakramenti ya Ndoa ina mwelekeo pia wa kimissionari, ili kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa baraka na neema ya Mungu kwa watu wake. Licha ya uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa, kuna familia zinazokabiliana na changamoto zinazokwenda kinyume kabisa cha Mafundisho ya Kanisa!

Kanisa linapaswa kuwasaidia wanafamilia kwa kujikita katika ukweli wa upendo, huku wakitambua kwamba, bado ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Wanafamilia hawa wanapaswa kushughulikiwa kwa hekima na busara na kwamba, hakuna njia ya mkato! Viongozi wa Kanisa wawapokee na kuwasaidia ili waweze kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa; kwa njia ya Sala, Ibada, Tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma; huku wakijikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha haki na amani!

Yesu katika maisha na utume wake alijitahidi kutoa mwaliko kwa wote, kumbe ni wajibu wa Kanisa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano kati ya familia na Jumuiya ya Kikristo, kwa kuchota neema na baraka kutoka kwa Mungu mwenyewe. Kanisa liwe daima na malango wazi, tayari kuwapokea wale wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, changamoto ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya familia. Ikumbukwe kwamba, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto nyingi tena za hatari. Familia inapaswa pia kushiriki kikamilifu katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kujikita katika ustaarabu wa binadamu hapa duniani unaoongozwa na kanuni kuu mbili: Umoja na uzazi!

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu katika maisha kwa kupitia katika Lango la Huruma ya Mungu ambaye ni Kristo Yesu! Waamini wawe na ujasiri wa kupitia Lango hili kwa njia ya toba, wongofu wa ndani na matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.